23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Marando: Dk. Slaa anusurika kuuawa

Dk.slaaNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amenusurika kuuawa na mlinzi wake.
Hilo limebainika baada ya kitengo cha ulinzi cha chama hicho kutibua mpango unaodaiwa kuratibiwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (TIS), wa kumuua kiongozi huyo kwa kumtumia mlinzi wake binafsi (PSU), Khalidi Kagenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Mabere Marando, alisema Kagenzi akiwa mlinzi binafsi wa Dk. Slaa katika kipindi cha miaka miwili, amebainika kutumiwa na vyombo vya usalama vya nchi pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuvujisha siri za chama hicho, na kupewa kazi ya kumuua katibu huyo wa Chadema.
Akielezea tukio lililombaini mlinzi huyo, Marando alisema lilitokea Ijumaa iliyopita baada ya mashushushu wa chama hicho kumwona mlinzi huyo akipanda gari lenye namba za usajili T 213 ARS linalodaiwa kutumiwa na Ofisa Usalama wa Taifa wa Kinondoni.
“Baada ya kuonekana ndipo mashushu wa Chadema walichukua jukumu la kumkamata na kumfanyia mahojiano ambapo walifanikiwa kumpekua katika simu zake mbili zinazotumia mitandao ya Vodacom, Airtel na Tigo.
“Katika simu hizo, walikuta ujumbe mfupi wa maneno uliokuwa ukitoka kwa …, aliyempigia mara tatu na kumtumia fedha kati ya Desemba 4, mwaka jana na Julai 14, 2014. Namba nyingine zilizokutwa zilikuwa za maofisa Usalama wa Taifa,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya upekuzi huo katika ‘Note book’ na simu zake, waligundua kuwa kigogo mmoja wa ngazi za juu wa CCM alimtumia muda wa maongezi wa Sh 50,000 kwa namba ya simu 0764 …222 Julai 14, 2014 na Desemba 4, 2014 alimtumia Sh 150,000.
Marando alisema katika upekuzi wa kwenye simu, walibaini mazungumzo yake yote yalikuwa yakitumia muda usiopungua saa mbili hadi tatu, na mara zote ni wakati ambao Chadema walikuwa wakifanya mikutano yao ya ndani.
“Alikuwa akitumia simu yake kurekodi kila kilichokuwa kikizungumzwa kwenye mikutano yetu na kusambaza kwa CCM, na iligundulika akiwasiliana na maofisa wa Usalama wa Taifa waliofikia 22,” alisema.
Marando aliongeza kwa kusema kuwa kama isingekuwa suala la kutolewa kwa uhai wa Dk. Slaa, wasingezungumzia suala hilo na pia anazungumziwa huenda akachaguliwa kuwa mgombea wa urais wa Ukawa.
Alisema kuwa jana chama hicho kimetoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kuchukua hatua za kisheria ambao ndio wanaweza kutaja majina ya maofisa usalama wa waliohusika na mpango huo.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu afya ya Dk. Slaa, alisema hadi jana alikuwa salama ingawa bado hajapima kubaini hilo.
Marando alisema baada ya kugundulika kufanya hujuma hizo, Ijumaa iliyopita walimsimamisha majukumu yake ya kumlinda kiongozi huyo hadi pale uchunguzi dhidi yake utakapokamilika.
Ingawa chama hicho hakikueleza kiasi cha fedha ambacho mtuhumiwa alipewa kufanyia shughuli hiyo, lakini kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa kwa Idara ya Ulinzi wa chama hicho, alionyesha ndani ya simu yake kiasi cha Sh milioni 7 ambazo zilikuwa muda wa maongezi kwa muda wa miaka miwili.
MTANZANIA ilimpomtafuta kigogo wa CCM aliyetajwa, hakupatikana ofisini kwake Lumumba wala Dodoma, na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa.
Pamoja na jitihada hizo, pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ‘SMS’ hakuweza kujibu hadi tunakwenda mitamboni.
Taarifa kutoka ndani ya Chadema zinaeleza kuwa tangu Ijumaa baada ya kugundulika kwa mpango huo walinzi wa chama hicho walikuwa wakimsulubu kwa kipigo Kagenzi ili kuweza kupata ukweli.
Huku akiwa anapigwa, Kagenzi alilazimika kutaja majina ya watu wote waliokuwa wakifanya kazi hiyo ikiwamo kuandika taarifa maalumu ikiwamo shughuli binafsi za Dk. Slaa.

POLISI WAZUNGUMZA
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camillus Wambura, alithibitisha kufikishwa mtuhumiwa huyo katika Kituo cha Polisi Oysterbay ambapo alisema wanaendelea na mahojiano naye ili kujua ukweli wa tuhuma zinazomkabili.
“Tumempokea leo (jana) mtuhumiwa, tumeanza kuwahoji waliomleta na baadaye kumhoji muhusika ili tuweze kubaini ukweli kuhusu tuhuma dhidi yake,” alisema Kamanda Wambura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles