30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kivule kupata shule kidato cha tano

Na Jestina Zauya (TUDARCo), Mtanzania Digital

Shule za Sekondari za Abuu Jumaa na Misitu zilizopo Kata ya Kivule kuanzia mwakani zitaanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano ili kukabili upungufu wa uhaba wa shule ambao umesababisha watoto kuchaguliwa shule za mbali.

Akizungumza wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kuanzia Desemba 2020 hadi Agosti mwaka huu, Diwani wa Kata ya Kivule, Nyansika Getama, amesema baadhi ya watoto ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne wamekuwa wakipelekwa shule za mbali kutokana na kata hiyo kutokuwa na shule.

“Kuanzia mwakani tutakuwa na kidato cha tano na sita na hilo limeshapitishwa sasa hivi liko kwenye ngazi ya wataalam kutembelea, mimi ndiyo sauti yenu kwenye Halmashauri ya Jiji hivyo, nitahakikisha nazifanyia kazi changamoto zote ili kuleta ufanisi kwenye kata”, amesema Getama.

Aidha amesema zaidi ya Sh milioni 344 zimetumika katika kipindi hicho kwenye sekta ya elimu kwa kukarabati na kujenga vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, ofisi za walimu na ununuzi wa madawati katika shule za msingi na sekondari.

Kwa mujibu wa diwani huyo katika Shule ya Msingi Bombambili vimejengwa vyumba viwili vya madarasa na matundu 12 ya vyoo, Shule ya Msingi Kivule Annex (vyumba viwili vya madarasa), Shule ya Msingi Serengeti (vyumba viwili na ununuzi wa madawati 67), Shule ya Sekondari Abuu Jumaa (vyumba vinne, meza 58 na viti 58) na Shule ya Sekondari Misitu (vyumba sita na viwili vya walimu).

“Nilifanya ziara kwenye maeneo yote ya huduma za jamii shule nilizozikuta zilikuwa na uhaba wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo nikapambana tukapata fedha,” amesema.

Aidha katika sekta ya afya amesema baadhi ya majengo yanaendelea kujengwa katika hospitali ya wilaya ikiwemo jengo la meno, wodi ya wanaume, wodi ya wanawake na wodi ya watoto.

Diwani wa Kata ya Kivule, Nyansika Getama

Hata hivyo amesema bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa shule Mtaa wa Magole A na kituo cha polisi chenye hadhi ya kata.
Diwani huyo pia amewataka wananchi kutoa ushirikiano wakati zoezi la kuhesabu watu litakapoanza ili Serikai ijue idadi kamili ya wakazi wa kata hiyo kurahisisha upangaji wa shughuli za maendeleo.
Takwimu za Sensa ya mwaka 2012 zinaonyesha Kata ya Kivule ina wakazi 36,031 na kati yao wanaume ni 13,016 na wanawake ni 21,015 huku pia kukiwa na kaya 8,149.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kivule, Anna Masawe, amesema kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kaya 182 zimenufaika na kwamba hakuna mtaa ambao hauna walengwa.

“Mlengwa wa Tasaf haangaliwi kwa sura au umbo lake bali ni hali yake kiuchumi, je ana uwezo wa kula angalau milo miwili, nyumba yake ikoje, maji ya kunywa anachota wapi, ana uwezo wa kumnunulia mtoto sare…ukisema unalala chini lazima tuingie ndani tujiridhishe,” amesema Masawe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kivule, Hemed Nyunguru, amewataka viongozi wa matawi kuhakikisha ofisi zinakuwa wazi wakati wote na wenyeviti wa serikali za mitaa wazitembelee mara kwa mara ili kuona ufanisi wa utendaji kazi.

“Ofisi za matawi zinafungwa lakini kwa bahati mbaya majani mpaka mlangoni, hatuwezi kufanya kazi namna hii naagiza ofisi ziwe wazi muda wote na wenyeviti wa serikali za mitaa tembeleeni muone udhaifu wao,”amesema Nyunguru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles