31.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

KASI UHARIBIFU MRADI WA HIFADHI YA MITI YATISHA

Na Derick Milton, Meatu


SHERIA ya Misitu namba 14 ya mwaka 2014 inazitaka mamlaka za serikali kuu, halmashauri, pamoja na serikali za vijiji kuhakikisha zinalinda, zinahifadhi na kutunza maeneo yote yaliyotengwa kuwa hifadhi ya misitu.

Sura namba 5 na 6 za sheria hiyo zinatamka wajibu wa Mkurugenzi wa Misitu Tanzania, maafisa misitu halmashauri na kata kuhakikisha wanasimamia masuala yote ya misitu na watekelezaji wakuu wa sheria hiyo.

Hata hivyo, sheria hiyo imetoa fursa kwa mamlaka za usimamizi misitu ngazi zote, kumfikisha mahakamani mtu yeyote atakayebainika kuaribu, kuingia ndani ya hifadhi bila ya kibali maalum na adhabu yake ni kifungo cha miaka 2 jela au faini Sh milioni moja au vyote kwa pamoja.

Mamlaka za serikali za vijiji zimetajwa katika sheria hii, zikiwa wasimamizi wakuu wa hifadhi za misitu katika kijiji ikiwa pamoja na kutunga sheria ndogondogo za kulinda, kutunza, misitu kwa kijiji husika.

Licha ya kutungwa kwa sheria hiyo, mwaka 1998 serikali iliweka sera ya misitu ambayo lengo kubwa ilikuwa kuhakikisha hifadhi zote za misitu zinaendelezwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

“Jamii itahimizwa, kuwezeshwa kushiriki katika kupanga, kusimamia, kutumia na kuhifadhi misitu iliyoko katika eneo lake kwa maendeleo ya hali za kibinafsi na jamii na taifa kwa ujumla,” inasema Sera.

Uwapo wa sheria hiyo na sera bado havijaleta mafanikio yoyote yaliyokuwa yametegemewa, badala yake uharibifu wa mazingira umeendelea kufanyika kwa kasi katika maeneo mbalimbali hapa nchini hasa miti kukatwa ovyo.

Maeneo mengi ambapo uharibifu umefanyika, wananchi wanarushiwa mpira kuhusika zaidi kutokana na shughuli mbalimbali za kilimo, makazi na uchomaji mkaa wanazoziendesha.

Moja ya uharibifu huo ni mradi wa hifadhi ya ardhi Shinyanga (HASHI), mradi wa upandaji miti, ulianzishwa katika maeneo yaliyokumbwa na ukame na kutishia kuwa jangwa.

Mradi huo ulitekelezwa kuanzia mwaka 1980 hadi 2000 na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirikika la Maendeleo la Norway (NORAD), ukigharimu zaidi ya Sh bilioni moja.

Wilaya ya Meatu ilikuwa miongoni mwa maeneo ambayo mradi ulitekelezwa, maeneo mengine ni wilaya za Maswa, Bariadi, Kahama, Shinyanga Vijijini, Shinyanga Mjini, pamoja na Wilaya ya Bukombe.

Pamoja na kutumia kiasi kikubwa cha fedha (zaidi ya bilioni moja) mradi umeharibiwa. Wananchi wamevamia maeneo yaliyopandwa miti na kuendesha shughuli za kilimo, uchomaji mkaa na makazi.

Kata ya Mwandoya iliyoko katika wilaya hiyo ni moja ya maeneo mradi ulitekelezwa, ambapo jumla ya hekari za miti 1000 zilipandwa ambazo zilikuwa zikimilikiwa na serikali za vijiji, watu binafsi pamoja na taasisi za serikali zikiwamo shule.

Ofisa Misitu wa kata hiyo, Samweli Malya anasema kata hiyo yenye vijiji sita ambavyo ni Mwandoya, Mwagumaga, Igobe, Mwakaluba, Inonelwa na Makomangwa, vilipanda hekari 90 huku hekari 10 zikiwa mali ya watu binasfi na shule.

“Asilimia 90 ya hekari zote za miti iliyopandwa wakati mradi imekatwa, ni hekari 10 tu ambazo zimebaki kwenye kata hii, ambazo mbili zipo kwenye shule ya msingi Igobe na moja kwenye shule ya sekondari Mwandoya, saba zinamilikiwa na watu binafsi,” anasema Malya.

Kijiji cha Igobe kilichopo katika kata hiyo kilikuwa kinamiliki hekari 100 za hifadhi za miti, ambazo zilikuwa zimepandwa katika Shule ya Msingi Igobe, kando kando ya Mto Igobe na katika shamba la kijiji.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Tambilija Kuzenza anasema serikali ya kijiji ilikuwa inamiliki hekari 50 za hifadhi ya miti zilizopandwa kwenye shamba la kijiji ambalo lilikuwa mali ya serikali ya kijiji.

Anasema hifadhi hiyo imeharibiwa yote baada ya wananchi kuvamia na kukata mito yote na kuanza kuendesha shughuli za kilimo, makazi pamoja na uchomaji mkaa.

“2015 kwenye mkutano wa kijiji wananchi waliamua kukata miti yote iliyokuwamo kwenye hifadhi, ni baada ya kutokea mmoja wa wananchi Mahona Doya kudai eneo hilo ni mali yake aliloachiwa na wazazi wake waliokuwa wamelitoa kwa ajili ya kutumika kama shamba darasa wakati wa mradi,” anasema Kuzenza.

Anasema Doya alitaka kurejeshewa eneo hilo ili kufanya shughuli nyingine na wananchi walikubali na kuamua miti yote iliyokuwamo ikatwe na Doya apatiwe eneo lake.

“Niliwakatalia lakini haikuwezekana baada ya kusema kuwa wao ndiyo wenye uamuzi wa mwisho kwenye mali ya kijiji, kesho yake baada ya mkutano hifadhi ilikatwa miti yote,” anasema.

Kamanda wa Jeshi la Jadi (Sungusungu) Lembo Matana ambao walikuwa wamepewa jukumu na kijiji kulinda hifadhi hiyo, anasema walikabidhiwa hifadhi hiyo na serikali ya kijiji mwaka 2003 kwa ajili ya kuilinda.

“Toka mwaka 2003 hatujawahi kumuona au kusikia mwananchi yeyote kutoka kwenye kijiji chetu akisema eneo hilo ni mali yake au wazazi wake, hii ilijitokeza ghafla,” anasema Matana.

Anasema walifanikiwa kulinda hifadhi hiyo kwa kiwango kikubwa, ambapo baadhi ya wananchi wakiwamo wafugaji walipewa adhabu au kuchukuliwa mifugo yao walipokutwa kwenye hifadhi bila ya kibali.

“Waliotupatia dhamana ya kulinda na hifadhi baada ya kufanya uamuzi mengine ya kugawa eneo hilo sisi hatukuwa na nguvu tena, walifanya uamuzi ya kulitwaa wakakata miti na kugawa eneo,” anasema Matana

Mtendaji wa kijiji hicho, Japhet Mwandu anasema baada ya uharibifu huo walitoa taarifa Idara ya Misitu ya Halmashauri, ambapo baadhi ya wahusika walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

“Kesi ilipelekwa Mahakama ya Wilaya Meatu, nasi viongozi akiwamo mwenyekiti wa kijiji na wajumbe wake, tuliitwa mahakamani kutoa ushahidi, lakini mpaka leo hatujui kinachoendelea kwenye kesi hiyo,” anasema Mwandu.

Hata hivyo, si kata ya Mwandoya pekee katika wilaya hiyo ambayo imeadhirika kwa kiwango hicho, bali robo tatu ya eneo zima la wilaya lililopandwa miti wakati wa mradi limevamiwa na kukatwa miti.

Idara ya misitu katika halmashauri ya wilaya hiyo inaeleza kuwa uharibifu huo umesababisha kubaki hekari za hifadhi za miti 5821 kati ya 14,155 zilizopandwa wakati wa mradi sawa na asilimia 30 ya miti yote iliyopandwa.

Timotheo Maduhu ambaye ni Kaimu Ofisa Misitu wa halmashauri anasema maeneo yote ambayo hifadhi zote zimeharibiwa, njia zilizotumiwa na wananchi kuvamia na kukata miti zinafanana.

Uharibu wa mradi huo umeanza kuleta madhara makubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo, ikiwamo ukame mkubwa ambao umekuwa ukiikumba wilaya kila mwaka.

Ukame huo umesababisha mito mikubwa Igobe, Mhanuzi, Mwandoya, Mwamishali, Bukundi na Nkoma kukauka na kusababisha wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.

Katika kijiji cha Igobe chenye wakazi wapatao 3758 chanzo kikuu cha maji ni mto Igobe ambao umekauka kutokana na kukamtwa kwa miti iliyokuwa imepandwa kando kando ya mto wakati wa mradi huo.

Getu Kaesi, mkazi wa kijiji hicho anasema wanatumia muda wa saa mbili kutembea kufuata maji katika mto huo ambao kwa sasa umekauka.

“Wanawake tunahangaika na maji, mimi hapa Igombe natembea kilometa tatu, wananchi wa kitongoji cha Bomani ambao kwao hakuna chanzo cha chochote cha maji wakitegemea mto huu wanatembea kilometa 10,” anasema Kaesi

Kwa upande wake Dende Buhondo, mkazi kitongoji cha Mwagigili, anasema wanalazimika kutembea umbali wa kilometa saba kutafuta maji wakitumia muda wa saa sita hadi nane kutafuta huduma hiyo.

Wananchi wa kijiji hicho wanasema mto huo ambao ni chanzo kikuu cha maji, hautiririshi maji tena kama ilivyokuwa zamani kutokana na miti iliyopandwa kando kando kukatwa.

Wanasema kuwa hali hiyo inawalazimu kuangaika kupata huduma hiyo kwa kuchimba madimbwi kila sehemu katikati ya  mto huo kutafuta maji na wakati mwingine wanakosa.

Kwa mijibu wa idara ya maji katika halmashauri hiyo yenye watu 299,619; asilimia 43.6 ya wananchi wa vijijini na asilimia 38 ya wananchi wa mjini, ndiyo wanaopata maji safi na salama kupitia miradi iliyotekelezwa na idara hiyo.

Kaimu Mhandisi wa Maji Romanes Thomas anasema idadi kubwa ya wananchi wa vijijini na mjini, wanatumia maji ya madimbwi ambayo wamekuwa wakichimba katikati ya mito mikubwa isiyotiririsha maji.

Maji yanayochimbwa kwenye mito hiyo si safi na salama, ambapo wananchi wengi wamekuwa wakipata matatizo ya magonjwa ya tumbo kutokana na kutumia bila ya kuweka dawa au kuchemsha.

Idara ya Afya kwenye halmashauri hiyo kila mwaka bajeti yake imeendelea kuwa kubwa, kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa wa matumbo yanayotokana na kutumia maji hayo.

Mganga mkuu wa wilaya hiyo Asey John anasema magonjwa ya matumbo yanayotokana na utumiaji wa maji si safi na salama.

“Magonjwa haya ni ya pili baada ya ugonjwa wa maralia, kati ya magonjwa 10 yanayowakumba wananchi wilaya hii, lakini pia yanashika nafasi ya pili kwa vifo baada ya maralia,” anasema Asey.

Anasema katika bajeti ya 2016-17 magonjwa hayo yametengewa asilimia 13.58 ya bajeti nzima ya idara ya afya ya Sh bilioni 1.8 kiwango ambacho kila mwaka kimekuwa kikiongezeka.

Asey anaeleza kwa mwaka 2016 jumla ya wagonjwa 745 walikutwa na magonjwa ya tumbo, wanawake wakiwa 397 na wanaume 348 huku vifo vikiwa 14 wanawake wakiwa tisa na wanaume watano.

Asey anasema kwa mwaka huo huo, watoto chini ya miaka mitano wapatao 568 walilazwa hospitali na vituo vya afya kutokana na kusumbuliwa na magonjwa hayo huku 7 wakipoteza maisha.

Anaongeza kuwa idara afya haina mkakati wowote wa kutibu maji hayo, badala yake wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhakikisha wanachemsha maji hayo kabla ya kunywa.

Aidha, uharibifu wa mradi huo unaelezwa kusababisha uwapo wa mgogoro wa muda mrefu kati ya wafugaji na pori la akiba la Maswa lililoko katika Wilaya hiyo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 2,200.

Mgogoro huo unatokana na wafugaji wa wilaya hiyo kuchunga mifugo yao ndani ya hifadhi bila ya kibali, kutokana na maeneo yao kukosa malisho baada ya kuaribu hifadhi hizo zilizotumika kuchungia mifugo.

Hifadhi hizo licha ya kulinda vyanzo vya maji, zilisaidia kupatikana nyasi, ambapo wafugaji walitumia kuchungia mifugo yao na kupata chakula cha kutosha.

Kinda Yohana mfugaji kutoka kijiji cha Igobe mwenye ng’ombe 400 anasema; “tunalazimika kutembea umbali wa kilometa zaidi ya 100 kwenda katika pori tengefu la Maswa kufuata malisho.”

Anaongeza; “Hatuna sehemu yoyote nyingine ya kupeleka mifugo yetu, Hifadhi ya Igombe ndiyo ilikuwa mkombozi wa mifugo yetu kwenye kijiji cha Igobe sisi wafugaji, baada ya kuvamiwa na kukatwa miti yake yote wafugaji tunaangaika sana,” anasema Yohana.

Awali Yohana alikuwa na ng’ombe 600 pamoja na mbuzi 120, ambapo wamebaki 400 na mbuzi 50 baada ya wengine kukamatwa wakiwa ndani ya pori la Maswa.

“Kila mara mifugo inakamatwa kwenye pori, hatuna jinsi ni lazima tukapeleke uko, ukikamatwa unauza ngombe 10 ili ulipe faini unakomboa mifugo yako. Sasa hivi tunahangaika na sehemu za malisho,” anaeleza Yohana.

Meneja wa Pori hilo Lusato Masinde kila mwezi wanakamata ng’ombe kati ya 3000 na 5000, ambapo wahusika wamekuwa wakitozwa faini kwa kuingiza mifugo bila ya kibali na wakati mwingine mifugo kutaifishwa.

“Wafugaji wana mifugo mingi hasa Meatu. Hawana maeneo ya malisho, hivyo wanaamua kuleta huku kwenye hifadhi:, kila siku tunawakamata lakini hawaachi” anasema Masinde.

Licha ya madhara hayo kutokea kutokana na kuharibiwa kwa mradi huo, uchunguzi unaonyesha kuna hatari kubwa ya hifadhi zaidi ya 5000 zilizobaki kuaribiwa ndani ya mwaka mmoja kutoka na kasi ya kuvamiwa kuwa kubwa.

MWISHO.

 

Pix 1:  Geti Kaesi Mkazi wa Kijiji cha Igobe kata ya Mwandoya wilaya ya Meatu akichota maji kwenye mto Igobe ambao hautiririshi maji kutokana na kukauka hali inayowalazimu kuchimba mashimo kufuata maji chini.(Picha na Derick Milton).

Pix 3,4: Wananchi wa Kijiji cha Mhanuzi Wilayani Meatu wakichota maji katika mashimo yaliyochimbwa kati kati ya mto mkubwa wa Mhanuzi ambao umekauka, maji hayo siyo safi na salama, (Picha na Derick Milton)

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles