25.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kampuni za simu kuingia DSE ifikapo Januari mwakani

mbarawaNA HADIA KHAMIS-DAR ES SALAAM

HAKUNA makali yasiyo na ncha na mwanzo wa ngoma ni lele, kwani baada ya giza jingi  ndio siku hucha.

Kwa miaka mingi sasa nchini Tanzania wawekezaji wazawa walikuwa hawaoni ndani katika biashara ya mawasiliano, kwani pamoja na biashara hiyo kuleta na kutengeneza faida kubwa, hakuna wazawa waliokuwa wanamiliki hisa za kampuni za simu.

Lakini mambo yako bayana sasa kuwa itakapofika Januari mwakani, kampuni za simu zitaanza kufungua milango kwa watu wa ndani kwa kuuza hisa zake za awali IPO, kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na hivyo kuleta ushindani wa kukata na shoka nchini kwani kampuni hizo zina mvuto na zinatengeneza faida kubwa.

Kampuni za simu ziko kubwa saba zikiwamo Milcom (Tigo), Vodacom Tanzania (Voda), Bharti (Airtel),  Etisalat (Zantel),  Agakhan Foundation (Smart) Vettel (Halotel) TTCL (TTCL Mobile); kampuni zote kwa ujumla wake zimekuwa zikishikilia hisa zake wenyewe bila ya kuhusisha wawekezaji wa ndani. Serikali ilipitisha sheria ya kuwataka wawe kampuni za umma (Public) badala ya binafsi ili wananchi wafaidike na uwekezaji huo, lakini umoja wao wa MOAT (Mobilephone Operators Association of Tanzania) ulipinga na kukubali mwaka huu kwenye enzi ya Dk. Magufuli, ambapo inasemekana waliambiwa wafunge virago kama hawataki kutoa hisa hizo.

Sheria zilitungwa mwaka 2010 na kuyataka makampuni hayo na yale ya madini kutoa hisa baada ya miaka mitatu ya utendaji kazi, lakini bila mafanikio katika utekelezaji Sheria.

Rekodi zinaonesha kuwa mwaka 2014 Oktoba, makampuni hayo yalisema yangetekeleza wito huo itakapofika 2015, lakini hawakufanya hivyo hadi mwaka huu ambapo vitisho vya Serikali vikafanya mabadiliko ya kutekeleza matakwa ya sheria.

Makampuni haya yanadai kuwa shida yao si ukaidi bali yanakwamishwa na mipangilio ya sheria na udhibiti wa kisheria unaowakabili bila kufafanua zaidi.

Kwa mujibu ya maelezo ya Ofisa Mtendaji  Mkuu wa DSE, Moremi Marwa, kuingia kwa hisa za kampuni hizo ni faraja kwa soko hilo kwani litakuza thamani ya soko na kina cha soko hilo na uwezo wake kipesa na hivyo kuongeza ukuaji wa soko la mitaji la nchi hii.

Soko la sekta ya mawasiliano lina wateja zaidi ya milioni 43 ambao ni sawa na ufikiaji wa asilimia 80 ya kampuni zile kubwa na hivyo kuwa na wateja zaidi ya milioni 38.

Soko la simu hukua kwa asilimia 24 kwa mwaka na Halotel inafikia wateja kwa asilimia 90 kufikia mwisho wa mwaka huu, baada ya kuwekeza zaidi ya dola milioni 104 na ameahidi kuwekeza kiasi hicho kila mwaka ili kukuza mtandao.

Kwa wenye makampuni kuruhusu uuzwaji hisa, ni kitendo kizuri na faraja na kufuta maneno na minong’ono kuwa hapa ni shamba la bibi watu kuja kuchuma tu na si kuneemesha wenyeji wa hapa.

“Hatua hiyo iliweza kutafsiriwa kwa kauli mbalimbali ikiwemo kuwa wamiliki wa kampuni za simu za mkononi wanataka faida peke yao,” anasema Juma Mselem, wakala wa simu za mkononi wa Sinza Kijiweni.

Pamoja na kuwepo kwa soko la hisa, bado kampuni nyingi zimeshindwa kupeleka hisa zao katika soko hilo ili kuwarahisishia wananchi kuweza kununua hisa hizo na kutajirika kwa pamoja.

Rekodi za IPO za  makampuni mbalimbali zinaonesha wazi kuwa kuna mahitaji makubwa ya umiliki hisa nchini, kwani mara nyingi mahitaji yalizidi kuliko uwepo wa hisa hizo sokoni (oversubscription), yaani wapo wananchi waliowengi wanaohitaji kununua hisa kutoka katika kampuni mbalimbali za mawasiliano.

Sekta ya mawasilianio ni sekta moja inayoendelea kukua kwa kasi duniani na kuchangia ukuaji wa kiuchumi Tanzania na hasa kupitia mpango wake wa kuweka na kusafirisha fedha ambao unafanya vizuri nchini na kufanya watu wanaofikika na huduma za kibenki kuchupa kutoka asilimia 18 mwaka 2014 hadi asilimia 75 mwaka huu.

Wawekezaji weliowekeza katika sekta hii wanapata faida kubwa sana, ukizingatia mpaka sasa tayari benki zimeweka mawakala wao kwa ajili ya kutoa huduma za kifedha.

Historia ya utekelezaji

Serikali baada ya kuliona hilo Machi 2010, ilipitisha muswada wa kuzitaka kampuni za simu kuuza hisa zao kwa umma, wamiliki wa kampuni za simu  baada ya miaka mitatu tangu kupita kwa sheria hiyo  zinatakiwa ziwe zimeorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Lakini Julai 2010, sheria ilifanyiwa marekebisho na kusomeka kwamba kampuni za simu zinaweza kuorodhesha hisa sokoni, baada ya kufanya mazungumzo au kushauriana na waziri husika mwenye  dhamana yaani Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Kampuni inapoingia sokoni, lengo kuu ni kupata mtaji kwa sababu tayari zimekuwa zimejitosheleza kwa kiwango kikubwa katika suala zima la mtaji, lakini teknolojia ya mawasiliano huhitaji kuboreshwa mara kwa mara. Hivyo mtaji bado unahitajika kwani simu ya leo si simu tu bali ni kila kitu. Simu ni ofisi, benki, tarishi, burudani, sinema na kila kitu.

Hisa ni sehemu ya umiliki wa kampuni. Hivyo hisa moja inawakilisha asilimia ndogo ya umiliki katika kampuni.

Kama kampuni ina hisa milioni moja na mwekezaji anamiliki hisa 10,000, mwekezaji huyu anamiliki asilimia moja  ya kampuni.

Mwekezaji anayenunua hisa basi ananunua haki ya kumiliki kampuni.

Stahili za mwenye hisa ni pamoja na kushiriki katika kutoa maamuzi ya kampuni katika mkutano mkuu wa wanahisa na kupata gawio litokanalo na faida kila mwaka kama ipo au katika kila baada ya miezi mitatu.

Ana haki pia ya kuuza hisa zake kwa faida pale ambapo kuna ongezeko la thamani ya hisa.

Kwa kutambua umuhimu wa sheria hiyo kwa kampuni za simu ya mkononi, MTANZANIA liliweza kufanya mahojiano na Ofisa Masoko Mwandamizi wa DSE, Marry Kinabo, ambaye anasema  kwa sasa tayari kampuni za simu zimefuata shauri la Serikali  la kujiunga na soko la hisa na yapo baadhi ambayo yameshaanza kufuatilia kwa kina.

Anasema kwa sasa bado ni mapema sana kusema kuwa wamiliki wa kampuni za simu za mkononi wamekaidi  shauri hilo kwa sababu wapo wengine walioko kwenye mchakato wa kujiunga na soko la hisa kama serikali ilivyoamuru.

“Kwa muda huu itakuwa mapema sana kusema wamekaidi shauri hilo kwa sababu kuna ambao wako kwenye mchakato, tusubiri angalau Januari mwakani ambapo watakaokuwa bado hawajajioredhesha ndipo watakuwa wamekaidi shauri hili na tutaweza kuwataja,” anasema Marry.

Jee soko la hisa ni nini?

Anasema soko la hisa ni soko ambalo huwezesha hisa kutofungana na dhamana nyingine zilizoorodheshwa katika soko hilo kuuzwa na kununuliwa.

Anasema bidhaa hizo huitwa dhamana au kwa lugha ya Kiingereza (securities). Soko la Hisa hapa Tanzania limeanzishwa mwaka 1996 kama kampuni binafsi yenye dhima (limited by guarantee); kwa maana kwamba wanachama wa soko hawatakiwi kuweka mtaji wowote.

Anasema  mwanzoni kulikuwa na wanachama 11 ambao ni madalali wa soko la hisa pamoja na wawekezaji wakubwa (Institutional investors). Soko la hisa lilianza kazi zake rasmi Aprili mwaka 1998 wakati hisa za TOL Ltd zilipoorodheshwa na kuanza kuuzwa na kununuliwa.

Soko la hisa ni soko ambalo linajiendesha lenyewe likisimamiwa na Baraza la Wadhamini (DSE Council). Kwa sasa lina wanachama 27.

 

 Ni ipi faida ya kuwekeza kwenye hisa, hatifungani na vipande?

 

Marry anasema kwa ujumla dhamana za fedha (hisa, hatifungani, vipande) ni rasilimali ambazo zinagawanyika na ni rahisi kuziuza. Kutokana na urahisi huo, dhamana zinaweza kuwekwa rehani kwa ajili ya kupata mkopo kutoka taasisi za fedha.

“Wawekezaji kwenye hisa wanapata gawio ikiwa kampuni itakuwa imepata faida. Wanahisa pia huweza kupata faida itokanayo na ongezeko la thamani iwapo bei ya hisa itaongezeka kwenye soko la hisa.

Ongezeko la thamani ni tofauti na bei ya kununulia hisa na bei ya kuuzia. Ikiwa bei ya kuuza ni ndogo kuliko bei ya kununulia, mwanahisa anapata hasara.

Uwekezaji kwenye hisa hauna uhakika wa gawio kwa sababu gawio linategemea faida ya kampuni,” anasema Marry.

Anasema  hatifungani, riba inayolipwa inajulikana tangu mwanzo kwa sababu ni asilimia ya deni lote. Riba inayolipwa inaweza kuwa ya kubadilika badilika au isiyobadilika.

Anasema wawekezaji kwenye hatifungani wanaoamua kukaa nazo hadi zitakapopevuka wanajua kiwango cha faida yao tangu wanapowekeza.

Anasema kwa upande wa vipande, faida inategemea aina ya mpango. Vipande ni sehemu ya umiliki kwenye mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

Anasema vipande ni tofauti na hisa kwa sababu vinajumuisha mseto wa uwekezaji wa vitega uchumi mbalimbali ambavyo fedha zikikusanywa kwa ajili ya uwekezaji wa pamoja zinawekezwa.

Anasema zinawekezwa kama ni mpango wa kukua, mwekezaji anategemea kufaidika kutokana na kukua kwa thamani ya vipande. Wawekezaji wanatakiwa kujua kuwa bei ya vipande inabadilika mara kwa mara. Kama mpango wa uwekezaji wa pamoja ni wa mapato, mwekezaji anafaidika kutokana na mgao wa mapato ya mpango huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles