Na Walrer  Mguluchuma-Sumbawanga
MWANAMKE aitwaye  Noelia   Pintilila  (80)  Mkazi wa  Kijiji cha   Kanyezi  Tarafa ya  Mwazye,  Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa ameuwawa kwa kupigwa kichwani na  fimbo baada ya kutuhumiwa kuwa ni mchawi .
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa,  Geoge  Kyando  aliwaambia waandishi wa  habari  jana  kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa tano  asubuhi kijijini hapo .
Alisema siku hiyo ya tukio marehemu alikuwa nyumbani kwake akiwa anaendelea na shughuli ndogo ndogo za kila siku mara baada ya kuwa  amemaliza kunywa  chai ya asubuhi .
Kamanda Kyando  alieleza wakati marehemu akiwa  anaendelea na shughuli zake   alifika  mtuhumiwa wa mauaji hayo  ambae jina  lake  limehifadhiwa  alikuwa ni mgonjwa wa kifafa  na ndipo  alipomshuku marehemu  kuwa  ni  mchawi amemroga ugonjwa wa kifafa .
Hata hivyo marehemu    alimkatalia kuwa yeye si mchawi na wala tabia hiyo ya ushirikina  tangu  kuzaliwa  hajawahi kuwa nayo.
Licha ya kujitetea huko mtuhumiwa huyo aliendelea  kumshutumu  kikongwe huyo kuwa yeye  ni mchawi na ndiye  aliyemroga  ugonjwa wa kifafa.
Baada ya mabishano hayo kuendelea  kwa muda mrefu  ndipo mtuhumiwa alipoanza kumpiga kwa fimbo   kichwani marehemu Noelia   hadi kufariki  dunia  hapo hapo .