24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Ligi za Ulaya zinavyowapa ‘wazimu’ Wabongo

ligi-za-ulayaNa MARTIN MAZUGWA

MOJA kati ya mchezo unaoteka hisia za  watu wengi duniani ni soka uliojikusanyia mashabiki wengi ambao wamekuwa wakiufuatilia hapa nchini na nje ya nchi.

Watanzania wengi wamekuwa wakifuatilia ligi kubwa barani Ulaya kama Ligi Kuu ya England (EPL), Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) ambazo ndizo zinazoongoza kwa kutazamwa zaidi na mashabiki wa mchezo huo nchini kutokana na ubora wa klabu zinazoshiriki ligi hizo.

Wadau wengi wa soka nchini wamekuwa ‘watumwa’ wa soka la Ulaya ambalo limeonekana kupiga hatua zaidi kuliko barani Afrika, ambapo inaonekana bado kuna juhudi za kufanya ili kusonga mbele na kuvutia makampuni makubwa ya uwekezaji yaweze kuwekeza katika timu.

Kutokana na msisimko wa ligi hizo kubwa, imefikia hatua Watanzania wengi kuzifuatilia ligi hizo ambazo zimekuwa kivutio zaidi mpaka kwa watoto ambao wamekuwa wakileta ubishani kitu kinachosababisha madhara kwa ligi yetu ambayo imeanza kupoteza mvuto mbele ya macho yao.

Ugumu wa ligi hizi umeongeza mvuto wa aina yake kwa watazamaji hapa nyumbani, kutokana na timu kubwa kama Manchester United, Bayern Munich, Barcelona, Real Madrid, Inter Milan,  Juventus, Manchester City, Arsenal, Chelsea, Schalke 04, Borrusia Dortimund na Liverpool kupata matokeo ya kushangaza wanapokutana na timu zisizo na majina makubwa jambo ambalo linaongeza msisimko zaidi.

Watanzania wamekuwa wafuatiliaji wakubwa kiasi cha kuwapa majina ya utani wachezaji wanaocheza ligi hizi barani Ulaya ili kuongeza ladha ya ushabiki katika vibanda vinavyoonyesha mchezo wa soka.

Nyota ambaye amekuwa gumzo hapa  nyumbani ni kinda raia wa England anayecheza katika kikosi cha Mashetani Wekundu Manchester United, Marcus Rashford, licha ya umri wake kuwa mdogo amekuwa mwiba kwa timu pinzani kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufumania nyavu ambaye amepachikwa jina la utani la Mzanzibar na mashabiki wa soka hapa nchini.

Mshambuliaji huyo kinda  amepewa jina hilo kutokana na rangi yake ya mwili kuwa nyeusi sababu iliyopelekea mashabiki kumpachika jina hilo la utani ambalo limekuwa maarufu katika kumbi mbali mbali.

Beki wa kati wa klabu ya FC Barcelona na timu ya Taifa ya Hispania, Gerard Pique ni mchezaji mwenye jina kubwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzuia na kupandisha mashambulizi, nyota huyu muhimu katika kikosi cha Braugrana amekuwa akitaniwa kwa kuitwa jina la utani la ‘Baba Shakira’ alilopewa na mashabiki wa soka hapa nyumbani.

Nyota huyo wa Catalunya ambaye ana mtoto mmoja wa kiume  aliyepata na mwanamuziki Shakira ambaye alikutana naye mwaka 2010 katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Afrika Kusini, ambapo timu ya taifa ya  Hispania iliibuka na ubingwa kwa kuifunga timu ya taifa ya Uholanzi.

Mkali wa kufumania nyavu raia wa Argentina, Lionel Andres  Messi  ‘La pulga’ ambaye hapa nyumbani amekuwa akijulikana kwa jina la utani la  ‘Andunje’ ambalo amepewa na mashabiki wa soka wakimaanisha mtu mfupi kutokana na umbo lake, Messi  ambaye hivi sasa   amekuwa katika kiwango cha hali ya juu tofauti na msimu uliopita ambao alikumbwa na majeraha ya mara kwa mara yaliyomfanya aonekane mara chache uwanjani.

Nahodha wa kikosi cha Manchester United, Wayne Rooney ‘White Pele’  ambaye hivi sasa kiwango chake kimekuwa hakiridhishi kiasi cha kuanzia  benchi tofauti na msimu uliopita ambao alikuwa katika kiwango kizuri, ameendelea kukaa benchi huku akiwaacha vijana wakiendelea kutesa nyota huyo ambaye hapa nyumbani anafahamika kwa jina la utani la ‘Baba mwenye nyumba’ kwa kuwa ndiye kiongozi wa kikosi hicho cha kocha Mreno Jose Mourinho.

Mchezaji nyota wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo ambaye anashikilia tuzo ya mwanasoka bora barani Ulaya ambaye amekuwa katika kiwango cha juu miaka ya karibuni mara baada ya kuipatia timu yake ya taifa Kombe la Euro, baada ya  kuwafunga wenyeji timu ya taifa ya Ufaransa, mshambuliaji huyo ambaye amekuwa maarufu kwa jina la ‘Mzee wa Morocco’ kutokana na tabia yake ya kwenda Morroco mara kwa mara.

Mshambuliaji mpya wa klabu ya Manchester United kutoka PSG, Zlatan Ibrahimovic ambaye amekuwa katika uwezo wa hali ya juu, amepata umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kufumania nyavu, amekuwa akifahamika zaidi kwa jina la utani la ‘Mkara taker’ ambalo amepewa na mashabiki hapa nyumbani kutokana na uwezo wake wa kucheza mchezo wa Taekwondo ambao pia anamiliki mkanda mweusi wa mchezo huo.

Ni mchezaji ghali duniani Mfaransa Paul Labile Pogba ambaye amevunja rekodi ya usajili ya nyota wa Wales, Gareth Bale alipotoka Totenham ya London kwenda Real Madrid, nyota huyo amekuwa gumzo kutokana na tabia yake ya kubadili staili za nywele mara kwa mara kiasi cha kubatizwa jina la  ‘Ndanda  Kosovo’ kutokana kuweka rangi nywele zake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles