22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Kampuni 500 kushiriki maonesho SADC

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

ZAIDI ya kampuni 500 zimethibitisha kushiriki maonesho ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) yanayotarajiwa kufanyika nchini Agosti 5 hadi 9.

Maonesho hayo ni miongoni mwa shughuli zinazotarajiwa kufanyika kuelekea mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo ambao Rais Dk. John Magufuli atakabidhiwa uenyekiti kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Akizungumza jana, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alisema hadi juzi waliojiandikisha walikuwa 531 na kati ya hao Watanzania ni 158 na wengine wanatoka nchi mbalimbali za SADC.

“Bado makampuni yanaendelea kujisajili na kuna uwezekano idadi ikafika 1,000.

“Ni heshima kubwa kwa nchi yetu kuwa mwenyeji wa mkutano wa SADC, hivyo Watanzania na wenye viwanda wachangamkie fursa hii kwa sababu tuna rasilimali nyingi kulinganisha na nchi nyingine,” alisema Bashungwa.

Alisema pia washiriki wa mkutano huo watapata fursa ya kutembelea Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZ) kujionea viwanda vilivyopo na kujifunza kupitia mazuri yaliyofanywa na Tanzania.

Kwa mujibu wa Bashungwa, Wiki ya Viwanda itafunguliwa na Rais Magufuli na kufungwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Katika hatua nyingine, waziri huyo alisema wanatarajia kupitia sheria na sera zote zinazoathiri utekelezaji wa biashara kuiwezesha Tanzania kufanya vizuri biashara katika nchi za SADC na zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema muswada wa marekebisho ya sheria hizo unatarajiwa kuwasilishwa wakati wa Bunge la Septemba ili kuongeza ufanisi na kuifanya Tanzania kuwa sehemu rafiki ya kufanya biashara, kujenga uchumi wa viwanda na kuvutia uwekezaji.

“Tunapitia sera zilizopitwa na wakati, mfano SME Policy (Sera inayohusu wajasiriamali wadogo na wa kati) ni ya mwaka 2003, inatakiwa ifanyiwe marekebisho kubeba kiu ya Tanzania ya Viwanda.

“Ukizungumzia kwenda kwenye uchumi wa kati na viwanda, lazima tuangalie wafanyabiashara na viwanda vidogo kwa sababu huko ndiko Watanzania wengi waliko,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles