25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Utafiti: Paracetamol hufupisha maisha ya binadamu

paracetamol_0MWANDISHI WETU NA MASHIRIKA YA HABARI
MATUMIZI ya kila siku ya dawa za kupunguza maumivu za paracetamol huongeza hatari ya ugonjwa wa moyo, kiharusi na kufupisha maisha ya binadamu, utafiti mpya umeonya.
Paracetamol hupendelewa zaidi na madaktari wengi hudai zi salama kulinganisha na aspirin, ambayo imehusishwa na kuvuja damu tumboni na ibuprofen iliyohusishwa na magonjwa ya moyo na kiharusi.
Lakini watafiti wa Uingereza waliofanya uchunguzi huo uliowahusisha wagonjwa 666,000 wanasema hatari iliyomo katika dawa hizo huenda ilipuuzwa na sasa wameagiza uchunguzi ufanywe kuhusu usalama wake.
Taarifa hizo iwapo ni za uhakika, itakuwa pigo kwa wengi kwa vile paracetamol zimezoeleka kuliko dawa nyingine yoyote ile ya kupunguza maumivu, na inapatikana kirahisi na kila mahali.
Nchini Uingereza kwa mfano, ushauri zaidi ya milioni 22.5 kutoka kwa daktari wa kutumia dawa hutolewa kila mwaka.
Zaidi ya hayo, makasha milioni 200 ya paracetamol huuzwa kila mwaka.
Hata hivyo, Profesa Philip Conaghan wa Taasisi ya Dawa ya Rheumatic and Musculoskeletal mjini Leeds, Uingereza, amefichua kuwa matumizi ya muda mrefu ya paracetamol yana athari mbaya kiafya.
Professa Conaghan alipitia tafiti nane zilizofanyika huko nyuma kutathimini uhusiano baina ya matumizi ya muda mrefu ya paracetamol na matatizo ya kiafya kwa watu wazima.
Utafiti huo umebaini wagonjwa wanaopewa dawa hizo za kupunguza maumivu mwilini kwa muda mrefu wana hatari kubwa ya asilimia 63 kufupisha maisha yao.
Hatari ya kupatikana ugonjwa wa moyo na kiharusi iko juu kwa asilimia 68, huku pia kukiwa na hatari kubwa ya asilimia 50 ya kupatikana vidonda vya tumbo au hata kuvuja damu.
“Kwa kuegemea takwimu hizo hapo juu, tunaamini hatari halisi ya matumizi ya paracetamol kuwa ya juu kuliko inayodhaniwa na jamii ya wataalamu wa afya,” alisema.
Watafiti hao walihitimisha kuwa kutokana na ukubwa wa matumizi ya paracetamol na urahisi wa upatikanaji, uchunguzaji wa athari zinazoweza kupatikana kutokana na dawa hizo ulipuuzwa.
Professa Nick Bateman wa Chuo Kikuu cha Edinburgh, alisema wanadhani utafiti huo umetoa mwanga kuhusu matumizi ya muda mrefu ya paracetamol.
Anasema hata hivyo matumizi ya paracetamol hayapaswi kuachwa moja kwa moja.
Professa Bateman pia anashauri kuwa watu wanapaswa kutumia kiwango cha chini cha dozi ya paracetamol kwa kipindi kifupi ambacho kinaweza kuzuia matatizo ya kiafya.
Naye Professa Conaghan anakiri takwimu hizo zinaweza kuwatisha watu wanaotumia paracetamol kwa kipindi kirefu.
Hata hivyo, anasema watu wanapaswa kushauriana na madaktari wao au wataalamu wa afya kabla ya kutumia paracetamol kwa kipindi kirefu.
Watafiti wanasema utafiti huo ni muhimu kwa vile utawasaidia madaktari kuwashauri wagonjwa kuhusu hatari zilizopo iwapo watatumia dawa hizo kwa kipindi kirefu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles