24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

KINACHOENDELEA LIGI YA TAIFA YA WANAWAKE

ZAINAB IDDY NA MARTIN MAZUGWA


2MIAKA mingi timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ imekuwa ikiundwa kwa wachezaji kuokotezwa kutoka sehemu mbalimbali, lakini hivi karibuni tiba ya tatizo hilo imeweza kupatikana

Tiba hiyo imepatikana baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais  Jamal Malinzi, kufanikiwa kuanzisha Ligi ya Wanawake, ambayo  imeanzishwa ikiwa na mdhamini mmoja tu ambaye ni kituo cha Azam Tv, kinachoonyesha michezo yote kupitia king’amuzi chake.

Ligi hiyo inashirikisha jumla ya timu 11ambazo ni Evergreen Queens, JKT Queens na Mburahati Queens za Dar es Salaam, Panama ya Iringa, Kigoma Sisters ya Kigoma, Fair Play ya Tanga, Viva Queens ya Mtwara, Baobab ya Dodoma, Marsh Academy ya Mwanza, Majengo ya Singida na Victoria ya Kagera.

Wadau wengi wa soka wanaamini kuwa kuanzishwa kwa ligi hiyo ambayo ni ya kwanza Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kunaweza kuleta mafanikio makubwa katika soka la wanawake, kwa kuwa litaweza kuongeza idadi ya wanawake wanaocheza mpira wa miguu na kupelekea kuundwa timu bora ya taifa itakayokuwa na wachezaji wenye viwango.

Lakini pia benchi la ufundi la timu ya taifa litaweza kugundua vipaji vipya vitakavyojumuishwa kwenye timu ya hiyo, ambayo mwakani itaingia kwenye programu ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake kutoka kanda ya Afrika, ambapo michuano hiyo imepangwa kufanyika mwaka 2019 huko Ufaransa.

Wakati ligi ikiendelea na wadau kuwa na matumaini hayo, nyuma ya panzia yapo mengi yanaendelea, ambapo kwa kiasi kikubwa yanakatisha tamaa kwa washiriki kiasi cha miongoni mwao kuamini wanatwanga maji kwenye kinu.

SPOTIKIKI imeamua kuingia ndani zaidi na kugundua mambo kadha wa kadha, ambayo kimsingi yanapoteza dhamana ya ligi husika.

Wamuzi kuzibeba timu za mikoa yao

SPOTIKIKI imebaini kuwa moja ya vitu vinavyopigiwa makelele katika soka hilo ni waamuzi, kwani kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo, inaonyesha asilimia kubwa ya waamuzi wanaochezesha ligi hiyo hufanya kazi katika mikoa walipo.

Mfano mwamuzi anayetoka jijini Dar es Salaam ni nadra sana kumkuta akichezesha mechi kwenye Mkoa wa Tanga, jambo ambalo linalalamikiwa na timu zinazoshiriki kwa madai kuwa inachangia kupangwa kwa matokeo.

“Ukiangalia waamuzi wengi wamepangwa katika vituo vya mikoa wanayoishi, hii inatoa urahisi kwao kuzipendelea timu za mikoa yao na hivyo kutokea kwa suala la upangaji wa matokeo,” anasema mmoja wa viongozi wa timu inayoshiriki ligi hiyo ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake.

Zawadi ni kitendawali

Wakati ligi hiyo ikiendelea, hadi hivi sasa washiriki hawajajua kama zawadi ya fedha itapatikana  kama ilivyokuwa kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Awali TFF ilibainisha  hakutakuwa na zawadi ya fedha zaidi ya kombe na medali kwa timu shiriki, hakuna tuzo ya mchezaji bora, mfungaji bora wala kipa bora, ingawa lipo jopo la kuwachagua, jambo hili linaonekana kuwakatisha tama vijana ambao wanaona hakuna thamani ya kusakata kabumbu kwa kutoa jasho, wakati hakuna wanachovuna.

Fedha za wadhamini ‘kizungumkuti’

Imebainika kuwa, katika fedha zilizotolewa na wadhamini, Azam, kila timu imepewa kiasi chake, jambo linalozua utata miongoni mwa washiriki.

Mfano mzuri ni katika timu ya Viva Queens, ambao wao wamepewa kiasi cha Sh milioni 10 hadi ligi itakapomalizika, wakati Marsh Academy ya mkoani Mwanza wakiingiziwa Sh milioni 11.5 kwenye akaunti yao kwa awamu tofauti tofauti, kitu ambacho kinaonekana hakina usawa, ukizingatia timu zote zinacheza ligi moja.

Posho za waamuzi

Ni vigumu mwamuzi kutenda kazi yake ipasavyo kwa kutumia sheria 17 za soka kama hajaweka chochote mfukoni.

Inaelezwa kuwa, TFF hadi sasa imeshindwa kuwalipa posho waamuzi katika mashindano hayo, huku ikiwa ni sababu mojawapo inayowaingiza katika vitendo vya kupokea  rushwa.

Jambo hilo limethibitishwa na mmoja wa waamuzi kutoka kituo cha Dar es Salaam, aliyetaka kuhifadhiwa jina, ambaye anasema TFF wamekuwa wakiwapiga kalenda kuwapa  posho kiasi cha kwamba wamejikuta wakitumia fedha  zao za mfukoni ili kukidhi mahitaji yao.

“Naweza kusema TFF wameamua kutukopa, japokuwa hatujui lini  tutalipwa, kiukweli waamuzi tunafanya kazi ili kutimiza wajibu wetu, kwani tunadai fedha za posho,” anasema.

Kucheleweshwa kwa mgawo wa fedha

Licha ya kila timu kupewa kiasi tofauti cha fedha, lakini bado malipo hayo hayatolewi kwa wakati, jambo mbalo linasababisha viongozi wa timu shiriki kutoa fedha zao ili kutatua baadhi ya mahitaji.

Zipo timu zinatoka mbali na kujikuta zinachelewa katika kituo walichopangiwa kucheza mechi, kutokana na kucheleweshewa fedha zitakazoiwezesha kusafiri.

Kutokana na kutofika katika kituo  kwa wakati, kunasababisha pia timu kujikuta zikiambulia mvua ya mabao kutoka kwa wenyeji wao.

Panga, pangua ya ratiba

Kama kawaida ya TFF kupangua ratiba za ligi, ndivyo inavyojiri katika soka la wanawake, baada ya kupanguliwa kwa mechi kadhaa.

Ligi hiyo iliyoanza Novemba Mosi mwaka huu, baada ya kuchezwa mechi za ufunguzi, ililazimika kupanguliwa kwa michezo miwili kwa kupelekwa mbele kupisha maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa timu ya soka ya Taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars dhidi ya Cameroon, uliochezwa katikati ya mwezi huu.

Panga hilo la kupanguliwa kwa mechi, lilizikuta timu za kundi A kati ya JKT Queens na Mlandizi Queens, ambapo mchezo wao ulikuwa uchezwe Novemba 8.

Kama inavyokuwa ligi kuu, baadhi ya wadau waliona kitendo hiko hakikuwa cha haki kwa kuwa ratiba ya michuano ya kimataifa kwa soka la wanawake ilikuwa ikijulikana, hivyo wakati wa upangaji wa ratiba ilitakiwa kuzingatiwa, kwani kupangua ratiba kunatoa fursa ya upangaji wa matokeo.

Kauli za wanamichezo

Sophia Mwasikili, mchezaji wa timu ya JKT Queens, anasema kuwa licha ya TFF kufanya jambo kubwa la kuleta ligi ya wanawake ya taifa, lakini kukosekana kwa wadhamini wakukidhi mahitaji kunasababisha morali ya wachezaji kupungua kila kukicha.

“Ili mtu aweze kuwa na morali ya kufanya kazi lazima ajue mwisho wa siku kitu gani atakipata, lakini katika ligi hii wachezaji wanacheza kwa maana ya kujifurahisha, kwani tayari imeshaelezwa zawadi ni kombe, tena kama litakuja kupatikana, lakini pia suala la waamuzi kuzibeba baadhi ya timu linaonekana ni sugu kwa hapa Tanzania, kwa maana hiyo ili tupige hatua lazima yafanyike marekebisho makubwa kwenye uandaaji wa mashindano,” anasema Sophia.

Naye Katibu Mkuu wa timu ya Viva Queens, Happiness Guguluu, anasema fedha zilizotolewa hazilingani na mahitaji husika, kwani timu inatakiwa kusafiri kwenye mikoa tofauti, kupata vifaa bora vya michezo, hivyo hulazimika kutumia gharama kubwa kuliko kiasi kilichotolewa na TFF.

“Ukiangalia timu yetu ina mapungufu mengi, ikiwemo kupata wachezaji wenye uwezo finyu, mipango yetu ni kuona tunasajili katika usajili utakaofunguliwa, lakini hadi sasa hatujajua tutawezaje kufanya hivyo kwa kuwa kiwango kilichotolewa na TFF ni kidogo na kinahitajika kutatua matatizo yote,” anasema Happiness.

Kwa upande wake, Katibu wa Marsh Academy kutoka mkoani Mwanza, Ahmad Mohamed, anasema ni wakati wa TFF kuwapima waamuzi  uwezo na kuwapa mechi za kuchezesha, kwani wapo baadhi yao wanashindwa kutafsiri sheria 17 za mchezo huo.

“Licha ya ukata tunaokabiliwa nao kiasi cha kushindwa kufika kwenye vituo vyetu kwa wakati, lakini pia waamuzi wanaonekana kuwa tatizo kubwa kwenye mashindano haya kwa kushindwa kutafsiri sheria 17 za mchezo, kwani muda mwingine wanaonekana kuzibeba  timu za mikoa hayo na hii inapelekea kutoendeka haki,” anasema Mohamed.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles