25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 1, 2024

Contact us: [email protected]

Waganga tiba asili wanavyosaidia huduma afya ya uzazi Nyang’hwale

Na Yohana Shida, Geita

HUDUMA za tiba mbadala nchini, zilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1965 na kurejelewa mwaka 1990 hadi ilipotungwa Sheria ya Tiba Asili na Mbadala ya mwaka 2002.

Kutungwa kwa sheria hiyo, kulitoa fursa ya kuanzishwa kwa Baraza  la Tiba Asili na Tiba Mbadala mwaka 2005. Baraza hilo limepewa mamlaka ya kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala kwa upande wa Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa kifungu cha sheria, sehemu ya 4 ya sheria ya tiba asili na tiba mbadala namba 23 ya mwaka 2002 sehemu ya vifungu 6, 14, 22, 30 vinatoa kanuni za usajili wa tiba asili.

Kitendo cha usajili wa tiba asili umewezesha kurasimisha huduma hizo na kusaidia waganga wa tiba asili kwenye maeneo tofauti kushirikishwa katika maendeleo ya sekta ya  afya nchini.

Akizungumumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala hii, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Dk. Khadija Zegega, anasema usajili na utoaji vyeti wa tiba asili umesaidia waganga wa tiba asili kuwa mabalozi wa elimu ya afya ya uzazi.


“Jumla tuna waganga wa tiba za asili 301 kwa sasa hivi, wanaotambulika lakini waliosajiliwa ni waganga 242 kwa maana hiyo tukishawasajili huwa tunafanya nao vikao na katika vile vikao tunaelimishana kuhusu elimu mbalimbali za afya.

“Mojawapo ni kuelekezana dalili za hatari zinazoweza kujitokeza kwa wagonjwa mbalimbali hasa wajawazito, waweze kuwawahisha katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Vitalis Ndunguru, akitoa leseni kwa waganga wa tiba asili wilayani humo ambao wamesajiliwa.

“Wamama wanaojifungua kwa upasuaji wawatambue na wale wenye viashiria vya hatari wafike hospitali wapatiwe huduma stahiki,” amefafanua.

Dk. Khadija anasema waganga wanapatiwa elimu juu ya athari za kina mama kujifungua ili waweze kushirikiana nao na kuwapeleka vituo vya kutolea huduma, kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.

“Changamoto kubwa iliyopo ni kwa wale ambao hawajajisajili lakini kwa wale waliojisajili tunakwenda nao vizuri na tunawapa elimu.

“Kwa sasa tunachokifanya siyo kuwafundisha kuzalisha, tunachowafundisha ni mteja akifika kwake aweze kumleta kwenye kituo cha kutolea huduma,” anasisistiza.

Dk Khadija anasema kikubwa zaidi kinachowekewa mkazo kwenye elimu wanayopatiwa wakunga na waganga wa tiba asili ni juu ya utambuzi wa dalili za hatari kwa wajawazito.

“Kwa upande wa Nyang’hwale, kwa sasa mwitikio wa uzazi wa mpango umeendelea kuboreshwa  kwa sababu kipindi cha nyuma watu walikuwa hawaelewi umuhimu wa kutumia uzazi wa mpango,”.

Anasema elimu inayoendelea kutolewa kwa wananchi na wakunga wa jadi imeongeza mwitikio na wengi wanatumia dawa za kisasa za uzazi wa mpango na zinawasaidia pia kuweka nafasi kati ya mtoto mmoja na mwingine.

Anaeleza kwa kipindi cha nyuma watu walikuwa na imani potofu kwamba dawa za uzazi wa mpango zinaleta matatizo mbalimbali kama kansa ya vizazi lakini elimu inayotolewa imeondoa dhana hiyo.

“Sasa hivi imesaidia watoto wengi wanazaliwa bila ulemavu na mapungufu yeyote, mfano mgongo wazi unaotokana na mapungufu ya virutubisho tofauti inayopelekewa na tatizo la kuzaa mara kwa mara.

“Mama anapopumunzika kwa muda mrefu kizazi kikatulia akatumia lishe yake vizuri, haya madhara madogo madogo yatapungua.

“Uzazi ukiwa wa karibu karibu mama akipata shida kidogo ni rahisi yeye kupoteza maisha kwa hiyo kwa sasa hivi kwa Nyang’hwale hata vifo vya wajawazito vimepungua,” anasisitiza.

Mganga huyo Mkuu wa Halmashauri ya Nyang’hwale anawashauri wakunga kuendelea kuwa mabalozi wa huduma ya uzazi wa mpango kuwezesha huduma kukua zaidi ya asilimia 50.

“Huduma zipo za kutosha japokuwa bado tuna shida kubwa ya watumishi, yani hiyo ni changamoto kubwa sana, watumishi wanaotakiwa kuwepo Nyang’hwale ni asilimia 28 na upungufu ni asilimia 72,” anaeleza.

Mwenyekiti wa Waganga wa Tiba Asilia Halmashauri ya Wilaya ya Nyangwale, Bujukano Joseph, anasema ushirikiano kati yao na Ofisi ya Mganga Mkuu ni mkubwa na umesaidia sana kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

Bujukano anasema elimu wanayopatiwa kupitia semina mbalimbali imewawezesha kuelewa maana ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango na imewaongezea nguvu ya wao kuwa mabalozi wa elimu hiyo kwenye maeneo yao.

Bujukano anawaomba waganga wa tiba asilia kuendelea kufanya kazi kwa kufuata na kuzingatia maelekezo ya Serikali ikiwamo kusajiliwa na kupatiwa cheti cha utambulisho na utambuzi wa kazi zao.

Mirembe Nyanda mganga wa tiba za asili kutoka kijiji cha Kanegere, anaishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wao na kuwapatia elimu juu ya afya ya uzazi.

Anasema yeye ni mkunga na amekuwa akiwasaidia wamama wenye matatizo ya uzazi lakini anao uhitaji mkubwa wa elimu ya afya ya uzazi kuweza kuboresha huduma zaidi ingawa hadi sasa elimu waliyopewa imewasaidia kupiga hatua.

Naye Masumbuko Nyati anashukuru kwa kupata leseni itakayomwezesha kufanya kazi kwa uhuru ambapo anawashauri wengine kujiunga kupata leseni na cheti ili wapate elimu ya mambo tofauti ikiwamo afya ya uzazi na ugonjwa UKIMWI.

Juma Mabula  ni mkazi wa Nyang’hwale anakiri mbali na kutumia tiba asilia lakini amekuali kuokea uzazi wa mpango na umemusaidia kupanga idadi ya watoto anaowataka na hata kumupunguzia adha mke wake kutokujifungua kwa upasuaji.

Anasema hadi sasa ana watoto wanne pekee ambao anao uwezo wa kuwatunza na imemuwezesha kutoa huduma rafiki kwa wanaye na kumudu gharama za maisha.

Anasema uwepo wa watoto wengi ndani ya familia imekuwa kikwazo kwa familia nyingi kutofikia huduma bora na kuendelea kushadadia hali ya maisha duni mwaka hadi mwaka.

Mabula anawashauri wazazi wote kuchukulia kwa uzito wake suala la elimu ya afya ya uzazi kwani mbali na kupunguza idadi ya watoto inatoa fursa kwa mama kulea kwa amani, kufanya kazi za ziada na hata kuwa na afya njema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles