Na Salome Bruno, TUDARCo
Mashindano ya wazi ya gofu kwa wanawake (Lugalo Ladies Open 2021) yanatarajia kutimua vumbi kesho katika viwanja vya Klabu ya Gofu Lugalo, jijini Dar es Salaam.
Lengo la mashindano hayo ni kutafuta wachezaji watakaounda timu ya Taifa, itakayoshiriki mashindano ya kimataifa ya All Afrika mwaka 2022.
Akizungumzia maandalizi ya mashindano hayo, Ofisa Habari wa Klabu ya Gofu Lugalo, Kapteni Selemani Semunyu, amesema idadi ya wachezaji imefikia 100, wakiwamo nyota wa Tanzania.
“Wachezaji nyota wote wanawake Tanzania watakuwepo, mwaka huu mashindano ya Lugalo Ladies Open yatakuwa na ushindani mkubwa kutokana na aina ya wachezaji wanaoshiriki,” amesema Kapteni Semunyu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Wanawake Tanzania (TLGU), Sofia Vigo, amesema wanashiriki mashindano hayo kwa maandalizi ya kupata wachezaji wa timu ya Taifa.
“Tunaushukuru uongozi wa Lugalo kwa kazi nzuri na kuhakikisha mashindano haya yanafanyika vizuri, watakuwepo wachezaji wengine kutoka Uganda na Kenya,” amesema.