25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

LIPUMBA: MAHAKAMA ITAAMUA HATIMA YANGU CUF

Na PATRICIA KIMELEMETA

-DAR ES SALAA

MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi(CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa, hatima ya uongozi wake ndani ya chama hicho upo mahakamani.

Pamoja na hilo amesema anashangazwa na hatua ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kila siku kwenda kufungua kesi wakati suala hilo linauwezo wa kumalizwa kwa mazungumzo kwa mujibu wa Katiba ya CUF.

Kauli ya Lipumba imekuja baada ya chama hicho kuingia kwenye mgogoro wa uongozi uliosababisha kujitokeza kwa pande mbili ambapo huku kiongozi huyo akiwa anatambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na kundo lingine likipinga hatua hiyo kwa kumuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba  alisema kwa kuwa suala hilo kwa sasa lipo mahakamani anasubiri uamuzi wa kama mahakama itaamua kwa mujibu wa Katiba ya CUF ama laa.

Licha ya hali hiyo alisema kuwa Katiba ya CUF bado inamtambua yeye kama mwenyekiti halali kwani kikao kinachopaswa kumuondoa madarakani ni Mkutano Mkuu uliomchagua mwaka 2014 jambo ambalo bado mamlaka hiyo hajafanya uamuzi wowote tangu alipoandika barua hiyo Julai 2015.

“Ninashangaa sana suala hili Maalim nilimjua tangu mwaka 1973 pale Chuo Kikuu akiwa kiongozi wa wanafunzi kutoka Zanzibar na aliyekuwa akishinda msikitini kila siku eti hataki kukutana nami. Maana hata masheikh nao wanashangazwa na kila kikucha amekuwa kiguu na njia kufungua kesi mahakamani  ila kwa kuwa iko hiyo basi mahakama itaamua hatia yangu ila kwa sasa mimi ndiye Mwenyekiti wa CUF.

“Na kama mlimsikia akiwa Clouds kwenye mahojiano alisema wazi kama nikiingia pale yeye atatoka enhee amefikia hivyo tena. Na kwa kuwa ameamua hivyo mimi ndiye bosi wake na atafanyakazi chini yangu na si vinginevyo.

“Kwa mujibu wa katiba ya CUF, mimi ni mwenyekiti halali wa chama, nipo hapa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yangu na wala sipo kwa ajili ya kukivuruga chama kwa sababu nimetoka nacho mbali.

“Licha ya baadhi ya wanachama kufungua kesi,lakini nitaendelea kukiongoza chama pamoja na kutimiza majukumu mengine mpaka mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu suala hili.

“Mimi situmiki na CCM, wanaosema hivyo wana sababu zao, nipo hapa kwa sababu ya kukiongoza chama changu, kwa mujibu wa Katiba ya CUF nilishawahi kulisema hili, narudia tena, mimi ni mwenyekiti halali wa CUF na siondoki,” alisema Prof. Lipumba

Akizungumzia uteuzi wa wabunge wa viti maalumu, alisema katika uteuzi uliofanywa na Baraza Kuu la Uongozi ulizingatia orodha iliyowasilishwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi mwaka 2015 na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad.

Alisema orodha hiyo ilitokana na kikao kilichopitisha majina ya wabunge hao kilifanyika Julai 2015, Zanzibar ambacho alikiongoza yeye kabla ya kuandika barua ya kujiuzulu na wakati wa kupeleka majina NEC yalipelekwa na Maalim Seif Septemba 2015.

Alisema, kamati ya maadili ya chama hicho ilipoamua kuwafukuzwa wabunge wanane wa viti maalumu ambao wanatuhumiwa kukihujumu chama, NEC iliwaandikia barua kuhusu kuwaarifu kuwa wazi kwa nafasi hizo ambapo nao walitumia orodha hiyo kufanya uteuzi.

Uamuzi mdogo kesi ya wabunge leo

Mahakama Kuu Kanda ya Dar e Salaam  leo inatarajia kutoa uamuzi mdogo wa zuio la kuapishwa kwa wabunge wapya wa viti maalum wa CUF hadi pingamizi la Jamhuri dhidi ya maombi ya wabunge wanane na madiwani wawili wa chama hicho waliofukuzwa yatakaposikilizwa

Mahakama Kuu inatarajia kutoa uamuzi huo baada ya wabunge hao kupitia Wakili Peter Kibatala kuomba mahakama itoe amri hali iliyopo sasa ibaki kama ilivyo, wabunge wapya wasiapishwe, madiwani wasiteuliwe wala kuapishwa hadi mapingamizi ya Jamhuri yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Pia wabunge na madiwani hao wameomba mahakama itoe zuio la kuapishwa kwa wabunge hao wapya, hadi kesi yao waliyoifungua kupinga kufukuzwa uanachama itakapotolewa uamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles