Na Waandishi Wetu – Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu wa zamani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, amemtembelea hospitali Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na kusema afya ya mwanasheria huyo inazidi kuimarika.
Jana Lowassa kwenye ukurasa wake wa twitter aliandika pia kuwa kwa sasa Tanzania inapitia wakati mgumu hivyo watu wazidi kusali.
Tangu Lissu apigwe risasi Septemba 7, Lowassa ambaye mwaka 2015 alikuwa mgombea urais wa Chadema akipeperusha bendera ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alikuwa hajazungumzia chochote juu ya tukio hilo.
Lowassa kwenye ukurasa wake huo, aliandika: “Leo nilitembelea Hospitali ya Nairobi kumuona Mbunge wetu, Rais wa TLS (Chama cha Wanasheria wa Tanganyika) na rafiki mpendwa, anaendelea vizuri.
“Ni wakati mgumu kwa Tanzania, tuendelee kusali.”
Katika ukurasa wake huo, Lowassa aliweka picha ambayo yupo na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, mke wa Lissu, Alicia Lissu na dereva wa mbunge huyo, Simon Mohamed Bakari.
KANISA KATOLIKI LATOA TAMKO
Jana tamko kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), lililosainiwa na Makamu Rais wake, Beatus Kinyaiya, limeeleza kuwa wamelaani kwa nguvu zote matendo ya vurugu, mauaji na uvunjifu wa amani yanayoendelea kutokea nchini.
“Katika taifa sasa tunashuhudia matendo ya mauaji ya watu wasio na hatia na kama ilivyokuwa kule Mkuranga, Rufiji na Kibiti, utekwaji wa watu na kuteswa, utekaji wa watoto, ulipuaji ofisi za watu moto na hivi karibuni shambulio dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
“Tunapenda kutamka wazi na kwa nguvu zetu zote kuwa vurugu na mashambulizi ya aina yeyote ile yanalifedhehesha taifa, na matendo hayo ni dhambi, ni uhalifu na si utamaduni wa Watanzania, hivyo yakomeshwe mara moja,” alisema Kinyaiya katika tamko hilo.
Alisema kuwa maaskofu wa Baraza la Katoliki wanatoa pole na kwamba wanawaombea wahanga wa vurugu hizo wote na kuwakabidhi kwa Mungu wote waliopoteza maisha.
Kinyaiya alisema wanawaombea majeruhi wapate kupona haraka na kwamba wanaamini wote walio nyuma na matukio hayo, watatafutwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
KATIBU MKUU CHADEMA AHOJIWA
Katika hatua nyingine, jana Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alihojiwa na polisi kuhusu taarifa za kupigwa risasi kwa Lissu.
Dk. Mashinji alienda polisi kutokana na wito uliotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, akimtaka kiongozi huyo na dereva wa Lissu kufika kwenye Ofisi ya Polisi ya Mkoa wa Dodoma au Ofisi ya Mpelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuhojiwa.
Hivyo jana Dk. Mashinji alifika kwa DCI saa tano asubuhi kwa mahojiano na kutoka saa tisa jioni.
Mara baada ya mahojiano, Mashinji alisema maofisa wa polisi walimuhoji juu ya waliompiga risasi Lissu na kwamba aliwajibu kuwa hawafahamu watu hao.
“Waliniuliza uliongea nini na waandishi wa habari mara baada ya kutokea kwa shambulio la Lissu? Niliwajibu kuwa turejee kwenye mazungumzo hayo ili muweze kuangalia kama nilisema nawajua wauaji au la,” alisema Mashinji.
Alisema walirejea mazungumzo hayo na kubaini kuwa hakuna sehemu yoyote aliyozungumza kama anawajua watu hao zaidi ya kuwataka wananchi kurudisha polisi jamii ili waweze kuimarisha ulinzi.
Mashinji alisema kutokana na hali hiyo, polisi walitaka kujua kama anazo taarifa zozote kuhusu tukio hilo na akawajibu kuwa hana taarifa hizo ila aliwataka kuhakikisha waliofanya tukio hilo wanasakwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.
Hata hivyo, gazeti hili lilimtafuta DCI Robert Boaz ili kujua kuhusu mahojiano hayo na idadi ya walioitikia wito huo naye akajibu: “Niko njiani naelekea Dodoma, siwezi kujua waliofika ofisini kuhojiwa.”
Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka huu, akiwa nyumbani kwake Area D (Site III), wakati akitokea bungeni mara baada ya kuahirishwa kwa kikao cha mchana.
Juzi, taarifa iliyotolewa na Chadema na kusainiwa na Mbowe, ilieleza kuwa tangu matibabu ya mbunge huyo yaanze, yameshagharimu zaidi ya Sh milioni 100.
Aidha Mbowe alisema: “Kwa mara ya kwanza, Lissu aliongea juzi (Jumamosi) jioni na mkewe Alucia na baadaye na mimi, akisema ‘Mwenyekiti, I survived to tell the tale… Please keep up the fight (Mwenyekiti, nimeokoka ili niweze kuelezea mkasa huu… tafadhali endeleza mapambano).
“Lissu ameumizwa sana, tena sana, ni ukweli usiopingika kuwa miujiza ya Mungu ni mikubwa, hata kuweza kumwokoa katika bonde la mauti.
“Kutokana na ukweli huu, matibabu yake vilevile ni maalumu na yanayohitaji wataalamu wengi, vifaa tiba maalumu na gharama kubwa na kwamba hadi sasa zaidi ya Sh. milioni 100 zimeshatumika kuokoa maisha ya ndugu yetu Lissu.”
Mwenyekiti huyo alisema kuwa fedha si kitu ila thamani ya Lissu ni kubwa kuliko kiwango chochote cha fedha hizo.
Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa kila njia iliyo halali itatumika kupata fedha za kutosha kumtibu na hatimaye kumrudisha kwenye uwanja wa kudai haki, demokrasia na ustawi kwa wote nchini.
Pamoja na hayo, Mbowe aliwashukuru Watanzania wote kwa namna wanavyoendelea kusaidia wajibu huo aliouita kuwa ni mkubwa kwa maombi na michango mbalimbali ya fedha, huku akiwataka wasichoke kuendelea kuchanga.