Na Mwandishi Wetu
MCHEZAJI wa gofu wa Klabu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Lugalo(JWTZ), Isihaka Daudi ametwaa ubingwa wa mashindano ya Tanzania ‘Amateur Stroke Play’.
Mashindano hayo ya siku tatu yalimalizika Novemba 28,2021 kwenye viwanja vya TPC Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Daudi ambaye aliwapa changamoto wachezaji wenzake, ameshinda kwa mikwaju 210 dhidi ya Ally Mcharo aliyeshika namba mbili kwa 215 huku wa tatu akiwa ni George Sembi aliyepiga mikwaju 218 wote wakitokea TPC.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo, Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amevitaka vilabu kuendeleza vipaji vya watoto ili kuongeza chachu ya ushindani Kitaifa na Kimataifa
Kwa upande wake nahodha wa Klabu ya Gofu TPC Jaffari Ally, amezishukuru klabu zote kwa ushirikiano ambao ni bora katika kukuza uhusiano wa klabu za gofu nchini.
Washindi wengine ni divisheni A, mshindi ni Ally Mwinyi kwa mikwaju 209 akimtangulia Jaffari Omary aliyepiga 215 wote wa TPC.
Divisheni B mshindi wa kwanza ni Peter Gullo kwa mikwaju 136 akifuatiwa na Goodluck Peter 139, huku divisheni C aliyeongoza ni Isaya Kalula alipiga mikwaju 152, wote wa TPC, akifuatiwa na Boni Kiwellu wa Moshi Klabu kwa mikwaju 153.
Kwa upande wa watoto (juniors) mshindi ni John Mwinzani mikwaju 224, akimpiku Ibrahimu Gabriel mikwaju 233 wote wa TPC, wanawake mshindi ni J Daniel wa Kili Gofu mikwaju 138 akifuatiwa na Neema Olomi wa Arusha mikwaju 162.
Wachezaji wa kulipwa mshindi wa kwanza ni Frank Mwinuka kutoka Lugalo mikwaju 143, akifuatiwa na Hassan Kadio wa Dar Gymkhana 144, nafasi ya tatu ikishikwa na Nuru Mollel wa Arusha kwa mikwaju 146.