33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MDEE ATAKA PAC ISIINGILIWE SAKATA LA TRIL. 1.5/-

Na Aziza Masoud -Dar es Salaam                  |                  


MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), amesema Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) itatoa majibu sahihi ya sakata la Sh trilioni 1.5 zilizotajwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kama itajadili suala hilo kwa uhuru bila kuingiliwa.

Kauli ya Mdee imekuja siku moja baada ya Kitengo cha Habari, Elimu kwa Umma na Mawasiliano cha Ofisi ya Bunge, kutoa taarifa ya Spika Job Ndugai kuiita PAC na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) wiki ijayo, kuchambua taarifa ya CAG  kwa mwaka ulioishia Juni 30, mwaka jana.

Katika taarifa ya CAG, miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa, ni kuhusu sakata hilo la Sh trilioni 1.5 ambazo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) alilishikia kidedea.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Mdee ambaye alikuwa miongoni mwa wachangiaji wa suala hilo, alisema  PAC itaweza kutoa majibu sahihi ya sakata hilo na Bunge kutoa maazimio ya kuwawajibisha wahusika ikiwa watafanya kazi hiyo bila kuingiliwa.

“Kiutaratibu kazi ya PAC ni kukagua taarifa za CAG, baada ya hapo taarifa zinaletwa bungeni, lakini kwa suala hili la Sh trilioni 1.5 ambalo lilikuwa mjadala katika Bunge lililopita, kwa uzoefu wangu wa ndani ya Bunge, nadhani litaletwa bungeni katika Bunge la Januari mwakani, taarifa hizi haziwezi kupatikana Bunge hili,” alisema.

Alisema ili kupata taarifa hizo, PAC inapaswa kuwaita wadau wanaoshughulikia ukusanyaji wa mapato hayo, ikiwamo Mamlaka ya Mapato (TRA), Ofisi ya Hazina na wengine ambao wataeleza mahali ilipojitokeza tofauti hiyo ya fedha.

“Ninachokiona kamati itakuwa na changamoto ya presha kubwa kutoka nje, watu wa nje watawatumia wajumbe kufunika hili suala, lakini kamati ikiachwa kuwa huru tutapata majibu mazuri.

“Sisi kama wabunge tunatarajia kamati itatoa majibu sahihi, hasa ukizingatia mwenyekiti wake (Naghenjwa Kaboyoka) anatoka upinzani, tunaamini PAC watafanya kazi hii kwa weledi na si kufunika kombe mwanaharamu apite na wala atutarajii kuwa na vikwazo kutoka Serikali kuu,” alisema Mdee.

Alisema Serikali kuu inapaswa kukaa pembeni katika suala hili kwa sababu tayari walishajichanganya kusema fedha hizo zilipelekwa katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakati hazikwenda.

“Kuna dhamira ya kufichaficha suala hili la trilioni 1.5, lakini naamini halitafichwa na kamati haitahongwa, naiomba itumie nafasi yake kutoa ukweli wa suala hili,” alisema Mdee.

Alisema PAC imekuwa ikifanya kazi ya kuibua mambo, lakini inakwamishwa na baadhi ya watu waliopo serikalini, huku akitolea  mfano sakata la mkataba wa Lugumi.

“Yaani hili suala tusipoangalia linaweza likaenda kama la Lugumi, PAC mwaka 2016 walitaka kupata undani kuhusu suala la Lugumi (Said Lugumi, mmiliki wa Kampuni ya Lugumi iliyopewa tenda ya kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole katika vituo vya polisi), wakaomba kufanya uchunguzi,  lakini kilichotokea baada ya uchunguzi wakagundua mambo mengi yalifunikwa na hii ilitokana baada ya Serikali kuingilia,” alisema Mdee.

Alisema ili kuepuka yaliyotokea kwa Lugumi, mamlaka za Serikali zinapaswa kupeleka vithibitisho kwa kamati na baada ya hapo Bunge litoe maazimio ya kuwawajibisha wahusika.

Mdee alisema mara kadhaa ripoti zinazowakilishwa bungeni huwa zinakuwa na kasoro kwenye makusanyo na kudai kwamba  fedha hizo huenda zinakuwa zimeibwa ama zinakuwa na kasoro.

Gazeti hili pia lilimtafuta Mwenyekiti wa PAC, Kaboyoka, ambaye alisema atakuwa na nafasi nzuri ya kulizungumzia suala hilo kesho.

“Kwa sasa ndiyo nimeshuka  kwenye ndege, nipo Airport (Uwanja wa ndege) natoka Marekani, nimechoka, sidhani hata kama nitaweza kuongelea suala hilo, maana kichwa changu hakijatulia, naomba unitafate Jumatatu (kesho) tunaweza tukaongea vizuri,” alisema Kaboyoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles