23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JWTZ yatoa onyo kwa matapeli

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limetoa onyo kwa watu wanaotapeli  vijana na wazazi wakichukua fedha na kuwalaghai  kuwa watawapatia nafasi za kujiunga na jeshi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Novemba 30,2021 kwenye Makao Makuu ya Jeshi, Upanga, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda, amesema matapeli hao wamekwenda mbali zaidi kwa kutumia jina la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo.

Luteni Kanali Ilonda, ameeleza kuwa watu hao wanachukua fedha kwa vijana na kudai wametumwa na Mkuu wa Majeshi kwa lengo la kuwapatia nafasi za kujiunga na jeshi hilo.

“Ninapenda kupitia kwenu kutoa ufafanuzi kuhusiana na vijana wanaoandikishwa kujiunga na Jeshi, ambalo ndiyo zoezi linaloendelea hivi sasa.

“Hivi karibuni Serikali yetu pendwa imetoa nafasi za kujiunga na Jeshi kwa vijana waliopo katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), nafasi hizo si za vijana wote waliopo katika makambi ya JKT. Ni nafasi chache lakini kwa wingi wake si haba.

“Nimelazimika kuongea na Vyombo vya Habari, kupitia kwenu ili kuufahamisha Umma, kwa sasa kumeanza kuibuka tabia, mwenendo na vitendo vya baadhi ya watu ambao wameanza kutumia fursa hii ya kuandikisha vijana kwa kujinufaisha.

“Wameanza vitendo vya rushwa, kuwalaghai wananchi kwamba watoe fedha ili vijana wao wapate nafasi za kujiunga Jeshi. Udanyanyifu huu unaendelea kufanyika umesababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi na wazazi ambao wana vijana wao katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa.

“Mbaya zaidi matapeli hawa, wamekwenda mbali na kusema fedha hizo anatutuma Mkuu wa Majeshi, jambo ambalo si sahihi na si sawa.  Ni Jambo ambalo kwa kweli hatuwezi kulifumbia macho kuona viongozi wetu wanachafuliwa na watu tu ambao ni wadanganyifu,” ameeleza Luteni Kanali Ilonda.

Aidha amesema kuna kundi lingine la wazazi ambao wanawafuata viongozi hasa wa jeshi kuomba  wasaidiwe vijana wao kujiunga na jeshi wakiwa na madai mbalimbali ikiwamo ya kifamilia, kiuchumi.

Amefafanua kuwa hakuna nafasi ya kuingizwa jeshini kwa kutumia mgongo wa fedha kwa sababu Jeshi la Ulinzi lina taratibu zake zilizoanishwa kisheria na kanuni na lina miongozo ya kuchukua vijana, hivyo kamwe haliandikishi vijana kwa kigezo cha fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles