Na ELIYA MBONEA-ARUSHA |
WAKILI wa kujitegemea, Jebra Kambole amefungua shauri katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, akipinga matokeo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokupingwa mahakamani.
Maombi hayo yalipokelewa Julai 4, mwaka huu katika mahakama hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha na kusajiliwa kwa namba 018/2018 dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakili Kambole katika maombi yake, kupitia Ibara ya 41 (7), ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anadai kwamba inakiuka mkataba wa Afrika na haki za binadamu na watu.
Kwa mujibu wa Katiba, ibara hiyo inaelekeza kwamba, “iwapo mgombea atatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa mujibu wa Ibara hii basi hakuna mahakama yeyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”
Maombi ya Wakili Kambole ambaye kwenye shauri hilo anatambuliwa kama mleta maombi dhidi ya mjibu maombi ambaye ni Jamhuri, yalipokelewa na Msajili wa Mahakama, Dk. Robert Eno.
Baadhi wananchi mjini hapa waliozungumzia hatua ya Wakili Kambole, kupinga ibara hiyo ya Katiba walisema uamuzi alioufanya ni haki yake kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia hatua hiyo, mkazi wa Arusha, Jonathan Mbisse alisema shauri hilo pindi litakapoanza kusikilizwa na mahakama litatoa fursa pana zaidi kwa wadau wa siasa na uchaguzi kuifuatilia.
“Nadhani jambo hili litakwenda kufungua mlango mwingine wa siasa za Tanzania kwani kwa miaka mingi jambo hili limelalamikiwa sana na wadau wengi,” alisema Mbisse.
Hata hivyo, shauri hilo bado halijapangiwa tarehe ya kusikilizwa na jopo la majaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.