22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Katiba yapenya tundu la sindano

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakicheza ndani ya ukumbi wa bunge Dodoma
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakicheza ndani ya ukumbi wa bunge Dodoma

NA MAREGESI PAUL, DODOMA

RASIMU ya Katiba inayopendekezwa inaonekana kuigawa nchi, baada ya wajumbe wa Bunge Maalumu kuipitisha mjini Dodoma jana.

Baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura ambazo zilionyesha kupatikana kwa theluthi mbili upande wa Tanzania Bara na Zanzibar, wananchi wa kada tofauti, viongozi wa kisiasa, dini, wasomi na taasisi mbalimbali wameonyesha wazi kutofautiana.

Miongoni mwa makundi hayo, yameonyesha wasiwasi yakitilia shaka namna ilivyopatikana theluthi mbili ya kura za wajumbe wa Bunge hilo kutoka Zanzibar.

Wasiwasi huo uliibuka baada ya Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk. Thomas Kashililah, kutangaza matokeo ya kura hizo jana asubuhi na kuonyesha theluthi mbili iliyokuwa ikitakiwa kwa wajumbe wa Zanzibar na Tanzania Bara ili rasimu hiyo ikubaliwe, zimepatikana.

Dk. Kashililah, alisema theluthi mbili iliyotakiwa kwa upande wa Zanzibar ni kura 146 kutokana na wajumbe 219 waliotakiwa kupiga kura.

Alisema kati ya wajumbe hao 219, waliopiga kura ni 154 wakati 65 hawakupiga kura.

Kutokana na hali hiyo, alisema Zanzibar walifikisha theluthi mbili baada ya kupatikana kura 148.

Alisema katika kura hizo, za wazi za ndiyo katika kila ibara zilikuwa ni kati ya 106 na 108 na za wazi za hapana zilikuwa kati ya sita na nane.

Kwa upande wa kura za siri za ndiyo, alisema zilikuwa ni kati ya 38 na 40 wakati kura za siri zilizoikataa rasimu hiyo zilikuwa ni kati ya moja na mbili.

KURA ZA BARA

Dk. Kashililah alisema kwa upande wa Tanzania Bara, wajumbe waliotakiwa kupiga kura ni 411 na kwamba ili theluthi mbili ipatikane, zilikuwa zikitakiwa kura 274.

Baada ya kura kupigwa, alisema ilionyesha kura za ndiyo katika kila ibara zilikuwa ni kati ya 301 na 303 wakati kura za wazi za hapana zilikuwa ni kati ya kura moja na moja.

Kwa upande wa kura za siri za ndiyo, alisema zilikuwa ni kati ya 29 na 31 na kura za siri zilizoikataa rasimu hiyo zilikuwa ni kati ya kura moja na mbili.

Kutokana na matokeo hayo, alisema kura zote za ndiyo zilikuwa ni kati ya 332 na 334.

SHANGWE

Baada ya kutangazwa matokeo hayo, wajumbe walilipuka kwa shangwe na kuanza kuimba nyimbo za kupongezana na kucheza huku wakikumbatiana kwa furaha.

Baadhi ya wajumbe walihama katika viti vyao na kuwafuata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na viongozi wengine wa kisiasa na Serikali na kupongezana.

Hali hiyo, ilitokana na hofu iliyokuwapo awali kwa wajumbe hao juu ya kupatikana theluthi mbili ya kura kwa upande wa Zanzibar.

Baada ya shamrashamra hizo kudumu kwa zaidi ya dakika kumi, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alianza kuwatuliza wajumbe akitaka watulie ili shughuli nyingine ziendelee kazi ambayo haikuwa rahisi.

Baada ya Sitta kufanikiwa kuwatuliza wajumbe hao, Dk. Kashililah alianza kutangaza matokeo ya wajumbe wa Tanzania Bara ambayo pia yalionyesha theluthi mbili imepatikana.

Kutokana na hali hiyo, shangwe zilianza upya ambapo nyimbo, kelele, vigelegele vilitawala pamoja na maneno ya kashfa kwa waliokuwa wakipiga vita Bunge hilo.

SITTA AZUNGUMZA

Akizungumzia matokeo hayo, Sitta alisema kuna baadhi ya watu waliingilia matokeo ya kura zilizopigwa kwa mtandao ingawa hawakufanikiwa kuziharibu.

“Kuna watu walighushi kwenye mitandao na kusema Waziri Mkuu amenipa Sh milioni 500 niwashawishi baadhi ya wajumbe waipigie kura za ndiyo hii rasimu. Hawa watu ni wahuni na wapuuzwe.

“Wengine walidiriki kuingilia mawasiliano kati yetu na ubalozi wetu wa Saudi Arabia. Hawa walifanikiwa ila kura zote zilikuwa vizuri,” alisema Sitta.

KURA ZILIVYOHESABIWA

Wakizungumzia jinsi kura zilivyohesabiwa, mawakala wawili wa kuhesabu kura, Amina Makilagi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na Waziri Rajabu, walisema kwa nyakati tofauti kuwa kura zilihesabiwa kwa uwazi na hakukuwa na udanganyifu uliofanyika.

Kwa mujibu wa mawakala hao, Watanzania hawana sababu ya kuhofia matokeo hayo kwa kuwa kila hatua katika uhesabuji wa kura, ilifanyika kwa ukweli na uwazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles