NA GEORGE KAYALA
MWIMBAJI wa nyimbo za injili nchini, Lucy Masha, amewaonya waimbaji wenzake kuishi maisha matakatifu na
kuwa kielelezo kizuri katika jamii badala ya kufanya mambo yaliyokinyume na kile wanachokiimba kwenye tungo zao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Lucy, anayetamba na albamu yake aliyoipa jina la ‘Tetea Maisha Yangu’, alisema anaumizwa anapoona waimbaji wenzake wanafanya matendo yenye machukizo mbele za Mungu na kwa mtu asiyewajua huwachukulia kama wapagani, wakati wakiwa kwenye madhabahu huigiza kama wacha Mungu
wa kweli.
“Waimbaji wengi wa nyimbo za injili wamekuwa wakifanya usanii katik huduma hiyo, maisha wanayoishi yako
tofauti na ujumbe wanaoimba kwenye albamu zao, wengi ni waasherati, wazinzi, waongo, wasengenyaji, walevi, jambo ambalo ni chukizo mbele za Mungu, hivyo wanatakiwa kubadilika kwa kuwa wao ni kioo kwa jamii,” alisema Lucy.
Aidha, mwimbaji huyo amewataka wasanii hao kuchagua njia moja, ya kumtumikia Mungu ama kuwa wapagani ili kuepuka suala la kuendelea kuitukanisha huduma ya uimbaji.