23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Leticia Nyerere hatunaye

Leticia-NyerereNa Florian Masinde, Dar es Salaam

ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Leticia Nyerere, amefariki dunia.

Leticia,  alifariki juzi usiku katika Hospitali ya Doctors Community iliyopo Maryland nchini Marekani alikokuwa  amelazwa tangu mwishoni mwa mwaka jana akipatiwa matibabu dhidi ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Akizungumza na MTANZANIA jana, msemaji wa familia ya Mageni Msobi, John Shibuda alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.

Shibuda, alisema hata hivyo taarifa kamili kuhusu maandalizi ya mazishi, itatolewa baada ya vikao vya familia kufanyika.

“Ni kweli amefariki dunia, sisi kama familia tutakaa na kujadiliana mipango ya kuusafirisha mwili wa marehemu kuja nyumbani kwa ajili ya mazishi,” alisema Shibuda.

Wakati mwanasiasa huyo ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) alipokuwa akipata matibabu nchini Marekani, zilizushwa taarifa za  kifo chake.

Familia yake ilikanusha taarifa hizo na kueleza kuwa Leticia alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na hali yake ilikuwa mbaya.

Leticia aliolewa na mtoto wa Hayati Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere mwaka 1996 na baadae walitengana, ingawa walifanikiwa kupata watoto watatu.

Enzi ya uhai wake, Leticia alichukua uraia wa Marekani na kuishi kwa muda mrefu nchini humo, kabla ya kurejea nchini ambapo mwaka 2010 aliteuliwa kuwa mbunge wa viti maalumu (Chadema) kwa miaka mitano.

Harakati za kisiasa

Marehemu alikuwa mbunge wa Chadema katika Bunge la 10, (2010-2015), huku akiwa Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Baada ya Bunge la 10 kumaliza muda wake Julai mwaka jana, Leticia alitangaza kujiondoa Chadema na kurudi kukitumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akitangaza uamuzi wake Julai 27, mwaka jana, Leticia alisema awali aliamua kuihama CCM baada ya kutoridhishwa na baadhi ya mambo wakati huo.

Hata hivyo, alikiri kuwa  alikurupuka katika uamuzi wake huo.

“Moyo wangu umekuwa ukisononeka kutokana na kukaa Chadema na kuacha chama kilichonilea na kunisomesha nje ya nchi, sasa nasema narudi nyumbani kukitumikia chama changu,” alisema.

Dk. Magufuli, Maria Nyerere

Katika hatua nyingine, Rais John Magufuli alimtembelea na kumpa pole mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani, jijini Dar es Salaam baada ya kupata taarifa za msiba huo.

Pamoja na kutoa mkono wa pole kwa Mama Maria, Rais Dk. Magufuli pia aliwapa pole wanafamilia wote na amewaombea kuwa wavumilivu  kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na ndugu yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alimweleza Rais Dk. Magufuli kuwa familia inakamilisha taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Marekani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles