21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

KIGOGO ADAI WANATUMIKIA KIFUNGO MAMBOLEO

Na KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA Kanji Mwinyijuma anayeshtakiwa pamoja na vigogo wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), kwa kusababisha hasara, amedai wamefungwa kifungo mamboleo kwani tangu Machi 2016 hadi leo wako rumande na kesi haijaanza kusikilizwa.

Alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Wakili wa Serikali, Patrick Mwita kudai Jamhuri inaendelea kuandaa taarifa za kupeleka Mahakama Kuu ili kesi ianze kusikilizwa na kuomba iahirishwe hadi tarehe nyingine.

Kanji, Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Rahco, Benhardard Tito na Katibu wa kampuni hiyo, Emmanuel Masawe, wanakabiliwa na tuhuma za kula njama, matumizi mabaya ya madaraka, uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 527,540.

Akiwasilisha malalamiko mahakamani, Kanji alidai Februari 15 mwaka huu mahakama hiyo ilitoa uamuzi kwamba upelelezi unachukua muda mrefu bila sababu za msingi, lakini hadi leo wako gerezani kama tayari wameadhibiwa.

“Tunajua Mkurugenzi wa Mashaka (DPP) kaweka hati ya kuzuia dhamana na mahakama imefungwa mikono.

“Kiukweli haki yetu ya kimsingi ya kikatiba inakiukwa, hakuna sababu za msingi za kuendelea kutushikilia, wanachofanya Jamhuri si sahihi, tunaomba mahakama iingilie kati ili suala hili lifike mwisho.

“Tangu Januari 17, 2016 tulikuwa tunakwenda wenyewe kuripoti Takukuru bila shuruti na walikuwa wanasema wanafanya upelelezi.

“Machi 14, 2016 tulifikishwa mahakamani hadi leo kesi haijaanza kusikilizwa, tunaonewa… Tumefungwa kifungo mamboleo… nadhani kuna mkono wa mtu,” alidai.

Hakimu Simba alisema ujumbe uliotolewa na mshtakiwa ni mzito mna umefika kwa upande wa Jamhuri.

Baada ya kusema hayo, mahakama ilitoa siku saba hadi Septemba 18, mwaka huu kwa Jamhuri kuelezea hatua iliyofikia.

Washtakiwa katika kesi hiyo, wanadaiwa kati ya Septemba Mosi, 2014 na 30, 2015, jijini Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama ya kutenda makosa kinyume cha sheria ya Takukuru ya mwaka 2007.

Katika shtaka la pili, inadaiwa Februari 27, mwaka 2015 katika ofisi za Rahco zilizopo Ilala, Dar es Salaam, mshtakiwa Tito akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, alitumia madaraka yake vibaya kwa kuiajiri Kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited.

Inadaiwa mshtakiwa wa kwanza aliiajiri kampuni hiyo kama mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya Rahco kinyume cha sheria za manunuzi ya umma.

Katika shtaka la tatu, mshtakiwa wa kwanza na wa tatu, wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kusaini barua ya kumpitisha na kuhalalisha kampuni hiyo kutoa huduma za ushauri wa kifedha kuhusu mradi.

Shtaka la nne, inadaiwa kati ya Machi 12 na Mei 20, mwaka 2015, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, washtakiwa walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa kutimiza majukumu yao kwa kuwasilisha mkataba wa huduma ya ushauri kati ya kampuni hiyo na Rahco kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kinyume cha sheria ya manunuzi.

Shtaka la tano inadaiwa Mei 20, mwaka 2015 mshtakiwa wa kwanza na wa tatu, katika ofisi za Rahco, walitumia madaraka yao vibaya kwa kusaini mkataba kati ya kampuni hiyo na Rahco bila kibali cha Bodi ya Zabuni kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma.

Inadaiwa katika shtaka la sita kwamba kati ya Mei 20 na Juni 20, mwaka 2015 katika ofisi za Rahco, mshtakiwa wa kwanza na wa tatu, walitumia vibaya madaraka yao kwa kushindwa kuwasilisha nakala ya mkataba uliofanywa Mei 20, mwaka 2015 kwa AG na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kinyume na sheria za manunuzi ya umma.

Jamhuri ilidai katika shtaka la saba kuwa kati ya Machi na Septemba, 2015 katika ofisi ya Rahco, washtakiwa wote watatu waliisababishia Kampuni ya Rahco hasara ya Dola za Marekani 527,540 kama malipo ya awali na tozo la benki la kuhamisha.

Inadaiwa Agosti 18, mwaka 2015 katika ofisi za Rahco, mshtakiwa wa kwanza alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa zabuni ya kujenga kilomita mbili za reli ya kati kwa gharama ya Dola za Marekani 2,312,229.39 bila kibali cha Bodi ya Zabuni ya Rahco kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles