23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Mahakama yaamuru wabunge wanne Chadema wakamatwe

Mwandishi wetu-Dar es Salaam

WABUNGE wanne wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamejikuta matatani baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuamuru wakamatwa kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Wabunge hao ni John Heche (Tarime Vijijini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda).

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu Novemba 23, 2018 ambapo Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, ambao nao wanakabiliwa na kesi hiyo kufutiwa dhamana na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Mbowe na Matiko walirejea uraiani baada ya kushinda rufaa yao Mahakama Kuu Dar es Salaam, Machi 7 mwaka huu katika kesi iliyokuwa ikisikilizwa na Jaji Sam Rumanyika.

Kwa upande wanne wa safari hii, amri ya kuwakamata ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba, baada ya wabunge hao kutokuwepo mahakamani bila taarifa yoyote na wadhamini wao pia hawakuwepo.

Hakimu Simba alitoa hati ya wito wa wadhamini wa wabunge hao kujua sababu za kutowapeleka washtakiwa mahakamani.

Kabla ya kutoa amri hizo, Hakimu Simba alisema kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa, ambapo washtakiwa wengine walikuwamo lakini lakini wabunge hao wanne hadi saa 4:05 asubuhi walikuwa hawajafika mahakamani bila sababu za msingi.

Baada ya Hakimu Simba kueleza hayo wakili wa upande wa utetezi, Faraji Mangula aliyewawakilisha mawakili Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya aliieleza mahakama kuwa ana taarifa za Bulaya.

Kauli ya Mangula ilipingwa na Hakimu Simba aliyebainisha kuwa anayepaswa kuzungumza kuhusu washtakiwa kutofika mahakamani ni wadhamini na si wakili.

Katika kesi ya msingi, Mbowe na wenzake wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani, kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, Ester Bulaya ambaye ni Mbunge wa Bunda, alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16, mwaka huu barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili; Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, katika mkutano wa hadhara, mshtakiwa John Heche ambaye ni Mbunge wa Tarime Vijijini, alitoa lugha ya kuchochea chuki akitamka maneno; “Kesho patachimbika upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii… wizi unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano… watu wanapotea… watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome… .

Imedaiwa kuwa maneno hayo yalielekea kuleta chuki kati ya Serikali na Watanzania.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,712FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles