31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kiama cha wafanyabiashara chaja  

EFDsNA ARODIA PETER, DODOMA

WAFANYABIASHARA watakaokaidi kutumia mashine za kutoa risiti za elektroniki (EFDs) watafutiwa leseni za biashara kwa   miaka miwili.

Adhabu hiyo imependekezwa na Serikali katika Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2016 uliowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Muswada huo uliogawanyika katika sehemu 17 pia ‘umezibana mbavu’ kampuni za mawasiliano nchini kwa kuzitaka zijisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE)   na kutenga asilimia 25 ya hisa zake kwa ajili ya Watanzania ndani ya miezi sita kuanzia Julai mosi mwaka huu.

Vilevile, Sheria  ya Kodi ya Mapato imeweka utaratibu mpya wa ukokotoaji wa kodi katika kampuni za mafuta na gesi.

Akiwasilisha muswada huo bungeni jana, Dk. Mpango alisema sheria ya leseni za biashara imerekebishwa na kuingizwa kifungu hicho cha adhabu kwa lengo la kuzuia ukwepaji kodi unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Kuhusu kampuni za mawasiliano, sheria hiyo inazitaka kuweka tafsiri ya neno ‘local shareholder’ katika katiba zao   kuwezesha Watanzania kumiliki hisa zitakazouzwa na kampuni hizo kupitia soko la hisa la Tanzania.

Sheria hiyo pia itatumika kuthibitisha muundo wa umiliki wa hisa kama mojawapo ya taarifa zinazopaswa kuwasilishwa wakati wa kuomba leseni na litakuwa ni kosa kwa kampuni itakayoshindwa kutenga asilimia 25 za hisa kwa Watanzania.

“Kupitia hatua hii, kampuni za mawasiliano ya  elektroniki ambazo zimesajiliwa   nchini  zitawajibika kujiorodhesha na kuuza hisa zao ndani ya miezi sita kuanzia Julai mosi mwaka huu na zile zitakazosajiliwa baada ya muda huo, zitalazimika kuuza na kujiorodhesha katika soko hilo kwa kipindi cha miaka miwili.

“Sheria ya miamala ya simu imerekebishwa ili kutoza asilimia 10 ya ushuru wa bidhaa kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma wa simu katika kutuma fedha na kutoa fedha pekee.

“Lengo ni kuzuia ukwepaji kodi kwa baadhi ya kampuni za simu kwa kufanya sehemu ya ada ya utumaji kuwa sehemu ya ada ya mpokeaji na hivyo kuwa nje ya kodi.

“Sheria hii pia inapendekeza kuanzisha divisheni mpya ndani ya sheria ya kodi ya mapato   kuweka utaratibu mpya wa kutoza na kukokotoa kodi ya mapato kwa kampuni za madini, mafuta na gesi.

“Hata hivyo, baadhi ya vifungu vinabainisha kuwa  malipo ya ziada hayatapunguzwa kwenye mapato ya kampuni za madini, mafuta na gesi,” inasema sehemu ya muswada huo.

Dk.Mpango alisema   katika muswada huo, marekebisho yatafanywa  kumpa nguvu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kukadiria mapato yanayotokana na pango  kuiwezesha TRA kutoza kodi kwenye mapato ya mikataba ya kupangisha nyumba ili kuongeza ufanisi kwa kutoza kodi halisi na sahihi.

Dk. Mpango pia alisema kutakuwa na kifungu kipya cha sheria  kuwezesha bidhaa zinazotengenezwa Tanzania Bara na kuuzwa Zanzibar  zitozwe kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Kwa mujibu wa Dk. Mpango, lengo la sheria hiyo ni kuondoa utaratibu wa awali wa kufanya marejesho ya VAT kwenda Zanzibar.

Kwa msingi huo, alisema,  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), itakusanya kodi hiyo kwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara na kupelekwa huko.

 

Maoni ya kamati

  Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia, alisema kamati yake inakubaliana na muswada huo ingawa ilikosoa baadhi ya maeneo.

Ghasia alisema Serikali ina haja ya kubadili madaraja yanayotumika katika kupanga kodi ya mapato kwa sababu kundi kubwa la watumishi wa umma wanakatwa kodi ya mapato kati ya asilimia 20 na 30.

Kuhusu matumizi ya EFD’s, kamati hiyo imeonyesha wasiwasi juu ya adhabu inayopendekezwa ya kufutwa   leseni ya biashara kwa   miaka miwili ikisema kwamba inaweza kuzua mgogoro kati ya Serikali na sekta binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles