Na Mwandishi Wetu,
MWANDISHI, mshairi, mwanafasihi, mwanasiasa na mchambuzi mwenye asili ya Uganda na Sudan, Taban Lo Liyong (1936-) alisababisha taharuki katika ulingo wa usomaji miongo zaidi ya minne iliyopita (mwaka 1969) alipokosoa kwa ukali eneo la Afrika Mashariki aliposema ni ‘jangwa la usomaji’.
Wasomi wa ukanda huo kwa wakati huo walijibu maoni ya msomi huyo gwiji kwa ukali kama vile kummiminia risasi za moto mwilini wakisema kuwa kauli yake ilikuwa ni tusi kwa wasomi wa ukanda huo hususani baada ya kuondokana na ukoloni (walitoa maoni kwamba ilikuwa ni mapema mno kutoa hitimisho hilo lililoonesha kuegemea upande mmoja ikiwa ni takribani miaka kumi tu baada ya nchi za Afrika Mahariki kujipatia uhuru wake).
Kinyume chake leo ikiwa ni miaka 48 tangu Taban atoe maoni hayo, na ikiwa ni miaka 55 tangu Afrika Mashariki ipate uhuru, mwandishi amethibitisha kile kinachoufanya ukanda huo kujulikana kama ukanda wenye ‘utamaduni duni wa kusoma’. Kwa kuzungumzia uhalisia, haiwezekani uwepo ‘ustawi ki-uhalisia’ bila kuwapo usomaji wa kuridhisha au kutosha.
Kutokana na hali hiyo, inavutia kuona kuwa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo Tanzania ikishirikiana na Kampuni ya Jackson Group kulishughulikia suala hilo. Ukiwa ni ushirikiano kutoka sekta binafsi na si serikalini, taarifa hiyo inaweza kufungua fursa ya kuibua mjadala kutoka kada ya wasomi kuhusu ‘ugonjwa wa taaluma’ hususani katika ulingo wa kusoma na au kukosekana kwake.
Taarifa iliyotolewa na Tigo wiki iliyopita inataarifu wasomaji kwamba kampuni hiyo inashirikiana na Jackson Group kuzindua jukwaa jipya la mtandao linaloitwa Kitabu App ikiwa ni Kitabu elektroniki kilichoundwa kwa ajili ya kutoa aina mbalimbali za viatu kwa njia ya sauti na kuona kwa wasomaji tofauti nchini Tanzania.
Jukwaa hilo kama likitumika ipasavyo linaweza kukiteka kizazi cha sasa ambacho ni cha kidijitali na kuibua matumaini ya hamasa kubwa katika kusoma.
Meneja wa Mawasiliano ya Tigo, Woinde Shiasel anasema Kitabu App inaingia katika soko ikiwa ni suluhisho si tu kwa wasomaji bali pia kwa waandishi ambao hivi sasa wanaweza kuuza na kupigia debe mauzo ya vitabu vyao kupitia simu zao za mkononi.
Anasema hiyo itafanikiwa kwa kutumia mtandao wa Tigo 4G LTE.
Ni sahihi kusema mauzo kwa njia ya mtandao yanaweza kuwa ni mabadiliko katika waandishi kwa kuwa yanaweza kuwafungulia masoko ya nje.
Shisael anabainisha kuwa kupitia app hiyo, inatarajiwa kuwapo mabadiliko katika namna ambavyo Watanzania wanavyouchukulia dhana ya usomaji, dhidi ya kuporomoka kwake ambako kunahusiana na wananchi katika utamaduni duni wa kujisomea hivyo, kuhamasisha matamanio katika kusoma miongoni mwa jamii na hivyo kuhuisha zoezi hilo lililoporomoka ndani ya nchi.
Anasema; “Hii ni aina ya sauti ambayo inatakiwa kutoka kwa wahusika wa kitaaluma na mamlaka zinazohusika ikiwa ni kichocheo cha kuibua uchunguzi wa kitaaluma jambo ambalo ndilo lililokuwa ishara katika miaka ya mwanzo ya 1970 na mwishoni mwa miaka ya 1980 wakati taasisi za kujifunza zilipoibuka kikiwa ni kipindi kisichoweza kulinganishwa katika kupanuka kitaaluma.
“Kwa bahati mbaya minara yetu ya taaluma ya kisasa ya vyuo vikuu na mengineyo imekuwa ikijikita katika dhana mbaya ambayo ina imani potofu kwamba lengo la kusoma ni kufaulu katika mitihani tu dhana iliyohodhiwa na mitazamo mifupi ambayo haitazami hatima ya mwanafunzi atakapoingia katika maisha ya kiuhalisia ama katika ajira.”
Ukweli unabakia kuwa kulingana na vijana wa Kitanzania, kujisomea si tena kitendo cha thamani kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
Kutokana na mabadiliko ya teknolojia ambako mada nyingi za masomo zinafikiwa kupitia mtandao wa intaneti, ni jambo lisiloepukika kwamba kuna kasi ya mabadiliko kwa kujumuisha njia za mabadiliko ya kawaida za kupata uelewa kupitia kujifunza kwa kutumia njia ya mtandao.
Jambo linalofikirisha wengi ukiondoa mtazamo wa zamani kwa wale ambao kitaaluma waliyapitia mambo kabla ya enzi za kidijitali, ambapo uhalisia ulipozamishwa linaweza kuonekana kama ni kifo cha vitabu ambavyo tulikuwa tunavitumia.
Hata hivyo, Kitabu App inatoa taswira ya uhamasishaji-waandishi wengi wamekuwa wakiandika kwa lugha ya Kiswahili, ambayo inaeleweka kwa Watanzania walio wengi. Ni uboreshaji wa kweli kutoka Tigo, ambao unafahamika kwa mchango wake katika kuzibadilisha mada za ndani kama Kiswahili kuwapo katika Facebook.
“Tayari wateja wetu wengi wanapenda kutumia simu kuchati na marafiki na wanafamila. Kupitia Kitabu App, tunatoa jukwaa la uhakika kwa waandishi, waelekezaji na wasomaji wa jumla sehemu ambayo wanaweza kupata kwa urahisi mada za kusoma kupitia simu ya mkononi,” anasema Shisael.