23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa awataka wakurugenzi kufanya tathmini ahadi za JPM

BENJAMIN MASESE-MWANZA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakurugenzi wote nchini kufanya tathmini kwa kila halmashauri kwa kupitia ahadi zote za Rais Dk. John Magufuli alizozitoa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alitoa agizo hilo jana jijini Mwanza wakati akifungua mkutano wa 35 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat).

“Rais wetu Dk. Magufuli anafanya kazi kubwa kweli kweli, ikumbukwe mwaka huu ni wa nne tangu ameingia madarakani, sasa naomba kila halmashauri ipitie ahadi alizozitoa wakati akiomba kura alipopita halmashauri zetu, fanyeni tathmini na andaeni ripoti inayoonesha zile zilizotekelezwa.

“Sote tunajua Rais wetu anarudi kwa wananchi ifikapo 2020 kuomba ridhaa tena, hivyo ikiwa atapata ripoti hizi itamsaidia kwa kipindi hiki kujua ahadi zilizobaki na kuzitekeleza, najua tunapozunguka sisi tumebaini moja ya changamoto iliyobaki kubwa ni upungufu wa madaktari na walimu,” alisema.

Alieleza kushangazwa kwa kitendo cha baadhi ya watu kumsimanga Rais Magufuli anapoibua miradi mbalimbali huku akiwataka kuacha tabia hiyo.

Akijibu maombi ya risala ya Alat iliyosomwa na Mwenyekiti wake, Gulamhafeez Mukadam, alisema mwaka huu ni wa uchaguzi, hivyo aliwaagiza wakurugenzi kuendelea kuratibu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuhamasisha wananchi kujiandikisha.

Aliwataka wenyeviti wa halmashauri na wakurugenzi kusimamia miradi ya maendeleo huku akishangazwa na namna baadhi ya majiji nchini yalivyoshindwa kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo.

Alisema Serikali haijafanya kosa kukusanya fedha zote katika mfuko mmoja kwani walifanya tathmini na kuona ni heri fedha ikatunzwa eneo moja.

“Tumeelekeza kila halmashauri kubuni mradi wa kimkakati na kutuletea kwa ajili ya kuwapa fedha, lakini baadhi ya wakurugenzi wameshindwa kufanya hivyo, hawajui hata kuandika andiko, wakiandika wakileta linatupwa, sasa kama hamjui kutetea kile unachokitaka kuanzisha ni heri ukakodi mtu akuandikie.

“Mpaka sasa halmashahuri 17 zimekidhi matakwa katika miradi 22, hawa tunawapa mabilioni ya fedha ili kuanzisha miradi ya kimkakati, awamu ya pili halmashauri 12 zimeonekana kukidhi vigezo, nazo zitapewa.

“Ndiyo maana inafikia hatua Rais Magufuli anakuwa mkali kwenu, hasa kwa wale wanaofuja fedha, naomba kila halmashauri ipange mipango ya maendeleo,” alisema.

Alizitaka halmashauri kumi za mwisho zilizotajwa kwa kushindwa kukusanya mapato na kufikia asilimia 80 zijitathmini.

Awali, Mwenyekiti wa Alat, Mukadam, alisema moja ya changamoto kubwa inayowakabili ni posho ndogo na kiinua mgongo cha madiwani.

Pia aliomba kufanyika kwa mgawanyo wa kata, vijini na mitaa kwani baadhi ya maeneo ni makubwa sana jambo ambalo linaleta changamoto kwa viongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles