25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: Nilitumbukizwa katika siasa

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

GWIJI la siasa za upinzani nchini, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema alitumbukizwa katika siasa na kwamba ndoto yake ilikuwa ni kuwa mtumishi wa umma.

Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa  Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) kabla ya kuondoka kutokana na mgogoro wa uongozi uliokikumba chama hicho na kuhamia chama cha ACT-Wazalendo ambako kwa sasa ni mshauri wake mkuu alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano na kipindi cha Kokani kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.

Mwanasiasa huyo ambaye amepata kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema  alitumbukizwa katika siasa baada ya kumaliza chuo kikuu mwaka 1975, alipochukuliwa kuwa msaidizi wa Rais wa Serikali ya Mapinzudi ya Zanzibar wa wakati huo, Abdu Jumbe.

“Mwaka 1977 vyama viwili vikaungana, Afro Shiraz Party na Tanu ikazaliwa CCM (Chama Cha Mapinduzi), sasa katika mwaka huohuo baada ya kuungana chama bila kuulizana wala kushauriwa nikatangazwa kuwa Waziri wa Elimu na huwezi kukataa kazi.

“Mwisho wa mwaka huo kulikuwa na uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi, kwa hiyo mimi nilikwenda katika Mkutano Mkuu kwa sababu nilikuwa ni mjumbe wa Baraza la Mapinduzi ndiyo wadhifa wangu lakini sikuwa na hamu ya kugombea nafasi yoyote ndani ya chama.

“Lakini katika uchaguzi ule ukafanyika uchaguzi wa Halmashauri Kuu halafu hao viongozi wa Halmashauri Kuu wanachagua wajumbe wa Kamati Kuu. Na kwa wakati ule kwa Katiba ya CCM ilikuwa mwenyekiti wa chama ndiye anapendekeza majina nani waingie kwenye kamati kuu.

“Kwa hiyo majina yale yanapigiwa kura na wale wanaochaguliwa wanaingia, sasa wakati ule mimi niliitwa tu na mwalimu wangu Mzee Pius Msekwa (Spika Mstaafu) wakati ule ndiye alikuwa Katibu Mtendaji wa CCM, akaniita akaniambia bwana nimeagizwa na mwenyekiti ujaze fomu hii, nikauliza ya nini? Akanimbia ya ujumbe wa kamati kuu, nikamwambia sina hamu hiyo, akaniambia hakuna hamu hapa, uamuzi wa mwenyekiti jaza fomu,” alisema Maalim Seif.

Alisema baada ya kuambiwa hivyo alijaza fomu hizo akiwa na waziri mwenzake aliyemtaja kwa jina la Ali Salim ambaye pia alitakiwa kujaza fomu hizo na baada ya kuzijaza na kuziwasilisha akaondoka kurudi Unguja.

Maalim Seif alisema aliamua kurudi Unguja kuendelea na shughuli zake kwa sababu aliamini kuwa hakuna mtu yeyote aliyekuwa akimfahamu hivyo aliamini hawezi kuchaguliwa.

“Nikamwambia Ali nakwenda zangu unadhani kuna watu maarufu humu mimi na wewe tutapita, mimi nakwenda zangu Zanzibar kufanya kazi zangu.

Halmashauri Kuu ikakutana wakapiga kura usiku Mzee Msekwa akanipigia simu akaniambia kesho kuna Kamati Kuu na wewe umechaguliwa hivyo ndivyo nilivyoingia kwenye siasa,” alisema Maalim Seif.

Katika hatua nyingine mwanasiasa huyo alisema miongoni mwa mambo ambayo anayajutia ni pamoja na kushindwa kuwaambia wananchi waandamane barabarani kutokana na kile alichodai kuwa chama chake cha CUF kilishinda Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini mwaka 1995, na kwamba uamuzi huo ungewezesha matokeo halali kutangazwa.

Aidha alisema kuwa anajutia kumwamini Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, licha ya kuonywa na wazee kuwa makini naye.

“Kwa sababu tulipata maonyo kutoka kwa wazee kwamba huyu mtu mwangalieni vizuri lakini mimi bado nikaendelea kumwamini, sasa katufikisha hapa,” alisema Maalim Seif.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles