Na ALLY BADI,
MKOA wa Lindi ni miongoni mwa mikoa yenye tatizo la utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha udumavu mkoani Lindi ni asilimia 44, hali inayoashiria kwamba katika kila kundi la watoto kumi wenye umri chini ya miaka mitano, watano wamedumaa.
Tatizo hili linarudisha nyuma maendeleo ya mkoa na Taifa kwa kiasi kikubwa. Hali hii inachangia pia kutokufikia kwa malengo ya dira ya maendeleo ya Taifa kwani athari zinazotokana na utapiamlo ni watoto kupungua uzito, vifo na ukuaji duni kimwili na kiakili.
Moja ya sababu kubwa ya utapiamlo ni kukosekana kwa elimu sahihi kuhusu umuhimu wa lishe kwa watoto, pia kutokutambua umuhimu wa lishe wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua. Sababu nyingine ni kuendeleza mila na desturi zilizopitwa na wakati ikiwamo ya kukamulia maziwa ya awali ya mama kwenye figa kwa madai kwamba machafu na kuwalisha watoto vyakula kabla ya kufikia umri wa miezi sita.
Kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo, mashirika yasio ya kiserikali ya Rowodo na Ropa, yamejitolea kutoa elimu ya lishe ngazi ya kaya kwa njia ya sanaa kupitia Mradi wa lishe wa Hano (Harnessing Agriculture for Nutrition Outcomes) kwa kushirikiana na Shirika la Save the Children International
Kwenye kampeni hiyo, wadau mbalimbali wa maendeleo ya mtoto walionyesha hisia na kukerwa kwa baadhi ya tabia, mila na desturi zinazoendekezwa na wazazi.
Habiba Poza, mkazi wa Kijiji cha Kiwalala anasema serikali na wadau wa maendeleo wanatakiwa kujikita zaidi katika kutoa elimu, kwani inayotolewa ni ndogo ikilinganishwa na kiwango cha imani, mila na desturi walizonazo wananchi.
Mariamu Saidi, mkazi wa Majengo Mtama anasema idadi ya wanaoamini mila na desturi potofu bado kubwa ikiongozwa na wanaume ambao wanajiona kuwa wao wana haki zaidi hivyo kuwaona wanawake kama ni watumishi wao.
Mariamu anasema kutokana na hali hiyo, wanaume wengi wamewaachia wanawake suala la malezi ya watoto na wakati mwingine wamekuwa wakiwazuia wasihudhurie kliniki wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.
Anasema pamoja na mambo mengine, umasikini nao unachangia kuendeleza mila na desturi potofu hivyo kudumaza watoto.
Naye Said Ngwinde, mkazi wa Mbekenyera, Wilaya ya Ruangwa anasema serikali na wadau wanawajibu mkubwa wa kutoa elimu kuhusiana na lishe kwa kuwa ni watu wachache mno wenye ufahamu kuhusu lishe ya mtoto na umuhimu wa chumvi iliyowekwa madini joto.
Meneja wa Shirika la Save the Children, Mkoa wa Lindi, Nengilanget Kivuyo anasema suala la lishe duni kwa watoto linachangiwa pia na kitendo cha kuwalimbikizia kazi ngumu kina mama wanaonyonyesha.
Anatoa mfano wa kazi hizo kuwa ni pamoja na kulima, kuchota maji, kukata kuni, kupika, kufua na kutwanga, hali inayowafanya wakose muda wa kupumzika na kuwa karibu na mwanawe ili kuchochea tendo la unyonyeshaji.
Anasema wanawake ambao ni watumishi hawafahamu vizuri haki ya uzazi hivyo hushindwa kudai haki zao kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua.
Anasema hali duni ya maisha nayo huwafanya kina mama wengi kuacha kunyonyesha watoto wao mapema ili kwenda kutafuta riziki.
Anataja sababu nyingine kuwa ni ushiriki mdogo wa baba na wanafamilia wengine katika kuweka mazingira mazuri ya uwepo wa lishe bora kwa mjamzito na mama anayenyonyesha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Asasi ya Rowodo, Scolastica Nguli anasema kampeni maalumu ya lishe inayotumia sanaa yenye kuchochea majadiliano juu ya hali ya lishe ni mwendelezo wa elimu inayotolewa na mradi katika ngazi ya jamii na kaya.
Nguli anasema tatizo la ukosefu wa madini joto mkoani Lindi ni kubwa mno, ambapo takwimu za mwaka 2010 zinaonesha kuwa Mkoa wa Lindi ni asilimia 6 tu ya kaya hutumia chumvi zenye madini joto.
Anasema hawatilii mkazo suala hili licha ya kwamba madini joto kuwa muhimu kwa wajawazito kwani huzuia kuharibika kwa mimba, hupunguza uwezekano wa kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo na hupunguza uwezekano wa kuzaa mtoto mfu.
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Joseph Mkirikiri anasema takwimu za mwaka 2015/16 zinavyoonyesha kuwa kitaifa watoto wenye udumavu ni asilimia 34 wakati kimkoa zinaonyesha kuwa Lindi ni asilimia 44, tumevuka hata asilimia za kitaifa, hii inaashiria kwamba tatizo la utapiamlo ni kubwa mno mkoani Lindi.
“Ndugu zangu naomba niwakumbushe kuwa tukishindwa kuwapa malezi kipindii hiki, mtoto akidumaa hali hii haiwezi kurekebishika, hivyo kwa miaka ijayo tutakuwa na watu waliodumaa kiafya na kiakili,” anasema Mkirikiti.
Anasema uwepo wa madini joto mwilini husaidia utengenezwaji wa ubongo na kuongeza uwezo wa kiakili kwa binadamu, lakini hili huanza kufanyika tangu kutungwa kwa mimba.