CHAMA cha Wananchi CUF kinamtaka Rais, Dk. John Magufuli kutosaini Muswada wa Huduma za Habari kutoa fursa zaidi kwa wadau na kuanzisha mchakato shirikishi kwa maslahi mapana ya taifa.
Chama hicho kimeungana na wadau wote nchini kupinga Muswada huo wa mwaka 2016 uliopitishwa bungeni juzi na ukisubiri ridhaa ya Rais uwe sheria kamili.
Hayo yalibainishwa katika taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Mbarala Maharagande.
“CUF kimeupitia muswada huo na kujiridhisha kuwa haufai kusainiwa kuwa sheria na Rais kwa maslahi mapana ya taifa letu na wananchi wake na kwa ustawi wa demokrasia, utawala wa sheria na kulinda haki za binaadamu.
“Miongoni mwa upungufu mkubwa katika muswada huo ni kwamba taarifa zinathibitisha kuwa sote kwa ujumla kama wadau hatukushirikishwa vya kutosha katika kupitia muswada huo na kutoa maoni yetu kwa mujibu wa sheria na kanuni za bunge (kanuni ya 84),”alisema.
Maharagande alisema katika taarifa yake kuwa kanuni hiyo inataka muswada ukishasomwa kwa mara ya kwanza, Bunge lifanye matangazo kwa umma kuhakikisha umma unaelewa maudhui ya muswada na kuwezesha wananchi kutoa maoni yao.
“Ni aibu na fedheha kwa uongozi wa Bunge ambao ulirejesha fedha serikalini leo kuripotiwa kuwa ulishindwa kuchapisha nakala za kutosha za Muswada wa Habari kwa kamati ya bunge na kushindwa kutoa matangazo ya kutosha kwa wananchi waweze kupitia muswada huo na kutoa maoni yao,”alisema.
Alisema sheria imetoa mamlaka makubwa yaliyojificha na yaliyowazi kwa waziri mwenye dhamana na tasnia ya habari kufanya uamuzi juu ya vyombo vya habari kwa kadri ya utashi wake atakavyojisikia na kwa tafsiri yake juu ya habari ambayo ataona haimpendezi yeye binafsi na Serikali yake.
Chama hicho kinasema wananchi wanahitaji kuwa na demokrasia pana iliyo na uhuru wa vyombo vya habari visivyoingiliwa na mamlaka yoyote na kuiachia mahakama pekee ndiyo iwe muamuzi wa tafsiri za sheria za masuala yote yanayoonekana kukiukwa na wahusika.
“Ni dhahiri kwamba kuna vifungu kadhaa kikiwamo kifungu cha 7(1)(b)(iv), kifungu cha 60(2)(a) waziri amepewa mamlaka makubwa na kumfanya kuwa kama Mhariri Mkuu wa Taifa, inampa mamlaka hayo waziri kiasi ambacho ataweza kuendesha vyombo vya habari atakavyo yeye.
“Muswada umetafsiri uchochezi kuwa ni pamoja na kuandika au kutangaza mambo ambayo yanaweza kutafsiriwa kuwa yanaleta chuki ya wananchi dhidi ya Serikali.