24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Muhimbili yapandikiza vifaa vya usikivu

Dk. Mpoki Ulisubsya
Dk. Mpoki Ulisubsya

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

NDOTO ya muda mrefu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuanza kupandikiza vifaa vya kusaidia usikivu kwa watoto waliozaliwa na matatizo ya ukiziwi, hatimaye imetimia.

Huduma hiyo  ambayo kitaalamu inaitwa ‘cochlea implant’, ilizinduliwa rasmi hospitalini  hapo jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubsya.

Dk. Ulisubsya alisema hatua hiyo inafanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutoa huduma ya pekee katika nchi zilizopo ukanda wa Jangwa la Sahara.

“Kimsingi nina furaha iliyopitiliza kwa sababu wataalamu wa Muhimbili wameendelea kutekeleza kwa vitendo ile azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa nje ya nchi.

“Hatua hii itasaidia kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kutibu wananchi wetu nje ya nchi.

“Kwa mfano kwa mgonjwa mmoja mwenye tatizo la usikivu Serikali ilikuwa ikitumia takribani Sh milioni 100 kufanikisha upasuaji huu, kwa kweli ulikuwa ukitumia gharama kubwa,” alisema.

Dk. Ulisubsya alisema wizara itahakikisha huduma hiyo inakuwa endelevu ili iwasaidie wananchi wengi zaidi ikizingatiwa tatizo hilo limekuwa likiongezeka.

Mkuu wa Idara ya Masikio, Pua na Koo, Dk. Edwin Liyombo, alisema mchakato wa kuanzisha huduma hiyo ulianza takriban miaka mitatu iliyopita.

“Idara hii ilianza mwaka 2003, tulihudumia watoto watatu pekee, kadri miaka inavyosonga mbele ndivyo idadi ya wagonjwa inavyoongezeka hadi mwaka jana watoto 45 wamepelekwa India kupandikizwa kifaa hiki,” alisema.

Alisema kuna watoto 16 wanaosubiri kupandikizwa kifaa hicho ambao walikuwa wameandaliwa kwenda India.

“Hawa hawatakwenda, tutawafanyia hapa. Ili kufikia hatua ya upasuaji, wanahitajika kufanyiwa ‘mapping’ (uchunguzi wa awali). Januari, mwakani tutawawekea rasmi kifaa hicho,” alisema.

Alisema kutokana na uhitaji mkubwa uliopo liliandikwa  andiko kwenda Wizara ya Afya ambalo lilikubaliwa ambapo Muhimbili itatoa huduma hiyo kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Medel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles