32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kizaazaa chaibuka watoto 18 waliofungiwa Moshi

NA RODRICK MUSHI, MOSHI
ZAIDI ya raia 500 wameizingira nyumba moja iliyokuwa imewafungia ndani watoto 18 wenye umri kati ya miaka mitatu na 17 mjini Moshi.
Watoto hao inadaiwa walifungiwa kwenye nyumba hiyo yenye vyumba vinne na choo kimoja ambapo inadaiwa walikuwa wakifundishwa masomo ya dini.
Inaelezwa kuwa watoto hao walifungiwa kwenye nyumba hiyo kwa muda wa miaka mitatu, huku wakifundishwa masomo ya dini hali iliyozua hofu kwa wakazi wa Manispaa ya Moshi.
Taarifa za kuwapo kwa watoto hao zilibainika juzi jioni mjini hapa hali iliyovuta hisia za wakazi hao, huku wengi wao wakitaka kujua lengo la watoto hao kuwa eneo hilo na hali zao kiafya.
Hali hiyo ililazimu Jeshi la Polisi kuingilia kati na kuimarisha ulinzi ambapo waliwatoa watoto hao, huku wakitawanya wananchi hao waliokuwa wameizingira nyumba hiyo.
Chanzo cha kuaminika kutoka mjini hapa kiliiambia MTANZANIA kuwa watoto hao waliokusanywa katika nyumba hiyo wanatoka katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Mwanza.
Akizungumza na wananchi waliokuwapo eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga, alisema walipata taarifa ya kuwapo kwa watoto hao kutoka kwa msamaria mwema.
Alisema taarifa hiyo waliipata juma lililopita na kuanza kufanya uchunguzi wao na juzi ndipo walipokamilisha na kufika kwenye eneo hilo.
Polisi walizingira nyumba hiyo kuanzia saa 12:00 jioni hadi jana baada ya kutolewa kwa watoto hao.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema kitendo cha kuwakusanya watoto sehemu moja bila kibali ni kinyume cha sheria.
Alisema mmiliki wa nyumba hiyo alipaswa kuomba kibali kwa mamlaka husika kwa mujibu wa sheria na si kufanya suala hilo kienyeji.
“Mafunzo anayoyatoa kwa watoto hawa, hata kama ni ya dini, ni lazima yafuate taratibu za nchi. Sheria zipo, unapokusanya watoto mahala pamoja kunatakiwa kuwaje kuanzia mazingira hadi eneo lenyewe na kama una taasisi unaendesha mafunzo, je kituo kimesajiliwa? Na ndiyo maana tumeagiza watoto warudishwe kwa wazazi wao,” alisema Makunga.
Nyumba hiyo yenye idadi ya vyumba vinne na choo kimoja, imewafanya viongozi mbalimbali walipofika eneo hilo kupata wasiwasi kutokana na idadi kubwa ya watu wanaoishi humo.
Kwa upande wake, mmiliki wa nyumba hiyo, Abdulnasir Abdulrahman, alisema wamewakusanya watoto hao ili kuwafundisha masomo ya dini ya Kiislamu na kuwakuza katika imani hiyo wakiwa wadogo.
Alisema watoto hao wameletwa hapo kwa ajili ya kupata elimu ya dini, na wazazi wao wanajua na wanachangia vitu mbalimbali ikiwamo vyakula ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu
ya dini ya Kiislamu.
“Watoto wote tunaoshi nao hapa wana wazazi wao, ambao wamekubaliana na sisi waendelee kupata elimu hiyo hapa chini ya uangalizi wetu na wazazi wao wamekubaliana kuwalea,” alisema Abdulrahman.
Jeshi la Polisi linawashikilia baadhi ya wazazi na mmiliki wa nyumba hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles