23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Sekondari Liwiti kuanza kuchukua wanafunzi Januari

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Jumla ya Sh milioni 420 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Liwiti ambayo inatarajiwa kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani.

Diwani wa Kata ya Liwiti, Alice Mwangomo, akizungumza wakati wa mkutano na wananchi kuhusu ujenzi wa shule ya sekondari ya kata hiyo.

Kujengwa kwa shule hiyo kutalifanya Jimbo la Segerea kuwa na shule 18 za sekondari hatua ambayo itawapunguzia adha ya umbali mrefu waliyokuwa wakiipata watoto wanaotoka Liwiti kwenda kusoma shule zilizo nje ya kata hiyo.

Akizungumza wakati wa mkutano na wananchi Diwani wa Kata ya Liwiti, Alice Mwangomo, amesema shule hiyo itajengwa kwa mtindo wa ghorofa na kwamba kati ya fedha zilizotengwa Sh milioni 300 zinatoka Serikali Kuu na Sh milioni 120 zinatoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

“Wakati naomba ridhaa ya kuniweka madarakani niliahidi mambo mengi ikiwemo shule ya sekondari kwa sababu watoto wetu wamekuwa wakipelekwa mbali hadi Chanika, nina furaha kuwaambia jambo letu limekamilika shule inajengwa,” amesema Mwangomo.

Aidha ameiagiza kamati ya ujenzi wa shule hiyo kuhakikisha vibarua wanatoka kwenye kata hiyo huku pia akiwataka wajasiriamali wengine kama mama lishe kuchangamkia fursa ya kuuza chakula.

Naye Ofisa Elimu wa Jiji la Dar es Salaam, Mwalimu Mussa Ally, amesema tayari amemteua mkuu wa shule na kuwahakikishia wananchi wa Liwiti kuwa watapambana ujenzi huo ukamilike haraka ili Januari mwakani ianze kuchukua wanafunzi.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Liwiti, Ignas Maembe, akizungumza kwenye mkutano huo.

Kwa upande wake Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, ambaye aliwakilishwa na Katibu wake Lutta Rucharaba, amesema atahakikisha mipango yote iliyopangwa kwa ajili ya ujenzi huo inakamilika mapema ili watoto waanze kusoma Januari mwakani.

Amesema Jimbo la Segerea kwa sasa lina shule 17 za sekondari na kati ya hizo sita zimejengwa kati ya mwaka 2016 na 2021 chini ya uongozi wa mbunge huyo.

Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Steven Mushi, amesema sambamba na ujenzi wa shule hiyo pia wamepanga kukarabati vyumba vya madarasa katika shule mbili za msingi zilizopo kwenye kata hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles