26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

KIFO CHA KOFI ANNAN USINGIZINI CHATIKISA DUNIA

GENEVA, USWISI              |                   


SIMANZI imetawala duniani baada ya kifo cha Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan.

Annan amefariki dunia usingizini nyumbani kwake mjini Geneva, Uswisi jana akiwa na umri wa miaka 80, kutokana na kuugua kwa muda mfupi.

Raia huyo wa Ghana, alikuwa Katibu Mkuu wa saba wa UN na mshindi wa tuzo ya kimataifa ya Amani ya Nobel aliyoipata mwaka 2001.

Taarifa ya kifo chake ilitolewa jana kwa pamoja kati ya familia yake na taasisi yake ya Kofi Annan aliyokuwa akiiongoza.

“Kwa masikitiko makubwa, familia ya Annan na taasisi ya Kofi Annan Foundation zinatangaza kifo cha Katibu Mkuu wa zamani wa UN na mshindi wa Tuzo ya amani ya Nobel kilichotokea leo (jana) baada ya kuugua kwa muda mfupi na kufariki akiwa usingizini.

“Katika kipindi chote alichokuwa akiugua hadi mauti yalipomkuta, alikuwa pamoja na mkewe Nane na watoto wake Ama, Kojo na Nina.

“Familia inaomba faragha wakati huu wa maombolezo na mipango ya mazishi itatangazwa baadaye,” ilisema taarifa hiyo.

 MWEUSI WA KWANZA KUONGOZA UN

Annan alizaliwa Aprili 8, 1938 katika Kitongoji cha Kofandros, Kumasi nchini Ghana.

Elimu yake ya awali aliipata katika Shule ya Mfantsipim (1954 hadi 1957).

Mwaka 1958 alijiunga na Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Kumasi (sasa Chuo Kikuu cha Kwame Nkrumah).

Baada ya kuhitimu elimu nchini Ghana, alijiunga na Chuo cha Macalester kilichopo Jimbo la Minnesota nchini Marekani.

Alikuwa mwanadiplomasia, mpole na mtulivu.

Alijulikana kwa kuongoza kwa uthabiti UN katika siasa za kimataifa, tangu mwaka 1997 hadi 2006 akiwa Mwafrika mweuzi wa kwanza kukalia kiti hicho.

Wakati akiingia madarakani mwaka 1997, alipokea kijiti cha uongozi kutoka kwa Katibu mwenza wa Bara la Afrika, Boutros Boutros-Ghali, ambaye ni raia wa Misri.

Boutros alilazimika kuondoka madarakani baada ya jaribio lake la kuwania awamu ya pili kukumbana na kura ya turufu (veto) na taifa la Marekani, hivyo kukosa sifa.

KABLA YA KUWA KATIBU MKUU

Alijiunga na UN mwaka 1962 kama ofisa wa ngazi za chini wa Shirika la Afya la UN mjini Geneva.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa UN, alikuwa Mkurugenzi wa vikosi vya kulinda amani vya UN katika nchi ya zamani ya Yugoslavia.

Vikosi hivyo yakishirikiana na Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO), yalilinda Jimbo la Bosnia. Kwa sasa Bosnia na Herzegovina ni nchi ya Ulaya Kusini-Mashariki katika Rasi ya Balkani. 

UMAHIRI NA SIFA ZA UONGOZI

Akiwa UN, Annan alianzisha Mpango wa Maendeleo wa Milenia (MDG’s), Mpango wa Kupambana na Mambukizi ya Ukimwi (Global Fund to Fight AIDS), Malaria na Kifua Kikuu.

Hakuishia hapo, bali amekuwa Katibu Mkuu wa kwanza kuanzisha taasisi ya UN inayoshughulikia mapambano dhidi ya ugaidi.

Mwaka 2001, dunia ilishuhudia mwanadiplomasia huyo akitangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kutokana na uongozi wake ndani ya UN.

Pia wakati Kamati ya Tuzo ya Amani ya Nobel ilipomtangaza kuwa mshindi, ilimmwagia sifa kutokana na mipango madhubuti ya kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi barani Afrika na kupinga ugaidi.

“Kofi Annan alikuwa injini ya mambo mengi mazuri tuliyonayo. Ni huzuni kumpoteza mtu muhimu kama yeye ambaye amewafundisha wengi masuala ya uongozi wake.

“Kwa namna fulani Annan alikuwa ndiye Umoja wa Mataifa. Alipanda ngazi kutoka moja hadi nyingine hadi kuukwaa ukatibu mkuu, akiwa ameacha alama kubwa,” alisema jana Katibu Mkuu wa sasa wa UN, Antonio Guterres.

Annan alikuwa kiongozi wa kimataifa aliyepigania amani na utulivu kwenye mataifa mbalimbali duniani.

Katika kipindi cha uongozi wake, alipambana kwa kila fursa aliyopata ili kuhakikisha dunia inakuwa sehemu yenye amani, maendeleo, haki na utawala wa sheria.

Baada ya kustaafu UN, aliendelea na kazi yake ya usuluhishi na kutafuta amani kupitia taasisi yake na mwaka 2007 alikuwa mwanzilishi wa Asasi ya The Elders yenye dhumuni la kupigania amani na haki za binadamu duniani iliyomjumuisha pia Nelson Mandela. 

UPATANISHI KENYA

Annan alikuwa mpatanishi mkuu wa mgogoro wa kisiasa nchini Kenya baada ya kuzuka ghasia zilizosababishwa na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.

Katika uchaguzi huo, Mwai Kibaki alitangazwa mshindi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Samuel Kivuitu hatua iliyozusha machafuko ikidaiwa haukuwa ushindi halali, huku wengi wakiamini aliyeshinda alikuwa Raila Odinga wa Chama cha ODM.

Nchini Kenya, Annan anakumbukwa kama mwanadiplomasia aliyenusuru maisha yao na mtu muhimu katika ustawi wa taifa hilo hadi leo.

Katika ghasia hizo, watu zaidi ya 1,000 walifariki dunia na wengine 600,000 wakakimbia makazi yao baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa. 

BENDERA KUPEPEA NUSU MLINGOTI

Rais wa Ghana, Nana Addo Dankwa Akufo-Addo, ametangaza kuwa Serikali ya nchi hiyo itahakikisha inapeperusha bendera za taifa nusu mlingoti ikiwa ni ishara ya kuombeleza kifo cha Annan.

Taarifa hiyo imetolewa na Akufo mwenyewe kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

“Kwa niaba ya Serikali, wananchi wote wa Ghana, mke wa rais, Rebbeca, tumepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwenzetu Annan kilichotokea Berne nchini Uswisi.

“Kwa niaba ya wananchi wa Ghana, wote tumeumizwa na kifo hicho na tunatoa rambirambi kwa mjane wa Annan, Nane Maria, pamoja na watoto wake Ama, Kojo na Nina kwa kumpoteza mtu muhimu maishani mwao.

“Hata hivyo, baada ya kuzungumza na mjane Nane Maria, amenijulisha kuwa Annan amefariki kimya kimya akiwa usingizini.

“Kofi ni rafiki na mwanadiplomasia mwenye heshima kubwa duniani na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa wa kwanza kutoka ukanda wa nchi za Jangwa la Sahara kushika wadhifa huo.

“Nimetoa maagizo, kwamba kwa heshima yake, bendera ya taifa ya Ghana itapepea nusu mlingoti nchini kote na ofisi zote za ubalozi wetu duniani kwa wiki moja kuanzia Agosti 20, mwaka huu. Apumzike kwa amani,” alisema Rais Akufo. 

VIONGOZI WAMLILIA ANNAN

UINGEREZA: Waziri Mkuu, Theresa May, alisema; “Ni huzuni kubwa kusikia kifo cha Kofi Annan. Kioo cha uongozi na mtu aliyefanya mabadiliko makubwa ndani ya Umoja wa Mataifa, mchango wake ni mkubwa ambao umeonekana sehemu mbalimbali duniani. Daima aliamini dunia inaweza kuwa sehemu salama. Natoa pole na rambirambi kwa watu wote pamoja na familia yake.”

NEW ZEALAND: Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern, alisema; “Dunia imempoteza muungwana, kiongozi na mtu msumbufu wa kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake. Pumzika kwa amani Kofi Annan.”

AUSTRALIA: Waziri Mkuu wa zamani wa Australia, Kevin Rudd, alisema; “Dunia imempoteza kiongozi mkubwa leo (jana). Kofi ndiye mwanzilishi wa MDG’s. Alifanya jitihada kubwa kuzuia vita ya Irak. Alizungumzia umoja. Hakika nitamkosa sana rafiki mwema kama yeye.”

INDIA: Waziri Mkuu wa India, Narenda Modi, ametoa salamu za rambirambi kutokana na kifo hicho na kusisitiza kuwa Afrika na dunia zimempoteza mtu muhimu.

EU: Mwenyekiti mwenza wa Bunge la Ulaya la Mahusiano ya Kimataifa na waziri mkuu wa zamani wa Sweden, Carl Bildt, amesikitishwa pia na kifo hicho akisema; “Mtu mtaratibu, mwenye busara na hekima na rafiki ametuacha leo (jana).”

KENYA: Spika wa Bunge la Kenya, J. B. Muturi ametoa salamu za rambirambi kwa wananchi wa Ghana na familia yake kwa kueleza; “Kofi Annan, ni Mwafrika mweusi wa kwanza kuongoza Umoja wa Mataifa. Annan alitimiza wajibu na alipenda amani duniani.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles