24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: WASTAAFU WENGINE WANAWASHWAWASHWA

*Asema ni tofauti na majaji, agoma kupelekewa orodha waliohukumiwa kunyongwa

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amewaponda baadhi ya viongozi wastaafu wanaosemasema kila wakati akisema kuwa wanawashwawashwa.

Ametoa mfano wa majaji wastaafu akiwaeleza kuwa  ni tofauti na wastaafu wengine na kwamba huenda kujua sheria ndiko kunakowasaidia kutokuwa waropokaji.

Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo jana wakati wa kumuapisha Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma (59), ambaye aliteuliwa juzi baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu Januari, mwaka huu.

“Nawashuruku majaji wakuu wastaafu, Barnabas Samatta na Augustino Ramadhani, walifanya kazi kubwa ya kujenga misingi ya mahakama nchini.

“Bahati nzuri majaji hawa ni waadilifu sana huwezi kumsikia Jaji Chande, Samatta, Augustino, Lubuva (Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Uchaguzi) au majaji walioko hapa.

“Ukiangalia wastaafu wa maeneo mengine hawachoki kusema, wanawashwawashwa.

“Ndiyo maana nawapongeza sana mahakama ni safi mno, nina uhakika wao wanapotaka kutoa ‘advice’ yoyote lazima wanakushirikisha ndiyo faida ya kujua sheria.

“Sisi wengine huku ambao hatujajua sheria mahali popote, chochote unaweza ukazungumza,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Kuhusu uteuzi wa jaji huyo, alisema hakushinikizwa na mtu yeyote bali alikuwa na vigezo vyake ambavyo Profesa Juma alikidhi.

“Kazi ya kumteua au kumchagua jaji mkuu ni ngumu, ni lazima ujue historia. ‘Nimeu – test’ ujaji kidogo wakati nilipokuwa nikimteua Jaji Mkuu. Sikuelewa historia nzuri ya majaji wengi, ilibidi nijipe muda wa kujiridhisha.

“Si kwamba majaji walikuwa hawafai, wote ni wazuri na wanafanya kazi nzuri. Walikuwapo wengi ambao walistahili kuwa majaji wakuu, wengine wamebakiza mwaka mmoja, miwili, mitatu na wengine wako hapa wananiangalia…nawaomba wanisamehe, lengo ni kupata jaji mkuu atakayekaa muda mrefu mpaka atakapoamua Mungu,” alisema.

Alisema katika uchambuzi alioufanya aliangalia zaidi huyo atakayemteua dhamira yake ataridhika naye kupambana na rushwa kwa sababu ni janga kubwa serikalini, mahakamani na kila mahali.

“Ndiyo maana nilitaka nipate kiongozi atakayekwenda kulisimamia hili kwa kipindi kirefu na katika kufanya uchambuzi huo Profesa Juma ali – meet qualification (alikidhi vigezo) hizo,” alisema.

Kuhusu changamoto zinazoikabili mahakama, Rais Magufuli alisema anazifahamu na zitaendelea kutatuliwa kadiri fedha zitakapopatikana.

Rais Magufuli  pia alitoa wito kwa vyombo vingine vinavyohusika na utoaji haki likiwamo Jeshi la Polisi kukutana na mahakama kujadili kwa pamoja changamoto za kuchelewesha haki za watu.

‘SITANYONGA MTU’

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema hana mpango wa kunyonga watu hivyo asipelekewe orodha ya waliohukumiwa adhabu hiyo.

“Nimeambiwa wako wengi tu wameshahukumiwa kunyongwa, naomba ile orodha wala msiniletee kwa sababu najua ugumu wake ulivyo,” alisema.

JAJI MKUU

Naye Jaji Mkuu Profesa Juma, alisema ataheshimu sheria na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

“Tutaepuka utovu wa maadili, vitendo vya rushwa na ucheleweshaji wa mashauri, kazi yetu kubwa ni kusimamia upatikanaji wa haki kwa wakati.

“Wananchi wasipokuwa na imani na mahakama na vyombo vya ulinzi na usalama hawatakuja kwetu kutatua matatizo yao.

“Sisi hatutakasirika kama tutaambiwa kuna vitendo vya rushwa lakini usitoe tuhuma ambayo haina ushahidi,” alisema Profesa Juma.

Alitaja vipaumbele vyake kuwa ni kuongeza kasi katika kusikiliza kesi za dawa za kulevya, migogoro ya wakulima na wafugaji na kesi zinazohusu miundombinu ya ujenzi wa barabara, reli na viwanda.

Kuhusu changamoto zinazoikabili mahakama, alisema kuna mradi wa maboresho ya mahakama na mpango mkakati wa mahakama ambayo yote yanalenga kuzikabili.

Alisema mwaka huu zitajengwa mahakama kuu mpya na za kisasa katika mikoa ya Kigoma, Morogoro, Mara, Singida, Dodoma na Mwanza.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, mikoa 12 kati ya 26 haina majengo ya mahakama kuu, wilaya 113 kati ya 139 ndizo zenye mahakama na kata 976 ndizo zenye mahakama kati ya kata 4,000.

“Dar es Salaam kuna kata 89, ni kata 12 tu ndizo zenye mahakama na hata majengo yaliyopo mengi yana hali mbaya.

“Nilikaa na Jaji Chande kwa saa tatu aliponikabidhi ofisi, tuna changamoto nyingi sana. Mwaka 2007 majaji walitungiwa sheria ikaangalia masilahi yao lakini jana katika salamu za pongezi nilizotumiwa watumishi wa ngazi za chini waliomba na wao tuwakumbuke,” alisema.

WAZIRI KABUDI

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema Profesa Juma ni mtiifu, muadilifu, ana akili na nidhamu ya utendaji kazi.

“Nilimfundisha Profesa Ibrahim akiwa mwaka wa kwanza, ilikuwa huwezi kwenda kufundisha bila kujiandaa vizuri kwa sababu alikuwa anakesha akisoma.

“Nilibahatika kufanya naye kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) na sehemu nyingine, kazi ya mwisho tuliyoifanya ilikuwa ni ya kupitia mfumo wa sheria na taratibu za huduma za afya nchini.

“Alitufundisha tabia ya kuanza kazi saa 11 alfajiri na tulifanya hadi jioni. Ni mpole, amejaa utii, ni mtu mwenye maadili na nidhamu ya utendaji kazi,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema tabia ya Profesa Juma ya kuwahi kazini mapema ilisababisha katibu muhtasi wake amlalamikie kwa sababu kila alipokwenda kazini alikuta bosi wake huyo amekwisha kufika.

Profesa Kabudi alisoma Zaburi ya 15 na kumtaka Profesa Juma kuizingatia wakati wote atakapokuwa katika nafasi hiyo.

Alisema tafsiri ya zaburi hiyo, ni rafiki wa Mungu ambaye ni jaji au hakimu na kwamba Ibrahim maana yake ni baba wa mataifa, lakini pia ni rafiki wa Mungu, na ni wale walioepwa ridhaa ya kuhukumu.

“Alipoteuliwa Jaji Samatta, nilimwambia akasome zaburi ya 15, Jaji Ramadhani nilimwambia akaiimbe tena kwa sababu yeye ni muimbaji. Nakuombea kwa Mwenyezi Mungu uisimamie haki ya Watanzania na utunze yale yote ambayo leo umeyatamka,” alisema.

Zaburi hiyo ilisomeka hivi ‘Bwana nani atakayekaa katika hema yako, ni nani atakayefanya maskani yake katika kinywa chako kitakatifu, ni mtu aendaye kwa ukamilifu na kutenda haki, asemaye kweli kwa moyo wake asiyesingizia kwa ulimi, wala hakumtendea mwenzie mabaya, wala hakumsengenya jirani yake, machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa lakini  huwaheshimu wamchao Bwana.

SPIKA WA BUNGE

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema atahakikisha bajeti ya kutosha inapatikana kazi za mahakama zisikwame  wananchi waweze kupata huduma ipasavyo.

“Makombora bungeni ni kitu cha kawaida lakini tutajitahidi tusiingilie uhuru wa mahakama kwa sababu mahakama ndiyo usalama wetu na matumaini ya mnyonge,” alisema Ndugai.

KAULI ZA HIVI KARIBUNI

Hivi karibuni Rais  mstaafu Jakaya Kikwete, alivionya vyama tawala barani Afrika kutovichukulia vyama vya upinzani kama adui, bali viwaone kama washindani.

Aliyasema hayo   katika Kongamano la Uongozi Barani Afrika ambako alikuwa akichangia mada ya Utawala Bora na Utawala wa Sheria, iliyowasilishwa na Profesa Barney Pityana,   Makamu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini.

Kikwete alisema kitendo cha vyama tawala kuvichukulia vyama vya upinzani kama maadui kitasababisha uadui usiokuwa na faida kwa nchi.

Aliwataka wabunge wa vyama tawala na viongozi wengine kuvikosoa vyama vyao vinapokwenda mrama, badala ya kuwa waoga na kuunga mkono mambo yote.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Mafumbo ya nini. Hayasaidii kitu , yanadharalisha viongozi waliotumikia taifa. Kama unawafahamu, kwa nini usiwaalike nyumbani ongea nao upate usuluhishi. Hata wewe mwenyewe utafaidika . Huenda watakusaidia pia namna ya kuyatatua haya.Ukiwasikiliza, utafaidika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles