27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

LIGI KUU BARA LEO YANGA MZUKA KUIVAA LIPULI

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga, leo watashuka dimbani kusaka pointi tatu ugenini dhidi ya Lipuli FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja  wa Samora, Iringa.

Katika mchezo huo, Yanga itaingia uwanjani kuikabili Lipuli ikiwa na morali ya juu baada ya kufuzu hatua ya 16 ya Kombe la Shirikisho la Azam, iliposhinda penalti 4-3 dhidi ya timu ya Ligi Daraja la Pili ya Ihefu, katika mchezo wake wa mwisho kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Kabla ya mchezo huo, Yanga ilitakata baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, wiki iliyopita.

Katika msimamo wa ligi kuu, Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 28 baada ya kucheza michezo 15, ikishinda saba, sare saba na kupoteza mmoja.

Kama itaibuka mbabe leo, Yanga itafikisha pointi 31, hivyo kupunguza pengo la pointi dhidi ya mtani wake, Simba iliyoko kileleni ikiwa na pointi 35, huku pia ikiiombea mabaya Azam iliyoko nafasi ya pili na pointi zake 30, ipoteze mchezo wake dhidi ya Ndanda ambao pia utapigwa leo.

Lipuli kwa upande wake inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi 16, baada ya kushuka dimbani mara 15, ikishinda mitatu, sare saba na kupoteza tano.

Lipuli itaivaa Yanga ikiwa na hasira za kulazimishwa suhulu na Kagera Sugar katika mchezo wake wa mwisho wa kuhitimisha mzunguko wa kwanza kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Lakini kinachoufanya mchezo huu kutazamwa kwa jicho la kipekee, ni matokeo ya timu hizo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Agosti 27, mwaka jana Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, zilipotoka sare ya bao 1-1.

Katika mchezo huo, Lipuli ilianza kufunga bao la kuongoza kupitia wa mshambuliaji wake, Seif Karihe, dakika ya 44 kabla ya Yanga kusawazisha kupitia kwa Donald Ngoma, dakika ya 46.

Meneja wa Yanga, Hafidh Salehe, alisema jana kuwa kikosi chao kipo katika hali nzuri kuelekea mchezo huo.

“Wachezaji wote wako fiti kucheza,  Tambwe (Amissi) na Ibrahim Ajib, waliokosekana kwenye mchezo dhidi ya Ihefu wapo vizuri kuivaa Lipuli.

“Kazi inabaki kwa kocha, George Lwandamina, kuamua nani aanze nani asubiri,” alisema Salehe.

Vumbi la ligi hiyo pia litatimka kwenye viwanja vingine saba leo, Azam FC itakuwa nyumbani, Azam Complex kuumana na Ndanda FC, Mbeya City itakuwa mgeni wa Majimaji FC kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea.

Mbao FC itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza, wakati Njombe Mji itapimana ubavu na maafande wa magereza, Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mtibwa Sugar kutoka Manungu, Morogoro itazisaka pointi tatu dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, wakati Singida United itakuwa nyumbani kupepetana na Mwadui FC Uwanja wa Namfua, Singida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles