26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kaya 200 zaishi chini ya miti baada ya kuchomewa nyumba na TANAPA

tanapaNa WALTER MGULUCHUMA-KATAVI

 ZAIDI ya kaya 200 katika Kijiji cha Ipota, wilayani Mlele, mkoani Katavi,  hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuteketezwa kwa moto na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa madai si makazi rasmi.

Tukio  hilo lilizua  taharuki  kubwa kwa wakazi  wa  kijiji hicho ambao kwa siku mbili sasa familia zote zinalala nje.

Katika familia hizo wapo watoto wadogo, wajawazito na wazee ambao wameamua kuishi chini ya miti huku wakinyeshewa na mvua.

Inadaiwa askari wa  Tanapa na polisi  kutoka Kituo cha Polisi Kibaoni, waliteketeza nyumba za wakazi hao kwa moto juzi.

Kaimu  Mwenyekiti  wa  Kijiji  cha Ipota, Soguta Maduhu, akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo jana, alisema  kaya 210 hazina  makazi na msaada wa haraka unahitajika.

“Kaya 210 hazina makazi ya kuishi baada ya nyumba zao kuchomwa moto na askari wa Tanapa na polisi wamesababisha wananchi hawa kuishi kwa shida mno, licha ya mvua zinazoendelea kunyesha,” alisema Maduhu.

Akisimulia  tukio  hilo, Maduhu   alisema askari hao walifika  kijijini  hapo kwa kushtukiza na kuteketeza kwa siku mbili mfululizo.

“Kaya hizi zimepata mateso makubwa,  licha ya kuchomewa nyumba zao bado askari waliwapiga  wananchi…hawakuwa na huruma  kabisa, waliwapiga  watoto,   wajawazito na wagonjwa,” alisema.

Alisema kumekuwapo na mgogoro wa mipaka ya makazi kati ya  Tanapa na wakazi wa kijiji  hicho, Hifadhi  ya  Taifa  ya Katavi, eneo tengefu  la kijiji na uhifadhi wa misitu kwa muda mrefu sasa. Alisema nyumba hizo zinadaiwa kujengwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi.

“Ukweli  ni kwamba nyumba hizi  zilijengwa mita 800 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Katavi, utaratibu na sheria zilizopo wananchi wanatakiwa kujenga makazi yao umbali wa mita 500 nje ya hifadhi,” alisema Maduhu.

Kutokana na hali hiyo, aliuomba uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Katavi kufika kijijini hapo kupima mipaka ili ukweli ujulikane.

Kwa upande wake, Joseph Kalubwa alisema  mipaka inayotenganisha hifadhi hiyo na kijiji hicho ni ya asili.

Naye mkazi wa kijiji hicho, Samwel   Kisinja, alidai familia yake yenye watu wapatao 32 tangu juzi wamelazimika   kulala chini ya miti usiku kucha, baada ya makazi yao kuteketezwa kwa moto na askari hao.

Mkazi mwingine, Maria Mchelu, alisema  mbali ya kuchomewa na nyumba yake, askari waliteketeza magunia yake matatu ya chakula.

Naye Deus Kuhanda alisema wakazi hao  wameishi eneo hilo zaidi ya miaka 20.

Mbunge wa Mlele, Dk. Pudensiano  Kikwembe, alikiri kupokea taarifa hizo na kuahidi kuwasiliana na uongozi wa mkoa mara moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles