WASHINGTON, MAREKANI
MWENDELEZO wa kashfa zinazomkabili Rais, Donald Trump, ikiwamo anayodaiwa yeye binafsi alimtaka Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Upelelezi Marekani (FBI), James Comey kuachana na uchunguzi dhidi ya mshauri wake wa usalama wa taifa Michael Flynn unatishia urais wake.
Seneta Angus King, ambaye ni mwanasiasa huru japokuwa ameegemea Chama cha upinzani cha Democratic, iwapo taarifa hiyo mpya ni ya kweli uwezekano mkubwa unakuja kwa Trump kung’olewa.
Ikulu ya Marekani, White House ilikana vikali baada ya dondoo hizo kuanikwa na kusababisha heka heka za kupambana na ripoti zilizoonekana kuwa na madhara kwa utawala huu mpya.
Taarifa hizo kutoka kwa James Comey, zilifichuliwa na mtoa habari mmoja aliyeona kitabu cha kumbukumbu cha bosi huyo wa zamani wa FBI.
Taarifa hizo mpya zinakuja wakati utawala wa Trump unaojiingiza matatizoni kila mara ukiwa bado unahangaika kujisafisha kuhusu taarifa kuwa Trump alitoa siri nyeti kwa waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi na balozi wa nchi hiyo nchini Marekani.
Wakitetea hatua za Trump, maafisa walipuuzia umuhimu na usiri wa taarifa hizo, ambazo ziliwasilishwa na Israel chini ya makubaliano ya kubadilisha taarifa za kijasusi.
Na Trump binafsi amesema ana haki zote kama rais kubadilishana taarifa hizo zinazohusu ugaidi na usalama wa safari za anga na Urusi.
Pamoja na hayo washirika wa Marekani na baadhi ya wabunge wameeleza wasi wasi wao unaokaribia kuwa tahadhari.
Seneta kutoka Republican, John McCain ametoa matamshi makali jana kuwahi kutolewa na kambi ya chama hicho anachotoka Trump.
McCain amesema hali hii sasa imekaribia kiwango cha kashfa kubwa ya Watergate.
“Kitu ninachoweza kusema ni kuwa tuliisha ona filamu hii hapo kabla. Nafikiri inafikia katika kiwango ambapo ni sawa na Watergate na viwango vya kashfa nyingine ambazo mimi na wewe tumekwisha shuhudia. “
Comey, ambaye Trump alimfuta kazi wiki iliyopita, aliandika katika kumbukumbu baada ya mkutano wa Februari Ikulu mjini hapa kwamba rais mpya alimuomba kufunga uchunguzi dhidi ya Flynn kuhusu mawasiliano yake na Urusi.
Uchunguzi kuhusu Flynn ulikuwa sehemu ya ule mpana zaidi kuhusiana na Urusi kuingia uchaguzi wa rais mwaka jana.