25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kampuni za simu zaagizwa kupanua wigo wa mawasiliano

Na Allan Vicent, Tabora

KAMPUNI za simu zimetakiwa kupanua wigo wa mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiana na serikali ili maeneo yote yenye changamoto za mawasiliano yafikiwe na huduma hiyo.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Waziri wa Habari, Mawasiliano  na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew katika hafla ya uzinduzi wa mnara wa mawasiliano ya simu ya kampuni ya Airtel iliyofanyika juzi katika Kijiji cha Magulyati kata ya Loya wilaya ya Uyui mkoani Tabora.

Alisema huduma za mawasiliano ya simu ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii, hivyo minara inapaswa kufikishwa katika maeneo yote ili kuchochea matumizi ya teknolojia ya kisasa yenye uwezo wa kutoa huduma ya mtandao.

Mhandisi Kundo alibainisha kuwa serikali ya awamu ya sita inatambua umuhimu wa kupeleka mawasiliano katika maeneo yote mjini na vijijini ikiwemo sehemu zenye mawasiliano hafifu na upelekaji huo wa huduma uendelee kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yanayofikiwa na huduma .

Aliwahakikishia kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango wa makampuni ya simu ndio maana inasisitiza kuyafikia maeneo yote yenye changamoto za usikivu zikiwemo ukosefu wa miundombinu wezeshi kama umeme na barabara.

“Tunataka huduma bora za mawasiliano katika maeneo yote, uwepo wa miundombinu ya kutosha utapunguza gharama za uendeshaji na changamoto ya mawasiliano iliyopo sasa kwa baadhi ya maeneo,” alisema.

 Alisema kuwa serikali inatambua umuhimu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) kwa kutoa ruzuku ambayo ni sehemu ya gharama ya miundombinu ya mawasiliano hivyo akawataka kutumia mfuko huo ili kuboresha huduma zao.

Mtendaji Mkuu wa Mawasiliano kwa wote Mwanasheria Justina Mashimba alisema serikali ilianzisha mfuko huo ili kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu, runinga na radio katika maeneo ya vijijini na mjini yenye usikivu hafifu.

 Alisema serikali imejenga mnara huo uliogharimu zaidi ya sh mil 300 kupitia mfuko huo kwa kushirikiana na kampuni ya Airtel ili kuhakikisha wakazi wa vijiji hivyo wanapata huduma ya mawasiliano ya simu.

 Aliongeza kuwa mfuko huo unaendelea kutekeleza miradi mingine 19 katika maeneo tofauti ya Mkoa huo ikiwemo wilaya hiyo ambayo itaanza hivi karibuni.

Mbunge wa jimbo la Igalula Wilayani humo, Venant Daud alimwomba Naibu Waziri na Mtendaji Mkuu wa UCSAF kufikisha mawasiliano ya simu katika maeneo mengine ili kuinua maisha ya wananchi.

Alibainisha kuwa mawasiliano ya simu yanachochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi kwa kuwa hurahisisha upatikanaji na kubadilishana habari kwa haraka .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles