25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya Wakili Mwale yahamia Mahakama Kuu

NA JANETH MUSHI, ARUSHA

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, inatarajia kuanza kusikiliza kesi ya utakatishaji fedha haramu inayomkabili wakili maarufu jijini hapa, Median Mwale na wenzake watatu.

Hatua hiyo ilikuja jana baada ya upande wa Jamhuri unaowakilishwa na Wakili Oswald Tibabyakomya, kudai kuwa umekamilisha upelelezi wa kesi hiyo.

Watuhumiwa wengine katika shauri hilo ni Don Bosco Gichana, Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi.

Mbele ya Hakimu Mfawidhi Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Augustine Rwizile, Tibabyakomya alidai mahakamani hapo, kuwa upande wa mashitaka una mashahidi 46 pamoja na vielelezo 60 vitakavyotumika katika kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.

Wakili huyo aliyekuwa akisaidiana na mawakili Awamu Mbagwa na Shedrack Kimaro, walidai mahakamani hapo kuwa taratibu za kupeleka mashitaka hayo Mahakama Kuu zimeshakamilika.

Pamoja na hayo, waliomba kufanya marekebisho katika mashitaka mawili katika kesi hiyo ambayo ni shitaka la 12 na shitaka la 13 yanayohusu kughushi nyaraka.

Hakimu Rwizile aliwaeleza washtakiwa hao, kuwa kesi hiyo imefikia hatua ya mwisho mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Kutokana na hali hiyo, alidai kuwa washitakiwa watapelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

“Tumefika mwisho leo (jana) baada ya upande wa mashitaka kusoma idadi na majina ya mashahidi na vielelezo vya kesi hii dhidi yenu.

“Kwa hiyo, shauri hili litapelekwa Mahakama Kuu ambayo ina mamlaka ya kusikilzia kesi hii na kwa kupitia mawakili wenu, mtapewa tarehe na muda wa kesi yenu kuanza kusikilizwa huko,”alisema Rwizile

Mwale na Don Bosco walikuwa wakitetewa na Mawakili Omary Omary na Innocent Mwanga, wakati Mwimbwa alikuwa akitetewa na Emanuel Mvula na Ndejembi alikuwa akitetewa na Mosses Mahuna.

Mashitaka mengine yanayowakabili watuhumiwa hao ni pamoja na kughushi nyaraka na kukutwa na mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu ambapo wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya mwaka 2009-2011 kwa nyakati tofauti.

Kati ya makosa hayo 42, mtuhumiwa Mwale anakabiliwa na makosa 27 ikiwa ni pamoja na kuficha uhalisia wa mali ambapo anadaiwa kutumia Sh milioni 70 kununua shamba lililopo katika Kijiji cha Ekenywa, wilayani Arumeru mkoani Arusha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles