24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Majaliwa atoa takwimu mpya wagonjwa wa corona kupungua

 RAMADHAN HASSAN– DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema idadi ya wagonjwa wa ugonjwa wa corona,imepungua nchini na kuwataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo.

Amesema Jiji la Dar es Salaam katika Hospitali ya Amana kulikuwa kuna wagonjwa 12,lakini kwa taarifa ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Dk. Rashid Mfaume amebaki mgonjwa mmoja, Mloganzila walikuwa 6 kwa sasa amebaki mmoja, huku Temeke kukiwa hakuna mgonjwa hata mmoja.

Alisema kwa Mkoa wa Dodoma kulikuwa na wagonjwa 12, sasa wamebaki watatu, huku Pwani kukiwa na wagonjwa watatu kati ya 22,kwa upande wa Hospitali binafsi Aga Khan ilikuwa na wagonjwa 11, sasa wamebaki wanne na katika Hospitali ya Palestina kulikuwa kuna wagonjwa 14,sasa hakuna hata mmoja.

Akizungumza jana mbele ya waumini wa dini ya Kiislamu, wakati wa ibada ya swala ya Eid El- Fitri iliyofanyika Msikiti wa Gadaffi jijini hapa,Majaliwa alisema kwa sasa wagonjwa wa ugonjwa umepungua nchini.

Ibada hiyo iliongozwa na Sheikhe wa Mkoa wa Dodoma,Mustapha Rajabu,ambapo Majaliwa alisema jana asubuhi alizungumza na Dk. Mfaume na kumweleza wagonjwa wamepungua.

“Tunaposema ugonjwa umepungua ni kweli, taarifa za leo (jana) saa 1.30 asubuhi kwa wagonjwa wetu waliothibitishwa Mkoa wa Dar es salaam ambao ulikuwa na maambukizi mengi tukadhani tuchue Hospitali yote ya Amana na tulikuwa tumeandaa eneo la Sabasaba huko wakijaa tuwapeleke huko.

“Pale Temeke tukaomba wodi moja ya vitanda 10 kwa ajili ya kulaza wagonjwa, tukaacha Muhimbili na Mloganzila kubwa kwa sababu ya wagonjwa wengine.

“Tarehe 17,rais alituambia wamebaki wagonjwa 12, ninafurahi kuwaambia nimezungumza na Daktari wa Mkoa wa Dar es salaam asubuhi ya leo (jana) amebaki mgonjwa mmoja.

“Mloganzila pale tumejenga kambi yenye vitanda 30 na taarifa ya rais kulikuwa kuna wagonjwa 6 kwa taarifa ya Mganga Mkuu wa Dar es Salaam amebaki mgonjwa mmoja.

“Hospitali ya Temeke rais alisema hakuna mgonjwa na leo napenda niwaambie hakuna mgonjwa na mnajua Temeke,Mbagala Gongolamboto Tandala jinsi kulivyo na watu wengi, tunashuku ‘allah’ kwa kutokuwa na mgonjwa,”alisema.

Alisema wagonjwa wachache bado wapo katika Hospitali za binafsi ambapo alidai Aga Khan taarifa ya Rais ilisema kuna wagonjwa 11 lakini kwa sasa ambao wapo katika uangalizi ni wanne pekee huku,Hospitali ya Palestina kukiwa hakuna mgonjwa ambapo awali kulikuwa kuna wagonjwa 14.

“Lakini tuna hospitali za binafsi ambazo zimeunga mkono jitihada za Serikali kwa kutenga maeneo ya wagonjwa kama vile Hospitali ya Kairuki ilikuwa na wagonjwa wanne leo hakuna mgonjwa aliyethibitishwa.

“Palestina, rais alisema kuna wagonjwa 14 kwa sasa hakuna mgonjwa hata mmoja.Regence hakuna mgonjwa na Temeke pia.

“Wagonjwa bado tunao katika Hospitali ya Aga Khan tarehe 17 mheshimiwa Rais alituambia wapo 11 lakini wanne ndio wanaangaliwa kwa karibu,”alisema.

Alisema Mkoani Pwani katika Hospitali ya Kibaha kulikuwa kuna wagonjwa 22 lakini kwa sasa waliobaki ni watatu pekee huku kwa Mkoa wa Dodoma kukiwa na wagonjwa watatu kati ya wagonjwa 12 waliokuwa katika kituo cha Mkonze.

“Kule Kibaha walikuwa 22 leo kati ya hawo watatu ndio wanaangaliwa kwa karibu.Hapa kwetu Dodoma Mkonze 12 jana (juzi) tulikuwa na wagonjwa watatu hata asubuhi hii tumeamka na wagonjwa watatu hawa wote wanaangaliwa naamini Mwenyezingumu taendelea kutusaidia,”alisema.

HATA KAMA UNAMAAMBUKIZI FANYA KAZI

Aliwasisitiza Watanzania kuendelea kufanya kazi, huku akidai hata ambao wamekutwa na maambukizi ya ugonjwa wa corona waendele kufanya kazi huku wakiwalinda wengine.

“Nasisitiza usiache kufanya kazi zako hata kama unamambukizi ili tuweze kuukuza uchumi kwani unaweza kufanya kazi huku unaumwa Malaria na unakunywa dawa hivyo tufanye hivyo na kwenye ugonjwa huu.

WANAFUNZI KUFUATA MASHARTI

Aliwataka wanafunzi wa kidato cha sita na wale wa vyuo kufuata masharti pindi ambapo watafungua shule na vyuo.

“Kwa upande wa shule za sekondari na vyuo na wao kila mmoja ajitahidi kufuata masharti ili wafanye mitihani yao tusikatize mlolongo wa taaluma yao.

HATMA YA WANAFUNZI WENGINE

Alisema Rais Dk.John Magufuli ikimpendeza kwa mujibu wa wataalamu atatoa kibali cha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

“Wanafunzi wa sekondari kutoka chini hadi kidato cha sita tathimini inaendelea,mheshimiwa rais ikimpendeza kwa mujibu wa taarifa za wataalamu maeneo mengine tutayafungua tunatambua kuna wanafunzi wa kidato cha nne kidato cha pili na wao wanatakiwa kufanya mitihani mheshimiwa rais ikimpendeza atatoa kibali.

“Lakini ili imependeze zaidi ni lazima kila mmoja azingatie haya maelekezo ya wataalamu,”alisema.

ATAKA HOFU IONDOLEWE

Aliendelea kuwasihi Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari za kukabiliana na ugonjwa huo kwa kuhakikisha wanafuata maelekezo ya wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kuondoa hofu.

“Ugonjwa huu upo tuchukue tahadhari tusiwe na hofu huu ni ugonjwa kama ugonjwa mwingine tumekuwa na ugonjwa kama surua, malaria, muhimu zaidi, lazima tujue chanzo chake ni nini la lazima tujikinge.

“Umepita ugonjwa huu mahala pote kumbe kwa kuanza huko kumepelekea sisi watanzania kujifunza na kuuelewa.Mheshimiwa rais alijitokeza na kusema ugonjwa umeingia tusiwe na hofu.

“Rais wetu ameendelea kusema ugonjwa huu ni kama ugonjwa mwingine, ndugu Watanzania sidhani kama kuna mtu hajawahi kuugua ugonjwa wa mafua, hajapata kukohoa, kusikia maumivu ya mwili hajawahi kupiga chafya.

“Nataka niwaambie ugonjwa huu ni kama mafua,mafua yake ni makali kidogo na dalili zake ndio hizo ukiona hivyo wahi Hospitali.

HOFU IMEPUNGUA

Aidha,Waziri Mkuu alioneshwa kufurahishwa na jinsi ambavyo hofu ya ugonjwa huo ilivyopungua kwa Watanzania.

“Ndugu zangu leo (jana) ninaposimama hapa mbele yenu nafurahi kuwaambia ile hofu kubwa imeishapungua, hapa ni uelewa wa kawaida kwamba ugonjwa upo muhimu ni kila mmoja kufuata masharti

“Tunaposema haya Watanzania tuendelee kujikinga tuendelee kuwa na tahadhari ili kupunguza uwezekano wa kuwaambukiza wengine suala la kunawa mikono ni la lazima.Kama kila mmoja atazingatia basi naamini ugonjwa huu utapungua kwa kaisi kikubwa nasisitiza endelea kufanya kazi zako,”alisema.

APONGEZA MAOMBI

Katika hatua nyingine,Majaliwa aliwapongeza waumini wa dini ya Kiislamu na madhehebu mengine kwa jinsi ambayo waliombea taifa katika kipindi hichi cha ugonjwa wa Corona.

“Sisi Waislamu tumeomba sana pamoja na madhehebu mengine, leo tunamalizia dua jambo hili mheshimiwa rais anasema hata lisahau na tuzidi kumuomba Mwenyezingu atupunguzie janga hili.

“Lakini pia Rais anaendelea kuwaomba kuendelea kuomba wakati wote ili Mwenyezimungu aendelee kutupunguzia balaa hili.Leo ni siku ya Iddi mara baada ya kufunga mwezi mzima lakini pia Makamu wa Rais nae anatushukuru na anawashukuru kwa kumuomba Mungu atuondolee tatizo hili,kwani na yeye alikuwa pamoja na sisi katika kufunga,”alisema.

 UCHAGUZI WA BURUNDI

Alisema uchaguzi wa Burundi umefanyika kwa amani kutokana na kuiga jinsi ambavyo Tanzania imekuwa ikihubiri amani.

“Uzuri dini zetu zinatujenga katika upendo.Nchi hii dini imetufikisha hapa tulipo kutokana na amani tuliyonayo kwani mataifa mengine yamekosa amani lakini Tanzania imekuwa ni Nchi ya mfano leo tunashuhudia Burundi wanafanya uchaguzi kwa amani kabisa hata wanaposubiri matokeo bado wapo katika utulivu sababu ni sisi kuwa majirani wao.

“Tuendelee na tabia hii na viongozi wa dini muendelee kuhubiri kuhusu amani,Ujumbe wa Serikali baada ya swala hii watu waendelee kufurahia huku mkiendelea na shughuli zenu kwa amani Serikali itaendelea kuhakikisha mipaka yake inakuwa katika amani nataka niwahakikishie viongozi wa dini kwamba taifa letu bado lipo salama.

“Kama unalima lima sana kama unapiga kazi kiwandani nenda kapige na sisi tuliopewa dhanama tuendeleaa kuwa waadilifu nataka niwahakikishie serikali yenu ipo imara,”alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles