26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Hakuna siasa mpaka 2020

Tanzania's President elect Magufuli addresses members of the ruling CCM at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam*Asema ni wakati wa kazi, atamani kuongoza awamu moja

* Wapinzani, wadauwampinga wadai anataka kuua demokrasia

Elizabeth Hombo na Johanes Respichius, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli amepiga marufuku vyama kufanya ushindani wa siasa mpaka baada ya miaka mitano ili wananchi wahoji wanasiasa kama wametekeleza yale waliyoyaahidi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alitoa kauli hiyo  Ikulu Dar es Salaam jana baada ya kukabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva.

“Niwaombe wanasiasa wenzangu wafanye siasa za ushindani kwa nguvu zote baada ya miaka mitano  ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi kama tumeyatekeleza au hatujayetekeleza.

“Kila nchi hata zile zilizobobea kwenye demokrasia unapokwisha uchaguzi unakuwa ni wakati wa kazi.

“Haiwezekani mkawa   kila siku ni siasa watu watalima saa ngapi?  Kila siku ni siasa, ni vema tukatimiza wajibu wetu tuliopewa na wananchi na  watatupima kwenye hilo.

“Ni matumaini yangu kuwa Watanzania tunaowaongoza wanataka maendeleo. Iwe kwa bahati nzuri au mbaya Serikali inayoongoza ni ya Chama Cha Mapinduzi.

“Yapo tuliyoyaahidi kuyatekeleza kwa wananchi katika kipindi cha miaka mitano, nisingependa kuona mtu yeyote ananichelewesha kutekeleza hayo niliyoahidi kwa kipindi cha miaka mitano,” alisema Rais Magufuli.

Alisema ushindani wa sasa ambao unatakiwa ufanywe kwa nguvu ni kwa wale wawakilishi waliopewa mamlaka na wananchi kupeleka hoja zao kwenye maeneo yao.

“Kama ni madiwani wakapeleke hoja kwa nguvu zote kwenye maeneo yao, kama ni wabunge wakazungumze kwa nguvu sana bungeni lakini hata kuziba midomo nayo ni demokrasia, hiyo ni demokrasia ya mwelekeo wa ya aina yake,”alisema.

Alisema ingawa watu mbalimbali walijitokeza kugombea katika uchaguzi wa mwaka jana,   uchaguzi huo haukuwa na mshindi wala mshindwa na kwamba Watanzania wote ni washindi.

“Uchaguzi umekwisha, wakati wa uchaguzi watu mbalimbali walijitokeza kugombea wengine wakaibuka washindi lakini naomba niwaambie kwamba uchaguzi huu haukuwa na mshindi wala mshindwa, sisi Watanzania wote kwa umoja wetu ni washindi,”alisema.

Alisema Serikali yake imeamua kufanya kazi kwa kushirikiana na vyama vyote vya siasa lengo likiwa ni kutatua kero za wananchi na  atalisimamia hilo kwa nguvu zote kwa kuwa ni wajibu wake.

Rais aliahidi kushirikiana na wanasiasa katika changamoto zote zenye kujenga taifa na ushauri na maombi ya vyama hivyo vya siasa atavipokea kwa mikono yake miwili.

AMTETEA JK

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alimtaka Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete  kutokuwa na wasiwasi kuhusu  maneno ambayo amekuwa akirushiwa na baadhi ya wanasiasa juu ya utawala wake.

Alisema ni jukumu lake kuhakikisha rais huyo   na marais wengine wastaafu wanakuwa salama.

“Kipekee ninawashukuru viongozi wa Serikali, nikianzia na Mheshimiwa Jakaya Kikwete, kwanza kwa kutenga bajeti ya Tume…nakushukuru sana.

“Wewe ukae utulie kwa raha zotee…wala usisikilize kelele nyingine hizi za ovyo ovyo, wewe uko salama na hilo ndilo jukumu langu la kufanya kama Rais wa awamu ya tano, kuhakikisha wastaafu wote wanakaa kwa usalama na kwa raha.

“Viongozi wastaafu wote katika maeneo yao yote, tutawalinda. Watachonga weee…lakini nitahakikisha mnaishi kwa amani kwa sababu mna mchango mkubwa katika taifa hili.

“Kwa upande wa Zanzibar vile vile namshukuru Dk. Shein kwa kuweza kutenga bajeti na kuiwezesha ZEC kufanya uchaguzi na bahati nzuri wewe umepiga mara mbili na ukashinda, ulikuwa umejiandaa nakupongeza sana,”alisema Rais Magufuli.

KATIBA MPYA

Akizungumzia  Katiba mpya, alimshukuru Rais Mstaafu Kikwete kwa kumrahisishia kazi kuhusu mchakato wa Katiba mpya, akisema ulifika mahali pazuri hivyo atauendeleza   ulipoishia.

“Mchakato wa katiba ulifika mahali pazuri sana…namshukuru sana mheshimiwa Jakaya Kikwete, Dk. Shein (Rais wa Zanzibar), Samia (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba), mzee Sitta (aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba),  kwa jinsi walivyofanya kazi kubwa.

“Lakini pia namshukuru Warioba (Joseph, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya)  na tume yake kwa jinsi walivyotoa mchango wao, tumefikia mahali pazuri.

“Mheshimiwa Jakaya Kikwete umenirahisishia kazi, nitaendeleza ulikoishia kusudi nipamalizie.  Hivyo  Mwenyekiti wa tume ilikuwa ni vigumu kuwabebesha wanyamwezi mizigo miwili, hapa mnyamwezi alikuwa ni Kikwete. Haya mengine tutayafanyia kazi,”alisema Rais Magufuli.

AMJIBU JENERALI ULIMWENGU

Katika kile kilichoonekana kuwa kumjibu mwanahabari mkongwe na mchambuzi wa masuala ya siasa, Jenerali Ulimwengu (ingawa hakumtaja jina), Rais Magufuli alieleza kushangazwa kwa kitendo cha mwanahabari huyo kutaka Rais Kikwete ashtakiwe.

Wiki iliyopita akizungumza katika Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere, Ulimwengu alisema Kikwete anapaswa kushtakiwa kama viongozi wengine kwa kuisababishia hasara taifa kwa kutumia mabilioni ya fedha kwenye mchakato wa Katiba mpya huku ikiwa haijapatikana.

“Ninawashangaa sana wengine mambo wanayoyazungumza wakati mwingine ni ya ovyoooo…sijui fulani ashtakiwe mbona mimi nilikuwapo mbona hawakusema nishtakiwe?” alihoji Rais Magufuli.

ATAMANI KUONGOZA AWAMU MOJA

Alisema kutokana na changamoto za aina hiyo na ambazo amezishuhudia alipoingia madarakani, anatamani aongoze kwa miaka mitano tu.

“Lakini hizo ndizo changamoto za uongozi, mabaya yote ni yako na mimi nimeyashuhudia nilipoingia tu…nikasema kama ndiyo hii kazi ni vizuri unakaa miaka mitano halafu unaondoka.

“Uongozi ni msalaba ndiyo maana wakati mwingine inahitajika nguvu ya Mungu na ndiyo maana mara nyingi nimekuwa nikisema mniombee,”alisema.

USHINDANI MKALI

Akizungumzia kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli alisema uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkali, mvuto na msisimko wa  pekee ndani na nje ya nchi.

“Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa vyote kwa kushiriki kwa ukamilifu katika uchaguzi kwa kuonyesha ukomavu wa siasa katika nchi yetu.

“Uchaguzi ni nguzo muhimu ya kukuza demokrasia katika nchi na tumeona katika nchi mbalimbali jinsi uchaguzi ulivyovuruga amani.

“Uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulikuwa wa pekee sana kwa sababu ulikuwa wa kwanza kufanyika kwa mfumo elektroniki yaani BVR.

“Hivyo tume ililazimika kuboresha daftari la kupigia kura na iliweza kukamilisha hatua hiyo pamoja na kwamba ulikuwapo  ufinyu wa muda,”alisema.

Alisema kutokana na ushindani huo baadhi ya watu walionyesha wasiwasi wao kwamba  amani na utulivu wa nchi ingepotea.

“Hata hivyo, tumemaliza kwa utulivu na amani haya yote ni matokeo ya NEC, vyombo vya ulinzi, vyama vya siasa na Watanzania kwa ujumla,” alisema.

Alisema zipo kasoro zilizojitokeza na   jambo hilo lisiwanyime raha Tume kwa kuwa ni la kawaida.

“Ni jambo la kawaida kabisa…hakuna nchi hapa duniani ambayo imefanya uchaguzi isitokee kasoro. Pamoja na ukweli huo wametokea wakosoaji.

“Wakosoaji hao ni wa aina mbili; kundi la kwanza limetaja upungufu wa msingi kwa lengo la kuboresha uchaguzi wetu, naomba tume mpokee upungufu huo na muufanyie kazi.

“Kundi la pili;  wakosoaji ambao wao lazima wakosoe tu, hawa hata mngefanyeje lazima watawakosoa tu hawana njema.

“Mtunzi wa kitabu, Ben Carson alipata kusema kuwa; ‘even if you dance in water, your enemies will accuse you of raising dust… yaani hata kama ungecheza kwenye maji wenye husuda watasema unawatimulia vumbi’ mwisho wa kunukuu,”alisema Rais Magufuli.

Alisema wakosoaji wa namna hiyo kwao ili uchaguzi uonekane kuwa wa huru na haki lazima chama tawala kishindwe na   kikishinda maana yake uchaguzi si wa huru.

“Ninyi wenyewe mmeshuhudia wakati wanalaumu kwa upungufu uliojitokeza kule Zanzibar ambao ulidhihirika kuwa una upungufu.

“Lakini mimi sishangai wanailaumu ZEC kwa kufuta uchaguzi kwa sababu imekuwa ni tabia yao. Kwa wakosoaji wa namna hii ninawafananisha na wale wanaozunguka kila siku sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi wakiilaumu Serikali ya Jamhuri kuwa inaingilia masuala ya ndani ya Zanzibar.

“Ni hao hao wanaotaka  ZEC iwe huru lakini baada ya uchaguzi kufutwa watu hao hao wakataka mimi niingilie ili nitengue uamuzi wa ZEC, wazungu wangesema hii ni ‘contradiction’ lakini wakajisahaulisha kuwa ZEC ina mamlaka yake na ZEC ni chombo huru hivyo uamuzi wake hauingiliwi na mtu yeyote.

“Mimi nikasema hapana maana naheshimu katiba na sheria. Naheshimu mamlaka ya Zanzibar na uhuru wa ZEC. Lakini niliahaidi kuwa Zanzibar itaendelea kuwa ya amani na utulivu lakini hilo lilithibitika…uchaguzi wa marudio umefanyika huku amani na utulivu ikiendelea,”alisema.

Aliitaka Tume kuendelea kutoa elimu ya mpiga kura na kusimamia uchaguzi mdogo unaojitokeza na kuanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

NEC KUJENGWA DODOMA

Kuhusu tume kutumia jengo la kupanga, alisema Sh bilioni 12 alizokabidhiwa na NEC hivi karibuni zitatumika kujenga ofisi ya tume hiyo mjini Dodoma.

“Mmepanga katika majengo matatu hii si sawa kabisa  na nimesikia mnalipa Sh bilioni 1.3 kila mwaka kwa ajili ya kupanga.

“Hivyo kutokana na unyeti wa shughuli za tume hampaswi kutumia jengo la kupanga. Zile bilioni 12 mlizonikabidhi tutawapa ili mzitumie kwa ajili ya kujenga jingo lenu.

“Ningependa majengo hayo yajengwe Dodoma   kusudi wadau wako wa vyama vya siasa wafike Dodoma… nitashangaa ukishindwa kufika Dodoma maana na wewe Lubuva huko ni kwenu.

“Tukifanya hivyo tutakuwa tumetimiza ndoto ya Baba wa Taifa ya kuhamia Dodoma. Tukihamia Dodoma tutakuwa tumepunguza msongomano katika jiji la Dar es Salaama. Mniambie tu mmepata kiwanja halafu waziri anayehusika na fedha atawapa hizo bilioni 12.

JAJI LUBUVA

Awali, akikabidhi ripoti hiyo ya uchaguzi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, alisema ingawa tume hiyo haijaainishwa kwenye katiba kama nchi nyingine kuwa ni huru, lakini iliendesha uchaguzi kwa amani, haki na uwazi.

Alisema kutumia mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR), kuandikisha wapiga kura utawezesha daftari hilo kutumika kwenye uchaguzi mwingine.

Jaji Lubuva alisema changamoto ambazo zimekuwa zikikwamisha shughuli za tume  ni pamoja na kucheleweshwa  fedha za kuendesha uchaguzi.

KURA YA MAONI

Akizungumzia  kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa, iliyokuwa ifanyike Aprili 31 mwaka jana, Jaji Lubuva alisema Tume haikufurahishwa na kitendo cha Serikali kuahirisha kura hiyo ya maoni.

“Tume haikufurahishwa na kuahirishwa  kura ya maoni na Rais Msaafu, Jakaya Kikwete na nikiri isingewezekana mtu mmoja akabeba mizigo miwili kwa wakati mmoja kwani ilikuwa na jukumu kubwa la kuandaa Uchaguzi, lakini sasa Tume iko tayari kuanza mchakato wa kura ya maoni,”alisema.

Alitaka sheria ya kura ya maoni ibadilishwe haraka kwa kuwa imepitwa na wakati na   NEC kwa kushirikiana na ZEC, zimeshaiandaa bado kuiwasilisha sehemu husika.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete,  Mawaziri Wakuu Wastaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba  na majaji, viongozi waandamizi wa serikali.

Wengine ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Ali Shein, Makamu wa Pili wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha.

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Mwenyekiti wa chama cha United Democratic Party (UDP), John Cheyo, Makamu Mwenyekiti wa  CCM, Philip Mangula, Meya wa Ilala, Charles Kuyeko na viongozi  wengine.

 

SUMAYE AMVAA MAGUFULI

Akitoa maoni kuhusu matamshi ya Rais Magufuli ya kutaka vyama visifanye siasa kwa miaka mitano, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye alisema hiyo itakuwa ni katiba yake mpya.

“Nchi hii inaenda kule tunakofikria…siasa ziku zote ipo hauwezi kusitisha. Nchi hii imekuwapo siku zote.

“Siasa za vyama vingi haikuanza leo na hakuna Katiba mpya iliyotungwa kwamba inazuia mikutano ya siasa.

“Sasa hayo anayoyasema Magufuli itakuwa ni katiba mpya ambayo sisi hatuijui…lakini Katiba inaruhusu, wote tuilinde,”alisema Sumaye ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

ZITTO

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema chama chake kinaichukulia kauli hiyo ya Rais Magufuli kama tangazo la vita dhidi ya demokrasia na uhai wa vyama vingi nchini.

“ACT-Wazalendo tumepokea kauli ya Rais kwa mshtuko na masikitiko makubwa. Tunaichukulia kauli yake kama tangazo la vita dhidi ya demokrasia na uhai wa vyama vingi nchini,”alisema.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini, alisema chama chake kitaitisha vikao vya dharura kujadili hali ya nchi na namna ya kukabiliana na mashambulio yanayoendelea dhidi ya demokrasia nchini.

“Tunatoa wito kwa vyama vyote vya siasa nchini kuunganisha nguvu katika kuhakikisha tunapigana vita hii pamoja.

“Huu ni wakati wa vyama vya siasa na wanasiasa kuacha tofauti zao na kupambana kulinda uhuru wa kufanya siasa wakati wowote kwa mujibu wa sheria.

“Tunatoa wito kwa wananchi wote na taasisi za raia kusimama imara katika kulinda demokrasia. Tunasisitiza kuwa ushahidi wa sayansi unaonyesha kuwa huwezi  kuua demokrasia bila kuua juhudi za maendeleo. Tusiruhusu mtu yeyote mwenye mamlaka kuua demokrasia nchini,”alisema Zitto.

 

LISSU

Mwanasheria Mkuu wa  Chadema, Tundu Lissu, alisema watu wanaolitakia mema taifa hili ni vema wakamzuia Rais Magufuli kwa sababu ataipeleka nchi kwenye udikteta.

“Huyu Rais anaishi dunia ya wapi?  Mimi sifahamu… kwa sababu kazi ya vyama vya siasa ni kufanya siasa, mikutano, maandamano na uchaguzi. Sasa hicho anachokisema ametoa kichwani mwake na si kwenye Katiba.

“Ni vema akazuiliwa… kwa speed anayokwenda nayo atatupeleka kwenye nchi ya udikteta. Watu wanaoitakia mema nchi hii wamzuie na aachie ngazi.

“Hivi utayaambia makanisa yasifanye mahubiri kwamba eti wasubiri Krismas na Pasaka?”alihoji Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.

SAKAYA

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya alisema  anachokitafuta Rais Magufuli ni machafuko kwa sababu anayotaka kuyafanya hayawezekani.

“Siasa ni maisha ya kila siku, haina muda. Hicho anachokisema ni udikteta na hicho anachokitafuta ni machafuko kwa sababu Katiba inahurusu mikutano, maandamano.

Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua, alisema ni yema   Katiba ikabadilishwa ijulikane kwamba nchi ni ya chama kimoja kuliko yanayofanyika hivi sasa.

MTATIRO

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Julius Mtatiro, alisema tafsiri ya Rais Magufuli ni kwamba vyombo vya dola visiruhusu shughuli za siasa za vyama vya upinzani hadi baada ya miaka mitano.

“Tulianza kuona dalili za jambo hilo kupitia vitendo na mwelekeo wa vyombo vya dola, sasa mkuu wa kaya ametamka hadharani.

“Magufuli is very serious on implementing these undemocratic aims (hana utani katika kutekeleza malengo haya yasiyo ya  demokrasia).

“Na kuanzia sasa vyama vya upinzani vitegemee mibinyo zaidi na udhibiti zaidi maana mkuu ameanza kulihubiri hilo hadharani kwani kwa vyombo vya dola vya Afrika, mapendekezo ya Rais ni utekelezaji,” alisema Mtatiro alieyepata kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles