22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE CCM, UPINZANI WARARUANA BUNGENI

Na Fredy Azzah-Dodoma


WABUNGE wa upinzani na wale wa CCM  wameparurana juu ya demokrasia nchini huku mmoja akitaka Serikali ifanye mabadiliko ya Katiba nchi iwe ya chama kimoja na mwingine akidai Msajili wa Vyama vya Siasa kazi yake ni kuua upinzani.

Hali hiyo ilitokea jana   wakati wabunge hao wakichangia hoja ya Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi   ya Ofisi ya Maziri Mkuu.

Wakati wabunge hao wakisema hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alisema taarifa zinaonyesha kila wakati Chadema inaposhiriki uchaguzi matukio ya uhalifu hutokea lakini kisiposhiriki hali huwa shwari.

Ataka chama kimoja

Akitoa mchango wake, Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso (Chadema), alisema kuna jitihada za kuuwa vyama vya upinzani kwa kuvinyima haki yao ya  msingi.

Alisema ili vyama vya siasa vipate wanachama, lazima  vinadi sera zao kupitia mikutano kisha wananchi wachague kubaki walipo ama wajiunge navyo.

Wakati akiendelea kuchangia, Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM),  aliomba kutoa taarifa na kusema muda wa kunadi sera unaisha baada ya kampeni na sasa sera zinazotekelezwa ni za CCM iliyoshinda  kuongoza dola.

Baada ya mbunge huyo kuketi, Pareso alisema hana sababu ya kumjibu Mlinga.

Pareso alisema ni kulidanganya Taifa kuwaambia wananchi kwamba vyama vya siasa vinaendelea kufanya kazi vizuri huku mikutano ikiwa imekatazwa.

“Vyama vya siasa ni kama makanisa leo mtu anajiunga kesho anatoka,” alisema.

Pareso alikatishwa tena na Mbunge wa Kasulu Vijijini, Vuma Augustino (CCM), aliyesema mikutano kwa wabunge na madiwani haijazuiwa.

Akijibu taarifa hiyo, Pareso alisema yeye amejikita kwenye suala la vyama na wala hazungumzii wabunge wala madiwani.

Alisema Watanzania waliaminishwa kuwa maadui wao ni ujinga, umasikini na maradhi lakini kwa sasa vyama vya upinzani vimeongezwa kuwa adui wa nne wa wananchi.

“Nasema hivyo   kwa sababu leo  tunashuhudia wabunge na madiwani mbalimbali ama wanakamatwa, mara wanaambiwa waripoti polisi…waliowakamata wakiridhika basi wanaachilia… kila leo kuripoti polisi ama mahakamani,” alisema.

Alisema uchaguzi wa 2015 wananchi walichagua viongozi wao lakini sasa kuna wanaohama vyama kwa kurubuniwa.

Pareso alikatishwa tena na  Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) aliyesema: “Kazi ya chama chochote ikiwamo cha kwake ni kuua chama kingine kwa hiyo mimi sioni cha ajabu hapo”.

Pareso alijibu hoja hiyo kwa kusema, “Nafikiri uelewa wa mbunge ndiyo uliomfanya atoe taarifa hiyo, sioni sababu ya kumjibu”.

Akiendelea kuchangia, Pareso alisema Bunge lilitenga Sh bilioni nne   zitumike mwakilishi akifariki dunia  lakini sasa kwa sababu ya kuhamahama, Sh bilioni 6.9 zimekwisha kutumika.

“Tunajiuliza tunafanya kazi ya kuwarubuni na kuwanunua upande wa pili tunarudi tena kufanya uchaguzi huku kuna watanzania wengi hawana huduma za  msingi,”alisema.

Mbunge wa Viti Maalum,   Martha Mlata (CCM), alihoji wapizani hawakuona kuwa ni gharama kubwa zingetumika katika uchaguzi kwa kumnunua Nyalandu (Lazaro)?

Mbunge wa Tarime Vijijini, Easter Matiko (Chadema), alisema upo ushahidi  wa upande wa CCM kuwatongoza madiwani wa upinzani wahamie katika chama hicho lakini kama kuna ushahidi kuwa Chadema kilimtongoza Nyalandu ahamie Chadema basi utolewe.

Pareso akiendelea na hoja yake, alisema  kwa kiasi kikubwa uchaguzi wa marudio wa majimbo ya Siha na Kinondoni ulikuwa ni uchaguzi wa Chadema na jeshi la polisi.

Alisema ushauri wake   ni kwamba yawasilishwe bungeni marekebisho ya kufuta mfumo wa vyama vingi   dunia ijue kuwa serikali haitaki mfumo wa vyama vingi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba naye aliomba kutoa taarifa na kusema: “Uzoefu umeonyesha kuwa chama chake(Pareso)  kinaposhiriki katika uchaguzi kunakuwa na matukio mengi  ya uhalifu.

“Kuna uchaguzi mmoja ambao chama chako hakikushiriki hakukuwapo   matukio yoyote ya utekaji wala maumivu ya wananchi.”

Akijibu, Pareso alimtaka Mwigulu kwa sababu anaingia katika Baraza la Mawaziri, amwambie Rais Dk. John Magufuli afute vyama vya upinzani nchini.

Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali, (Chadema), alianza kwa kusema hekima ya upinzani imekuwa ikitafsiriwa kuwa ni uoga na upumbavu na CCM.

Alisisitiza kuwa hekima    hiyo haitalala.

Alisema kwenye Bunge lililopita, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na wenzake, walilalamika juu ya usalama wa raia ikaundwa kamati ya Bunge kuchunguza suala hilo lakini mpaka sasa hakuna taarifa iliyotolewa.

Baada ya maelezo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenister Mhagama, aliomba kutoa utaratibu kuhusu lugha ambazo zina maudhi.

“Hatuwezi sisi Serikali tuko hapa Bungeni kuwasilisha hotuba ya Waziti Mkuu, mbunge anasimama anatumia lugha za kutudhalilisha,” alisema Mhagama.

Naye Lijualikali alisisima na kusema: “Sijataka kumuudhi mtu, nimetumia neno ninaloamini si la kuudhi, kama limekuudhi nisamehe lakini naamini umenielewa,”

Alisema kwa sasa watu wanaokamatwa kwenye sheria ya mtandao ni wake wanaotoa maneno  ya kuikosoa serikali ndiyo maana jambo moja likiwekwa mtandaoni na mtu wa CCM halina shida, lakini likiwekwa na mtu wa upinzani anakamatwa.

Mbunge wa Chambani, Yusufu Salum Hussein (CUF), naye alisema Waziri Mkuu kwenye hotuba yake alisema Msajili wa Vyama vya Siasa anasimamia  vizuri, jambo ambalo yeye alilipinga.

“Mimi siamini katika hili, msajili ndiye anaua demokrasia hasa vyama vya upinzani.  Leo ndiye anaandikia barua Chadema   wajieleze kwa nini wasichukuliwe hatua kwa sababu ya kuandamana, kwani nchi hii kuandamana ni haramu?

“Yeye badala ya kusimamia vyama viende mbele anavikandimiza, ameifanyia Chadema hivyo, amepandikiza mgogoro CUF.

“Alivyo mnafiki huyuhuyu ndiye aliyemwandikia Maalim Seif (Katibu Mkuu wa CUF   Sharif Hamad) kwamba hakutakuwa na ruzuku.

“Msajili huyo huyo kamwandikia barua Lipumba kwamba hatotoa ruzuku kwa sababu chama kina mgogoro pia akamwandikia Katibu Mkuu barua hiyohiyo, lakini amempa Lipumba Sh bilioni 1.3, kama siyo unafiki ni nini?” alihoji.

Sukari ya Zanzibar

Alisema kero za Muungano zimeanza karne zilizopita, lakini hadi sasa hazijatatuliwa na kwamba hivi karibuni mawaziri wa biashara na viwanda wa Zanzibar na Bara walikutana kutatua changamoto ya sukari lakini wakashindwa.

Alisema Zanzibar kuna tani 460,000 za sukari lakini Serikali ya Muungano imeikataa na inaenda kunua Brazil.

Alisema kisingizo cha kuikataa ni kwamba  Zanzibar wananunua sukari nje wanachanganya na yao kisha kuuza Bara.

Hata hivyo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy (CCM), alimkatisha kwa kutoa taarifa kwamba kama sukari inayozalishwa Zanzibar haitoshi kwa matumizi ya Wazanzibari   iweje watake Tanzania Bara iinunue?

“Mnataka sisi tuwe jalala la wafanyabiashara wa Zanzibar kwa sukari ya magendo?” alisema.

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashantu Kijaji, alimpa taarifa Hussein akisema: “Kiwanda cha Sukari Zanzibar kina uwezo wa kuzalisha tani 8,000 za sukari kwa mwaka wakati mahitaji ya Zanzibar ni tani 17,000 mpaka tani 20,000, kwa hiyo msemaji ajielekeze kwenye hoja asipotoshe wananchi”.

Lakini Hussein aliikataa taarifa hiyo akisema  waziri anajua mambo ya fedha na siyo ya biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles