29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Sekta za mifugo SMT na SMZ zaweka mikakati ya maendeleo

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Sekta za Mifugo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia makatibu wake wakuu wamekutana na kuweka mikakati ya kuendeleza sekta hizo kwa wafugaji wa pande mbili za Muungano ambapo maazimio saba yameridhiwa ikiwa ni hatua ya kufikia malengo tarajiwa.

Maazimio hayo yamefikiwa Novemba 29, wilayani Chakechake Pemba, kwenye kikao kilichowakutanisha makatibu wakuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) wa Sekta ya Mifugo, Amosy Zephania na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Maryam Juma Sadallah.

Akifungua rasmi kikao hicho Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo (SMT) Bw. Amosy Zephania, aliishukuru Sekta ya Mifugo (SMZ) kwa maandalizi mazuri ya kikao hicho ambacho kilitanguliwa na kikao cha siku moja cha wataalamu wa sekta hizo kutoka pande mbili za Muungano na kusisitiza umuhimu wa vikao hivyo “vikao hivi tuvipe umuhimu wa kipekee ili tuweze kufanya tahmini ya maendeleo ya sekta zetu”. Alisisitiza Kaimu Katibu Mkuu.

Kaimu Katibu Mkuu pia aliongeza kuwa kwa kuendelea kushirikiana kupitia vikao na utekelezaji wa maazimio yanayoridhiwa na pande zote mbili, sekta za Mifugo zitapiga hatua na kunufaisha wananchi kiuchumi kulingana na idadi kubwa ya mifugo iliyopo nchini.

Zephania alisisitiza kuwa ni vyema wataalam wa sekta za Mifugo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kiutendaji kwa ajili ya kubadilishana uzoefu ili kupunguza au kuondoa kabisa kero na changamoto zinazowakabili wafugaji wa Tanzania.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maryam Juma Sadallah akimkaribisha Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo (SMT) Bw. Amosy Zephania, alishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) kwa kuendelea kushirikiana nao ikiwa ni pamoja na kutimiza makubaliano ya kukutana kwenye vikao kazi kama walivyokubaliana.

Aidha, Maryam aliipongeza timu ya wataalamu wa Sekta za Mifugo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa utekelezaji wa kiwango cha hali ya juu wa maazimio ya kikao kilichofanyika Juni 4, 2021 kwenye ukumbi wa TVLA jijini Dar es Salaam, “ Nawapongezeni wataalamu wetu kwa kazi nzuri mliyoifanya ingawa sio kwa asilimia mia moja lakini mmejitahidi sana,” amesema Maryam.

Aliwataka wataalamu kushirikishana kwenye mipango kazi yao ili iwe rahisi kusaidiana pia kutumia fursa zinazopatikana kwa faida ya pande mbili za Muungano akitolea mfano wa baadhi ya miradi ya miundombinu ya mifugo inayotarajiwa kujengwa Zanzibar kwa mkopo wa dola milioni 60 kutoka nchi ya Hungary.

Naye Afisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Pemba, Hakim Vuai Shein amepongeza timu ya wataalamu kwa utekelezaji wa maazimio mbalimbali na kusisitiza kuwa matarajio ya wadau wa sekta ni kuona changamoto zao zinafikia mwisho.

Baadhi ya maazimio yaliyofikiwa kwenye kikao hicho cha ushirikiano wa Sekta za Mifugo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni pamoja na kuwepo kwa makubaliano maalum kati ya Taasisi za Utafiti na Mafunzo.

Azimio lingine ni uzalishaji wa mifugo hususan mitamba ya ng’ombe chotara ambapo SMT itatoa mbegu za mifugo dozi 1,000 kwa ajili ya kiwezesha uhimilishaji kwa wafugaji wa Zanzibar.

Kufanya uchambuzi wa mnyororo wa gharama za uzalishaji wa mifugo na mazao yake na kuandaa maandiko ya miradi ya pamoja pia ni miongoni mwa maazimio yaliyoridhiwa na makatibu wakuu wa Sekta za Mifugo wa SMT na SMZ.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles