NA MWANDISHI WETU - Dar es Salaam
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amesafiri jana kwenda nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi, huku akiambatana na mkewe Alicia Magabe na dereva wake, Simon Bakari aliyekuwa naye aliposhambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.
Lissu aliyeshambuliwa Septemba 7, mwaka jana, alikuwa katika Hospitali ya Nairobi, Kenya akitibiwa kwa muda wa miezi minne kabla kuruhusiwa juzi kwenda Ubelgiji kutibiwa zaidi kwa gharama ya Chadema na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Kwa mujibu wa video iliyotolewa jana na MCL Digital, Lissu, alitoa salamu za shukrani katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kabla ya kupandishwa ndani ya ndege ya Shirika la Kenya Airways iliyomsafirisha kwenda Ubelgiji kwa hatua za mwisho za matibabu na aliishukuru Serikali ya Kenya kwa kumpa ulinzi wa saa 24 kupitia askari wake akiwa hospitalini hapo.
Lissu aliyeondoka jana saa mbili asubuhi huku akiwa amevalia suti nyeusi za sare ya Chadema, alisema Wakenya wamemsaidia kuokoa maisha yake na kutokana na uangalizi waliompatia ana deni kubwa na nchi hiyo.
“Wakenya wameokoa maisha yangu, askari wao wamenilinda kwa saa 24 kila siku katika hiki kipindi cha miezi minne, ninashukuru sana Serikali ya Kenya kwa sababu askari walionilinda wameajiriwa na Serikali. Pia nawashukuru wananchi kwa sababu wafanyakazi na wauguzi wao ndio wamenitibia na kuniuguza hadi nimefikia hatua hii,” alisema.
Pia aliwashukuru Watanzania akiwamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya, kwa kuongoza jopo la madaktari wa Dodoma kumpatia huduma ya kwanza mara tu baada ya kupigwa risasi.
“Namshukuru sana Dk. Mpoki kwa bahati nzuri wakati napata haya matatizo na yeye alikuwa Dodoma, wao ndio walikuwa wa kwanza kuokoa maisha yangu,” alisema.
Pia alisema matibabu anayoenda kupata Ubelgiji ni ya hatua za mwisho na yatahusisha mazoezi ya viungo na masuala mengine madogo madogo.
“Baada ya miezi minne ya kutibiwa Nairobi Hospitali na baada ya hali ambayo ninayo, sasa naingia katika hatua ya mwisho ya kwenda kukamilisha kazi ya kuuponya huu mwili na kurudi nyumbani kuendelea na mapambano, nitasimama, nitatembea, nitarudi, mapambano yataendelea,” alisema.
Akizungumzia kuhusu kutembelewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye hivi karibuni aliahidi kwenda kumwona baada ya kumalizika sikukuu za kufunga mwaka, Lissu alisema hadi jana hakuwa amefika na anamtegemea aende kumwona Ubelgiji.
“Spika naenda kumsubiria Ubelgiji, alisema atakuja kuniona kati ya tarehe tatu au nne, leo (jana) tarehe sita naondoka hajafika, naenda kumsubiria Ubelgiji,” alisema.
Awali, kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari uwanjani hapo, Lissu aliyesindikizwa na watoto wake wawili, alizungumza na Shirika la Utangazaji la BBC kupitia Idhaa ya Kiswahili, akisema jaribio la kumuua halijamshtua na kamwe hawezi kubadili msimamo wake kwa sababu hiyo.
“Tundu Lissu ni mwanasiasa na Lissu mwenye mtazamo fulani wa kisiasa nafikiri ni yule yule, kama atabadilika, ni kwa sababu kuna mambo ambayo yatakuwa yapo wazi zaidi,” alisema.
Pia alisema kwa mtazamo wake alifikiri kuwa anapambana katika demokrasia ya vyama vingi ya kistarabu ambayo hoja inajibiwa kwa hoja.
“Tanzania baada ya hili, hoja inajibiwa kwa risasi, kwahiyo kama ni kubadili msimamo ni kubadili kwamba jamani kwenye mapambano haya hoja yako inaweza ikajibiwa, lakini badala ya kujibiwa na hoja nyingine inaweza ikajibiwa na risasi, mapanga unaweza ukapotezwa,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, alisema amefurahishwa na hatua aliyofikia Lissu kwa kuwa afya yake kwa sasa imeimarika.
“Nimefurahi kumwona kawa na afya iliyoimarika, kilichobaki ni viungo tu, kwa sisi wataalamu wa tiba si tatizo sana, sasa hivi Lisuu yule waliokuwa watu wanamjua ndiye aliyepo,” alisema.
Dk. Mashinji ambaye alimsindikiza Lissu uwanjani hapo, alisema pamoja na chama hicho kuwashukuru madaktari wa Dodoma kwa weledi waliouonyesha, lakini wamedai kuwa huduma iliyopatikana Nairobi ni funzo kwa hospitali za Afrika Mashariki.
“Katika tiba hii, ni funzo kwa nchi za Afrika Mashariki katika kuimarisha huduma zetu za afya, inatupa fursa ya kutengeneza sera madhubuti zitakazosaidia kuhakikisha huduma zetu zinakidhi mahitaji ya maeneo yetu,” alisema.
Dk. Mashinji alisema Lissu kwa sasa yupo imara na kwamba tiba anayoenda kufanyiwa Ubelgiji ni mazoezi ya viungo ili viweze kufanya kazi kama kawaida na kumjenga kisaikolokjia aweze kurudi katika hali yake ya utendaji kazi wa kila siku.
Pia aliwashukuru Watanzania waliojitokeza kuchangia matibabu ya Lissu na chama kilichofanya uamuzi wa busara na kwa wakati mwafaka kuhakikisha watu wanaoteteta masilahi mapana ya taifa wanawalinda na kuwahifadhi.
“Hali ya sasa ya mkengeuko wa demokrasia uliopo nchini unahitaji kuweka mazingira ambayo yatatoa ulinzi na usimamizi mzuri wa viongozi wetu,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika, alisema kama chama wanashukuru Mungu kwa hatua aliyofikia Lissu, lakini wapo katika harakati za kuendelea kutafuta haki zake zikiwamo matibabu na kupata taarifa za uchunguzi wa tukio hilo.
“Kwakuwa amefikia hatua hii, ni wakati wa kutafuta haki yake, haki ya matibabu tunaendelea kuitafuta, lakini pia tunatafuta haki dhidi ya wale waliomfanyia jaribio la mauaji,” alisema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uenezi wa Chadema, Hemed Ali, alisema hatua aliyofikia Lissu kwa sasa ni kushukuru kwa kuwa alimpokea huku mwili wake ukiwa na shaka.
“Nimempokea Lissu mashaka yalikuwa mengi katika mwili wake, lakini kupitia yeye nimeona miujiza ya Mungu, kipindi chote cha miezi minne kimenipa ujasiri mkubwa katika mapambanio ya haki na demokrasia,” alisema.
Hemed alisema alikuwa akimuhudumia Lissu huku akiwa katika darasa la kupata moyo na ujasiri katika mapambano ya kidemokrasia.
“Kwakweli ulikuwa wakati ambao una mafunzo, huzuni na faraja kubwa, lakini faraja yote Mungu ametia mkono wake kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili (Chadema), aliyempa Lissu zawadi ya shuka la kimasai pamoja na mkewe kama ishara ya kumtunuku ushujaa, alisema anaamini kupona kwake kuna mkono wa Mungu.
“Kwa majeraha makubwa kama yale, naamini Mungu ameweka mkono wake, alisema tuchape kazi, anarejea mimi nimempa shuka, lile shuka ni zawadi, lile ni kwa ajili ya mtu jasiri na katika mila ya kwetu ile inatumika kama godoro, nimempa zawadi kama shujaa wetu na ataendelea kuwa shujaa,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Wakili Allute Mughwai, alisema wanawashukuru Watanzania na Wakenya na bado wanaendelea kufuatilia stahiki zake.
“Huko atapokwenda apate matibabu mazuri, sisi tumefarijika kweli. Kwa niaba ya familia natoa shukrani kwa wananchi wa Tanzania na Wakenya waliotuunga mkono tangu tarehe saba hadi leo ambapo anaenda kwa mazoezi zaidi, yale mengine yaliyobaki tutafuatilia na tutafanikiwa,” alisema.