24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

MABADILIKO MAKUBWA BAKWATA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limefanya mabadiliko makubwa ya uongozi, ikiwamo kufuta uchaguzi wa masheikh wa mikoa na wilaya.

Kutokana na mabadiliko hayo, kuanzia sasa mashekh hao watakuwa wanateuliwa na Baraza la Ulamaa.

Akitangaza mabadiliko hayo Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka, alisema hatua hiyo imeamuliwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa baraza hilo uliofanyika Dodoma Machi 31 hadi Aprili 1, mwaka huu.

Alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuleta ufanisi katika utendaji wa Bakwata mpya, ikizingatiwa suala la kuwa mwanachama wa baraza hilo si la kadi ila ni mfumo wa maisha ya Waislamu wote wa Tanzania bila kujali madhehebu yao.

“Kuanzia sasa mfumo wa uchaguzi kwa masheikh wa mikoa na wilaya umefutwa na badala yake watakuwa wanateuliwa na Baraza la Ulamaa, ambacho ndicho chombo cha juu cha wanazuoni ndani ya Bakwata.

“Na si hilo tu, hata mfumo wa uchaguzi kwa ndani ya masheikh wa kata na maimamu nao umefutwa ila kwa maimamu watakuwa wanateuliwa na mabaraza ya Bakwata ya mikoa na wilaya kulingana na sifa za wanazuoni hao husika.

“Unaweza kusema sasa tunafanya uchaguzi wa sheikh au imamu ambaye huchaguliwa na waumini wote, sasa kwa hali hii anaweza kuchaguliwa mtu ambaye hana sifa na kujikuta mnakwenda bila utaratibu mzuri wa kuwa na viongozi,” alisema Sheikh Mataka.

Pamoja na hayo, alisema mkutano huo umethibitisha wajumbe wa Mkutano Mkuu ambao wamechaguliwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara ili kuweza kuingia kwenye Halmashauri Kuu ya Bakwata ambacho ni moja ya chombo cha juu cha uamuzi.

“Bakwata ina vyombo viwili vikubwa vya juu vya maamuzi. Kwanza kuna Baraza la Ulamaa ambalo huwa chini ya Mufti  na Sheikh Mkuu wa Tanzania na pia tuna halmashauri kuu ambayo huwa chini ya Mwenyekiti ambaye anahusika na mambo ya utawala na fedha kwa shughuli za baraza za kila siku,” alisema.

Sheikh Mataka, alisema mkutano huo umethibitisha wajumbe tisa wa Bodi ya Wadhamini walioteuliwa na Baraza la Ulamaa.

Aliwataja wajumbe hao ni Alhaj Abubakar Haji, Alhaj Omary Nzowa, Alhaj Khasimu Jezani, Dk. Najimu Msenga, Ayasir Njambaha, Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Aboud, Yusuf Manzi, Salimu Masri na Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

 

MALI ZA BAKWATA

Sheikh Mataka, alisema kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Katiba ya Bakwata, kuanzia sasa Bodi ya Wadhamini imepewa jukumu la kuhakikisha inakusanya mali zote za Waislamu sambamba na kuziandikisha kwa mujibu wa Sheria ya Wakfu na si kuuzwa kwa mali hizo.

“Bodi ya Wadhamini itakuwa na kazi ya kuhakikisha mali zote za Bakwata nchi nzima zinakuwa kwenye utaratibu, ikiwemo nyumba zote za Wakfu kwa kuziendeleza na si kuziuza.

“Kwa mabadiliko haya, tunaamini sana sasa tunakwenda kuijenga Bakwata mpya, ambayo itakuwa na manufaa kwa Waislamu wote Tanzania na si kikundi cha watu fulani,” alisema.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles