25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

KWA HOJA HII TUNAMWUNGA MKONO WAZIRI LUGOLA

WAZIRI  wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, tangu ameteuliwa kushika wadhifa huo, ameonesha nia ya kupambana na vitu ambavyo vilikuwa haviendi vizuri.

Tumeshuhudia akitoa matamko mbalimbali kwa watendaji waliopo chini yake ili kuhakikisha anapata majibu ya msingi ya kero ambazo anaona zinapaswa kutatuliwa kwa wakati.

Moja ya hatua ambayo amewahi kuichukua ni uamuzi wake wa kumfukuza kikaoni aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dk. Juma Malewa kwa kitendo chake cha kuchelewa dakika mbili tu.

Uamuzi huo ulizua mjadala mpana kwa watu wa kada mbalilmbali, ghafla ndani ya muda mfupi Kamishna Jenerali akastaafu kwa mujibu wa sheria, huku watu wakisema uamuzi wa Lugola ulimweka matatani kiongozi huyo.

Miongoni mwa habari tulizochapisha katika gazeti hili toleo la jana ilikuwapo ya Lugola iliyokuwa na kichwa cha habari. “Kangi ataka mabasi yasafiri usiku”.

Katika taarifa hiyo, waziri huyo alimpa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro siku 14 na wasaidizi wake waende ofisini kwake wakiwa na majibu sahihi kwa nini mabasi hayasafiri usiku.

Alitoa agizo hilo alipofanya ziara makao makuu ya kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kilichopo Ukonga, Dar es Salaam.

Waziri huyo alimtaka IGP amweleze mikakati ya kuwawezesha Watanzania kufanyakazi saa 24 na mabasi kusafiri usiku.

Alisema mabasi kutotembea usiku ni kwa sababu Jeshi la Polisi limenyoosha mikono kwa majambazi na kwamba hata wananchi kufunga biashara zao mapema ikifika saa 12 jioni ni kwa sababu ya kuhofia usalama.

Alisema kama taifa hatuwezi kufikia malengo ya uchumi wa kati ikiwa Watanzania hawafanyi shughuli za uchumi.

Lugola alikenda mbali zaidi akasema, hatuwezi kupewa amri na majambazi kwamba ni masaa mangapi tufanye shughuli za kiuchumi au ni maeneo gani tuende na maeneo gani tusiende.

Hili ni agizo zito kutolewa kwa IGP Sirro, kwani aliwahi kuambiwa ahakikishe anadhibiti ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikikatisha uhai wa  Watanzania.

Katika kipengele hiki kumekuwapo na mafanikio makubwa tofauti na miaka mingine, kwani ajali zimepungua kwa kiasi kikubwa na hii ni kutokana na ukweli kwamba mikakati ya kuja na tochi umesaidia.

Katika hili tunamwunga mkono Waziri Lugola kwamba kitendo cha polisi kuzuia mabasi kutembea usiku ni dalili kwamba wamesarenda kwa majambazi.

Hakuna Serikali yoyote hapa duniani inayoweza kusalimu amri dhidi ya wahalifu. Jambo hili limekuwa kero ya muda mrefu kwa Watanzania kwani kuzuia mabasi kusafiri usiku ni kurudisha nyuma harakati za kiuchumi si tu kwa Serikali bali hata kwa mwananchi mmoja mmoja kiuchumi na kijamii.

Haiwezekani basi linalotoka Mwanza lilale mkoani Morogoro, wakati kipande kilichobaki kufika Dar es Salaam ni kidogo mno. Hivi ni kweli kuna ujambazi gani wa kutisha uliopo kati ya Morogoro na Dar es Salaam?

Tunaamini kama mabasi hayo yakiendelea na safari huku polisi wakiwa wamejipanga vizuri katika utendaji wao, ajali wanazohisi zinatokea hazitatokea kama wanavyofikiri.

Tunajiuliza kwanini nchi za jirani kama Kenya, Uganda na Rwanda mabasi yanasafiri usiku mzima isipokuwa Tanzania? Hii maana yake ni kwamba wenzetu wamedhibiti uhalifu kiasi kwamba wananchi hawana hofu katika shughuli za uzalishaji pamoja na suala zima la usafiri.

Sisi MTANZANIA, tunasema uamuzi huu umekuja wakati mzuri na tungependa kuona mabasi yanaanza kusafiri usiku.

Tunatoa rai kwa Jeshi la Polisi kubadilisha fikra zake za utendaji kazi wa mazoea na kuingia kwenye uhalisia wa vitendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles