Na Walter Mguluchuma-Tanganyika.
WAKAZI wa Tarafa ya Karema mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Tanganyika mkoani Katavi, wanaopakana na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wameondokana na tatizo la ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa lililokuwepo kwenye kituo chao cha afya cha Karema, baada ya Serikali kuwapatia gari jipya.
Kabla ya kukabidhiwa gari hilo jana, wagonjwa wa kituo hicho walilazimika kuagiza gari la wagonjwa kutoka makao makuu yao ya Wilaya ya Tanganyika umbali wa kilometa 110.
Gari hilo lilikabidhiwa na Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso kwa uongozi wa halmashauri hiyo kutokana na maombi aliyotoa mwaka jana kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalim.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Dk. Seleman Mtenjela alisema Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga vituo viwili vipya na kukifanyia ukarabati kituo cha afya Karema, ujio wa gari hilo utasaidia utoaji huduma uhakika kwa wagonjwa.
Alisema jukumu la Serikali, ni kuhakikisha watu wake wanakuwa na afya njema hivyo tatizo la kituo hicho kuangiza gari kwenye makao makuu ya Halmashauri pindi anapokuwa ametokea mgonjwa anae takiwa kusafirishwa kwenda hospitali ya wilaya au ya mkoa sasa halitakuwepo tena .
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Salehe Mhando alisema gari hilo halikupatikana hivi hivi, ni kutokana na jitihada za Kakoso kuomba Serikalini .
Diwani wa Kata ya Karema, Michael Kapata alisema ndoto za wakazi wa rarafa hiyo sasa zimetimia.