Kishasa, DRC
MAOFISA wawili wa Umoja wa Mataifa (UN) wametekwa nyara katika Mkoa wa Kasai katikati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Maafisa hao wa UN ni Michael Sharp wa Marekani na Zahida Katalan wa Sweden.
Serikali ya Kongo DRC imesema hadi sasa bado hawajawatambua watu waliowateka nyara maafisa hao.
Sharp na Katalan walikuwa miongoni mwa wataalamu wa UN wanaochunguza mizozo iliyoiathiri nchi hiyo tangu miaka ya 90.
Lambert Mende msemaji wa Serikali ya DRC ameeleza kuwa, wataalamu hao wa UN walitekwa nyara katika daraja moja katika mto Moyo na kupelekwa msituni na watekaji wasiofahamika.
Charles-Antoine Bambara msemaji wa kikosi cha kudumisha Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO) nchini humo amesema maafisa hao walitoweka Jumapili iliyopita.