VATICAN, ITALIA
KARDINALI Giovanni Angelo Becciu ambaye alikuwa mshauri wa karibu wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amelazimishwa kujiuzulu kutokana na ubadhirifu wa fedha ambazo anadaiwa kuzigawa kwa ndugu zake.
Kardinali huyo wa ngazi ya juu Vatican, Giovanni Angelo Becciu amejiuzuru ghafla bila kutarajiwa lakini imebainika kuwa aliambiwa na Papa Francis kufanya hivyo.
Kardinali huyo alishukiwa kutoa fedha ya kanisa na kuwapa ndugu zake ingawa amekanusha kufanya kosa hilo.
Kardinal Becciu alikuwa mshauri wa karibu wa papa na awali katibu wa Vatican.
Alihusika na mkataba ambao una utata wa kuwekeza katika kujenga jengo la kifahari mjini London kwa kutumia fedha za kanisa.
Uwekezaji huo ulikuepo tangu waanze kumfanyia uchunguzi wa matumizi ya fedha.
Inaelezwa kuwa kujiuzuru katika ngazi ya ukadinali ni jambo la nadra sana kutokea, taarifa kutoka ofisi ya baba mtakatifu zinasema.
“Baba mtakatifu amekubali maombi ya kujiuzulu yaliyowasilishwa na mwadhama kadinali Giovanni Angelo Becciu.”
Kardinali huyo mwenye umri wa miaka 72, aliuambia mtandao wa Domani nchini Italia kuwa alilazimishwa kujiuzulu kwa sababu alishukiwa kutoa fedha za kanisa kwa kaka zake.
Kadinali anasisitiza kuwa hakuiba hata euro moja
“Sijaiba hata euro moja. Sijafanyiwa uchunguzi lakini wakinipeleka mahakamani , nitajitetea mwenyewe kuwa sijaiba,” kadinali huyo alinukuliwa akisema.
Akizungumza baadae na vyombo vingine vya habari , kardinali alisema kuondolewa kwake kumekuja kwa kushtukiza.
Alisema, Papa alikuwa na wakati mgumu sana kutoa taarifa hizo.
“Lilikuwa ni jambo la kushangaza hadi jana… nilihisi kuwa rafiki wa papa, mtu wa karibu wa papa anayemwamini.
“Mara Papa akaniambia hana imani nami tena kwa sababu amepokea ripoti kutoka mahakamani kuwa nilifanya vitendo vya ubadhilifu wa fedha.”
Kadinali Becciu amesisitiza kuwa “hakueleweka”, akaongeza kuwa: “Niko tayari kueleza kila kitu kwa papa. Sijafanya jambo lolote baya.”
“Nilimwambia papa kwanini anafanya hivi kwangu na mbele ya dunia nzima?”
Giovanni Angelo Becciu, ni raia wa Italia ambaye amekuwa akitumikia ofisi ya huduma ya diplomasia ya Vatican.
Kuanzia mwaka 2011 hadi 2018, kadinali Becciu alikuwa katibu mkuu wa Vatican, wakati alipopewa jukumu la kumsaidia papa na shughuli zake za kila siku.
Giovanni Angelo Becciu alipata ukadinali Juni, 2018
Ni papa Francis ndiye aliyempa ukardinali huo mwaka 2018, wakati alipochukua jukumu jipya la kusimamia idara inayoangazia maisha ya utakatifu.
“Ni mshtuko mkubwa kwangu na familia yangu na watu wa nchi yangu. Ninakubali kutii kutokana na upendo wangu wa kanisa na Papa,” vyombo vya habari vya Italia vilimnukuu Ijumaa wiki hii.