24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

KITABU: TUTAFUTE MAZIMWI YA UFUKARA WA AFRIKA

 

 

Na Markus Mpangala,

MARRICKE Kofi Gane ni mzaliwa wa Ghana amekuwa gumzo kila mahali kutokana na maandiko yake mbalimbali kuhusu maisha ya Afrika.

Leo tunachambua kitabu chake cha “IS THIS WHY AFRICA IS? Kitabu hicho kimechapishwa na Marrickekofigane Publishing na kinasambazwa na kampuni kubwa ya uuzaji wa vitabu ya Marekani, Amazon. Kimepewa namba ISBN 978-1-9093326-20 na kina jumla ya kurasa 104 na kuandikwa kwa lugha ya kiingereza.

MAUDHUI

Maudhui ya kitabu hiki ni kujaribu kuonesha picha kwanini Bara la Afrika limebaki nyuma. Kwanini linachechemea katika suala la maendeleo. Amekigawa kitabu katika sura mbalimbali.

Sura ya kwanza ameipa jina la ‘In the Beginning was Pride, the Hope, then’. Sura hii anatuelezea namna maisha ya mwanzo yalivyokuwa sifa, matumaini na matarajio mengi zaidi. Anatuelezea maisha yake  tangu alipozaliwa katika mji wa Volta nchini Ghana. Anatuelezea namna alivyoweza kuifahamu miji ya Jos na Kaduna ya nchini Nigeria.

Kisha anatukumbusha maisha ya Benue. Huu ndio mwanzo wa matumaini yake. Mwanzo wa kuelekea nchi ya ahadi. Mwanzo wa kufanikisha katika maisha ya Kiafrika na wananchi wake.

Sura ya pili ameipa jina la ‘Can Someone please tell me why?  Katika eneo hilo anajiuliza ni namna gani Afrika imekuwa masikini kiasi kwamba haiwezi kuwekwa kwenye mizani ya dunia ya kwanza.

Anajenga mtiririko wa hoja kwamba ni lazima tujiulize maswali ya msingi, kwamba labda hatukuweza kuachana na utumwa na tungependa kuendelea nao.

Mwandishi anajenga taswira ya hangaiko kwa kuangalia mwenendo mzima wa maisha ya waafrika. Anatukumbusha hotuba ya Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah aliyotoa mwaka 1957. Namna ilivyokuwa na matumiani ya kuliunganisha Bara la Afrika na kuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi. Namna ya kuiwezesha Ghana na mataifa mengine kuibuka wababe kwenye uchumi.

Anaandika; “To those angry enough to dare see it change for good, even if beyond their time; To those unafraid enough to venture to ask the hard questions about Africa…”

Tafsiri ya kiswahili isiyo rasmi, “Wenye ghadhabu na uthubutu wa kuleta mabadiliko mema, hata ikiwa zaidi ya muda wao wa kawaida. Kwa wote wasiohofia chochote wajaribu kuhoji maswali magumu kuhusu Afrika.”

Anasema endapo Waafrika walinyanyaswa ni kwa vipi wameshindwa kurekebisha jambo hili. Ni kwa vipi hawajaweza kabisa kuachana na utumwa unaozidi kuwang’ang’ania nyakati zote za maisha yao.

Anasema; “Nilisimuliwa sifa nyingi za Afrika na babu yangu. Niliambiwa mengi kuhusu Waafrika na nikajawa matumiani, lakini sasa najiuliza ni nani anaweza kunieleza mazimwi hayo yanayowatafuna Waafrika?

Sura nyingine za kitabu hicho ni kama ifuatavyo; (ii)‘Could it have been the Curse? (iv)‘Could it have been our Independence? (v)Could it been our Miseducation?

Aidha, sura zingine; (vi)Could it have been Genetic or Cultural? (vii) Could it have been religious immension? (viii) Could it have been the Superpowers? (ix) Could it have been a different Africa? (x) In Conclusion changing guards.

Licha ya kumfanya msomaji atafakari na kuangalia kupata suluhisho, pia anaweka njia ya wazi ya kuweza kubaini nini kinachoweza kufanywa katika maendeleo.

Anahoji elimu yetu, utamaduni, jamii na uongozi kwa ujumla. Anawajadili washirika wa maendeleo, lakini mwandishi amekwenda sambamba na watoa maoni wengi wanaodhani washirika wa maendeleo kwa mtindo wa kutoa mikopo pekee ni jibu.

Sura ya mwisho ya ‘In Conclusion changing Guards, anawazungumzia viongozi na siasa. Hii ikiwa na maana ya mabadiliko ya viongozi wanaotutawala katika mataifa yetu ili kubadilisha mambo yote.

Mapendekezo ya mwandishi yanaturudisha kwenye misingi ya kutatua matatizo ya Afrika kwa njia za Afrika. Tunaweza kutegemea washirika wa maendeleo na wadau kutoka kada mbalimbali, lakini haliwezi kuwa jibu la moja kwa moja.

Bali njia ya uhakika na yenye kuweza kurekebisha hayo yote ni kuhakikisha watawala wanabadilisha mitazamo. Mwandishi anatoa mifano namna viongozi wanamshangaza kwa kushindwa kuthamini na kutoa faida ya matumaini kwa wananchi wao.

Mwandishi ametuachia maswali pekee ili tutafute majibu kulingana na jamii zetu. Je, ni wapi yametoka mazimwi ya dhiki barani Afrika? Tutafute majibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles