Andrew Msechu -Dodoma
BUNGE jana lilipitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba Nne wa Mwaka 2019, unaopendekeza kufanya marekebisho katika sheria 11, ikiwamo inayompa mamlaka Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), kupunguza adhabu iwapo mtuhumiwa atakiri kosa.
Awali akiwasilisha muswada huo bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, alisema katika Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo sura ya 108, marekebisho yanalenga kupanua wigo wa mfumo wa usajili wa vizazi na vifo yakijumuisha vifo vinavyotokea nje ya nchi, kutambua watendaji wa vijiji na kata kama wasajili wasaidizi baada ya kukasimiwa mamlaka na Msajili Mkuu ili kusogeza huduma karibu na jamii.
Dk. Kilangi alisema katika sheria hiyo, mabadiliko yanalenga kuongeza muda wa kubadili jina lililoandikishwa ndani ya rejesta na hati ya kuzaliwa, kupanua wigo wa usajili wa vifo vya raia wa Tanzania vinavyotokea nje ya nchi, kumpa mamlaka Msajili Mkuu kufuta jina lililoingizwa zaidi ya mara moja kwenye rejesta na kusajili kifo cha mtu anayedhaniwa kufariki baada ya kupokea amri kutoka mahakamani.
“Kifungu cha 26B kinapendekeza kuongezwa kwa lengo la kuweka masharti ya kuweka usiri wa taarifa zozote za vizazi au vifo zinazowasilishwa kwa Msajili Mkuu. Kifungu cha 26C kinapendekeza kuwekwa sharti la kutolewa kwa hati ya uasili pale Mahakama Kuu itakaporidhia uasili wa mtoto kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Dk. Kilangi alisema kwenye Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura ya 20, marekebisho yanalenga kuweka mfumo rasmi wa makubaliano ya awali ya makosa ya jinai, kati ya mwendesha mashtaka na mtuhumiwa au wakili wake, na kupunguza adhabu iwapo mtuhumiwa atakiri kosa.
Alisema katika Sheria ya Mawakili Sura ya 341, marekebisho yanakusudia kuzuia maofisa wa sheria, mawakili wa Serikali na wanasheria katika utumishi wa umma kufanya kazi za uwakili wa kujitegemea bila kibali maalumu kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Dk. Kilangi alisema katika Sheria ya Urejeshaji wa Wahalifu, Sura ya 368 marekebisho yanalenga kuboresha utaratibu wa kisheria wa ushirikiano wa kimataifa kurejesha watuhumiwa wa makosa ya jinai, kwa kumwezesha waziri mwenye dhamana kutoa hati ya kumrejesha mhalifu yeyote wa nje na kukabidhiwa kwa yeyote aliyeidhinishwa na nchi husika.
“Katika Sheria ya Mashauri Dhidi ya Serikali, Sura ya 5, marekebisho yanalenga kumtambua Wakili Mkuu wa Serikali na kumwezesha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa maelekezo kwa Wakili Mkuu wa Serikali ama kuendelea au kusitisha shauri lililofunguliwa na Serikali,” alisema.
Alisema katika Sheria ya Mahakama za Mahakimu Sura ya 11 marekebisho yanalenga kuongeza kiwango cha thamani ya fedha katika mashauri ya madai, kwa lengo la kupunguza mlundikano wa nashauri katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara.
Katika Sheria ya Taifa ya Mashtaka Sura ya 430, alisema marekebisho yanalenga kumwezesha Mkurugenzi wa Mashtaka kuanzisha utaratibu wa upatikanaji ridhaa na vibali, ili kupunguza idadi ya majalada yanayowasilishwa Makao Makuu ya Ofisi ya Mashtaka kupata ridhaa ya mkurugenzi huyo.
Katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, Dk. Kilangi alisema marekebisho yanalenga kumpa mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka kuweka utaratibu utakaotumiwa kupata idhini yake kumruhusu ofisa asiyekuwa mwendesha mashtaka kuendesha kesi zinazotokana na makosa ya rushwa.
Alisema katika Sheria ya Mapato yatokanayo na uhalifu Sura ya 256, marekebisho yanalenga kuhakikisha wahalifu hawanufaiki na mali zinazotokana na makosa ya rushwa, usafirishaji wa dawa za kulevya na utakatishaji wa fedha.
Dk. Kilangi alisema katika Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Sura ya 268, marekebisho yanalenga kuwazuia maofisa sheria au mawakili wa Serikali na mwanasheria waliopo kwenye utumishi wa umma kufanya kazi za uwakili wa kujitegemea isipokuwa kushuhudia viapo na uhakiki wa nyaraka.
“Pia, katika Sheria ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanganyika Sura ya 66 marekebisho yanalenga kuifanya itumike pande zote za Jamhuri ya Muungano na kupanua majukumu yake kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.